RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kimkakati wa Zanzibar Sports City unaoendelea katika eneo la Fumba, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michezo ya AFCON 2027.
Akiwa katika ziara hiyo, Dk. Mwinyi aliihakikishia Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo pamoja na Kampuni ya ORKUN GROUP, inayotekeleza mradi huo, kuwa Serikali imejitokeza kikamilifu kuhakikisha ujenzi unakwenda kwa kasi, ufanisi na uzingatiaji wa viwango vya kimataifa. Alisisitiza umuhimu wa changamoto zote zinazojitokeza kuwasilishwa mapema ili Serikali iweze kutoa ufumbuzi wa haraka.

Rais Mwinyi aliambatana na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo,Riziki Pemba Juma, pamoja na Naibu Waziri, Ali Abdulgullam Hussein, katika ziara iliyofanyika leo,Novemba 18. Mradi wa Zanzibar Sports City ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya michezo na kuchochea maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Awamu ya kwanza ya mradi huo inahusisha ujenzi wa Uwanja wa Kimataifa wa Mpira wa Miguu wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 36,500 pamoja na viwanja viwili vya mazoezi vyenye uwezo wa kubeba mashabiki 15,000 kila kimoja. Moja ya viwanja hivyo kimepangwa pia kutumika kwa sherehe za Kitaifa. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2026. SOMA: Makalla akagua uwanja wa AFCON , ujenzi wafikia 60%