Mke ajiteka kumtapeli mumeMke ajiteka kumtapeli mume

JESHI la Polisi Mkoani Tabora linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kutengeneza taarifa za uongo kuhusu kutekwa kwa mwanamke aitwaye Adijaji Jimmy (39), mkazi wa Mkoa wa Tabora, kwa lengo la kujipatia fedha kutoka kwa mzazi mwenzake Emmanuel Peter ambaye ni mwanajeshi mstaafu.

Watuhumiwa wengine ni Ashura Swalehe (48) na Vitus Joseph (34) ambao wanadaiwa kushirikiana kupanga na kusambaza simulizi la utekaji huo. SOMA: Polisi Songwe kuimarisha ulinzi uchaguzi mkuu

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Abwao, watuhumiwa hao wamedai kuwa Adijaji alitekwa katika Kijiji cha Vumilia, Wilaya ya Urambo, na kuwataka ndugu zake kutuma fedha ili kumuokoa. Kupitia taarifa hizo za uongo, walifanikiwa kupokea kiasi cha Sh 1,850,800 zilizotumwa moja kwa moja kwenye simu ya Adijaji.

Hata hivyo, uchunguzi wa polisi umebaini kuwa Adijaji hakutekwa, bali alisafiri kwenda Urambo kwa hiari yake, huku fedha walizotumiwa zikitolewa katika maeneo ya Wilaya ya Kaliua baada ya watuhumiwa kukodisha pikipiki na kwenda kuzitoa kabla ya kurejea Urambo.

Kamanda Abwao amesema watuhumiwa wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya uchunguzi na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa mara taratibu zitakapokamilika. Amesisitiza kuwa hakuna tukio lolote la utekaji lililoripotiwa mkoani Tabora na kwamba upotoshaji wa aina hiyo unaweza kuleta hofu isiyo ya lazima kwa wananchi.

Aidha, ametoa onyo kwa watu wanaotengeneza taarifa za uongo, akibainisha kuwa jeshi hilo lina wataalamu wa upelelezi wenye uwezo wa kubaini ukweli wa matukio yote yanayoripotiwa. Kuhusu madai kuwa tukio hilo lilitokana na mgogoro wa kifamilia, Kamanda Abwao amesema jeshi la polisi halijathibitisha taarifa hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *