Serikali yaita wadau kuchangia nishati safiSerikali yaita wadau kuchangia nishati safi

SERIKALI imeomba wadau wa maendeleo waendelee kuchangia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais, Profesa Peter Msoffe ametoa mwito huo aliposhiriki uzinduzi wa mpango wa nishati safi ya kupikia shuleni unaolenga kuwezesha taasisi za elimu kutumia nishati safi ya kupikia.

Uzinduzi huo ulifanyika pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.

SOMA: Wadau watoa elimu nishati safi ya kupikia

Profesa Msoffe alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira ya dhati ya kuwezesha upatikanaji wa nishati hiyo.

Alisema Rais Samia amekuwa akihamasisha ‘Ajenda 300’ inayolenga kupeleka umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030 kuwezesha wananchi kutumia umeme wa gharama nafuu na kuacha kutumia nishati isiyo rafiki kwa mazingira.

Profesa Msoffe alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili kumuwezesha kila Mtanzania kumudu.

Alisema serikali imetoa maelekezo kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuacha kupika kwa kuni na mkaa na inaendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia.

Alisema inatarajiwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Alishukuru wadau wa maendeleo likiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula (WFP) kwa kuanzisha programu ya nishati safi kupitia kwenye shule akisema Tanzania itaendelea kuwapa ushirikiano.

Profesa Msoffe alisema mpango huo si tu unaziwezesha shule kupata nishati safi ya kupikia bali pia unawajenga wanafunzi wawe mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii.

Mshauri wa Masuala ya Nishati wa WFP Tanzania, Geofrey Ndegwa alisema shule ni sehemu muhimu ya kuwekeza ajenda ya nishati safi ya kupikia kwa kuwa wanafunzi wanapata ufahamu kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati hiyo.

Ndegwa alipongeza juhudi za serikali za kuhakikisha taasisi zote za elimu zinazohudumia idadi kubwa ya watu (zaidi ya 100) zinatumia nishati safi ya kupikia kwa kuwa zikitumia kuni na mkaa, miti mingi itakatwa.

Alitoa mwito kwa serikali ishirikiane na wadau ikiwemo WFP kuhamasisha ajenda ya nishati safi ya kupikia katika shule zote.

Profesa Ed Brown kutoka programu ya Moden Energy Cooking Service alisema kuna fursa katika kuwezesha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kupata nishati safi ya kupikia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *