MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameagiza wadau wanaotoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka kuhakikisha kesho huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka (mwendokasi) inarejea katika barabara ya Mbagala.
Wadau hao ni Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na taasisi nyingine za serikali zinazohusika kuratibu kwa pamoja chini ya Katibu Tawala wa Mkoa.
Chalamila alitoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua na kufanya tathmini ya uharibifu wa miundombinu uliofanywa Oktoba 29, mwaka huu.
“Naagiza taasisi tajwa kuhakikisha kuanzia siku ya Alhamisi (kesho) saa 2:00 asubuhi au kabla, mabasi yote ya mwendokasi yarejee na kuanza kuchukua abiria katika barabara ya Mbagala kuelekea mjini,” alisema Chalamila.
Alisema juhudi zinaendelea kuhakikisha barabara ya Gerezani kuelekea Kimara inaanza kutoa huduma haraka iwezekanavyo, kwani matengenezo yanaendelea na vifaa vimeagizwa na vitatumika kukamilisha marekebisho hayo.
Chalamila alibainisha kuwa uharibifu huo ni hasara kubwa kwa serikali na kusisitiza kwamba hakuna chanzo kingine cha kupata fedha za ukarabati zaidi ya kodi za wananchi.
“Kuna Watanzania wema ambao ni mabalozi wa amani, lakini wapo wachache ambao wakichukia wanaona wachukue jiwe au kulipua kitu. Ukilipua kila kitu utaishije?
Tugombane tunavyoweza kugombana, lakini kamwe tusidhuru miundombinu inayoweza kusaidia vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.
Aidha, aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kusimamia na kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo ili kulinda miundombinu hiyo.
