STRAIKA Prince Dube amemaliza ukame wa kucheza bila kufunga bao tangu alipofanya hivyo Septemba 19  baada ya juzi kufunga bao muhimu lililoipa ushindi Yanga dhidi ya AS FAR Rabat, huku ikifichuka, jamaa alitaka asicheze mechi hiyo kabla ya wenzake kumrudisha mchezoni.

Dube alifunga bao lililoifanya Yanga kulivua joho ya unyonge kwa mechi za kwanza za makundi ya CAF tangu 2016, lakini kabla ya mechi hiyo Mzimbabwe huyo aliikata mechi hiyo akitaka apewe Andy Boyeli, ila wenzake walimkomalia na kocha Pedro Goncalves akamuanzisha.

Mmoja wa mabeki wa Yanga, amesema kauli ya Dickson Job kwamba katika mechi hiyo mashabiki watamuona Dube mpya haikuja kwa bahati mbaya, kwani walipambana kumrudisha mchezoni straika huyo baada ya kuomba asianzishwe.

Beki huyo alifichua kuwa, Dube alikuwa katika presha kubwa, akiwataka wenzake kuacha straika mwenzake, Andy Boyeli kucheza mechi hiyo kwa vile alitoka kufunga mabao mawili katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC wakati Yanga ikishinda 4-1.

DUB 01

Tangu kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu, Dube alikuwa hajafunga bao lolote zaidi ya lile la mechi ya kwanza ya raundi ya awali dhidi ya Wiliete Benguela wakati Yanga ikishinda ugenini 3-0 Septemba 19 na juzi alifunga bao la ushindi dhidi ya FAR Rabat dakika ya 57.

“Dube ni kati ya wachezaji waungwana sana, wakati tunajiandaa na hii mechi (dhidi ya AS FAR Rabat), alikuwa anakwenda kuomba huu asianze, alianza kwa kuwafuata manahodha akiwaomba wamuambie kocha kwamba aanzie benchini,” amesema beki huyo na kuongeza;

“Hata hivyo, manahodha walimgomea na sababu ya Dube ilikuwa moja tu alitaka aanze Boyeli ambaye alitoka kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa mwisho, bahati nzuri wakampa moyo wakamwambia asikatae kuanza kama makocha wakitaka aanze.

“Waliongea naye sana nakumbuka nilimsikia Job (Dickson Job) akimwambia kwamba tena akicheza anaweza kufunga na Dube akatoka ameelewa, nadhani mliona kwenye mkutano wa waandishi wa habari Job amesema mtamuona Dube mpya sasa kauli ile ilianzia hapo.

DUB 02

Kiungo mmoja aliyeanza mchezo huo aliongeza kuwa licha ya ukame wa kutokufunga kwenye mechi lakini Dube ni mmoja kati ya wachezaji wanaofanya vizuri mazoezini ambapo ni vigumu kwa kocha kumuacha nje hata kama anakosa kufunga.

“Sina maana kwamba wengine hawafai, hapana, lakini sisi ni wachezaji tunajuana, ukimuuliza yeyote kwamba kwanini kocha anaanza na Dube atakushangaa, ukija mazoezini utajua kwanini makocha wanaanza naye.

“Dube ni vile tu amekutana na ukame ni mshambuliaji mzuri sana hata Boyeli, Dube anafanya vizuri mazoezini na hata kwenye mechi ana mchango mkubwa sana uwanjani zile movement zake zina faida kubwa sana kuwafanya wale mabeki wasimuache.”

DUB 03

KOCHA MTABIRIA

Kwa upande wa kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema anaamini baada ya Dube kufunga dhidi ya FAR Rabat, basi mabao mengi zaidi yatakuja kutoka kwa mshambuliaji huyo.

Dube anayeitumikia Yanga kwa msimu wa pili, alifunga juzi na kumfanya afikishe mabao mawili katika michuano ya CAF na kitendo hicho kilimfanya kocha Pedro kusema mchezaji huyo ni kati ya wale wanaojua majukumu yao uwanjani ya kukaa sehemu sahihi, lakini anahukumiwa kwa kitu kimoja tu, kupoteza nafasi nyingi za kufunga.

“Kuhusu Dube, huwa anatupa mchango mkubwa sana. Ana mbinu nzuri sana, anaelewa nafasi yake uwanjani vizuri. Ni kweli, labda alikuwa amepoteza ujasiri kidogo, lakini nilizungumza naye, nikamsisitiza aendelee kupambana na kujiamini, kwa sababu anafanya vizuri, na mambo hayo hutokea,” amesema Pedro na kuongeza;

“Leo (juzi Jumamosi) alicheza vizuri sana, na natumai hili bao litamhamasisha kuendelea kufanya vizuri zaidi na mengi zaidi yatakuja kwa sababu tunamtegemea sana kama ilivyo kwa wachezaji wote.

“Nampongeza Prince, ilikuwa ngumu msimu huu kwa sababu ya ushindani uliopo miongoni mwa wachezaji,” amesema kocha huyo raia wa Ureno.

Katika mechi hiyo ya juzi, Dube ndani ya dakika saba za kwanza alipata nafasi tatu ambazo zote za hatari, lakini hakuweza kuzitumia kuitanguliza Yanga.

Dube ameanza kikosini katika mechi zote tatu chini ya Pedro tangu kocha huyo Mreno atue Yanga ambapo waliikabili Mtibwa, KMC na FAR Rabat. Msimu uliopita katika Ligi Kuu Bara, Dube alimaliza na mabao 13, matatu nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua wa Simba aliyekuwa na 16 akifuatiwa na Clement Mzize (14).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *