WAKATI mashabiki wa Simba wakiendelea kusonya huko mtandaoni kutokana na matokeo ya kipigo cha bao 1-0 ilichopewa timu hiyo, straika wa Wekundu hao, Jonathan Sowah wamewatuliza mashabiki kwa kuwaambia: ‘Tumewasikia na mtafurahi mechi zijazo’.
Simba ilikumbana kipigo hicho cha mechi ya ufunguzi wa Kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka kwa Petro Atletico ya Angola kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku mashabiki wakilitupia lawama benchi la ufundi kuwaanzisha benchini mastraika wote watatu.
Katika mechi hiyo inayokuwa ya kwanza kwa Simba kupoteza nyumbani katika michuano ya CAF tangu Februari 18, 2023 ilipocharazwa 3-0 na Raja Casablanca, makocha Dimitar Pantev na Seleman Matola walianzisha kikosi cha kwanza bila ya mshambuliaji wa kati asilia baada ya Sowah, Steven Mukwala na Seleman Mwalimu ‘Gomes’ kuachwa nje ya kikosi cha kwanza.
Jambo hilo liliwakera mashabiki ambao pia waliwatupia lawama wachezaji kwa kutojituma vyema uwanjani na kuamini imechangia kupoteza mbele ya Petro inayoongoza msimamo wa Kundi D, ikifuatiwa na Esperance ya Tunisia na Stade Malien ya Mali zenye pointi moja kila moja, huku Simba ikiburuza mkia bila ya pointi na ikijiandaa kuifuata Malien ugenini wikiendi hii.
Hata hivyo, straika Sowah aliyeingizwa kipindi cha pili, amewatoa hofu mashabiki kwa kuwaambia wamepoteza kwa bahati mbaya tu na kwamba bado anaamini wana nafasi ya kurekebisha makosa kupitia mechi zijazo za kundi hilo ikiwamo ile ya Ijumaa dhidi ya Malien.
Akizungumza na Mwanaspoti Sowah alisema, baada ya mechi hiyo ya juzi, wachezaji wamewasikia mashabiki na wapenzi wengi wakilia na kulaumu kiwango kibovu kilichoonyeshwa na timu na kuwaambia ni kweli wana haki kwa vile timu imepoteza, lakini hiyo haimaanishi kuwa wameshatolewa.
“Hata mimi kama mchezaji, nimeumia sana kupoteza nyumbani, sawa na ilivyo kwa wachezaji wote na wanasimba kwa ujumla. Sio kitu kinachoweza kupita kirahisi, nikiangalia mashabiki wanakosa raha, tupo hapa kupigania furaha yao lakini wanaikosa, inaumiza sana,” alisema Sowah na kuongeza;
“Kilichotokea kila mtu ameona, sitaki kuongea sana. Hatukustahili matokeo kama haya, hata hivyo bado tuna nafasi na wajibu wetu, tunatakiwa kubadilika kwa haraka. Kwa sasa natamani kupata muda zaidi wa kucheza, hiki ndicho kimenileta hapa, wachezaji tumeumizwa na matokeo haya, lakini hatupaswi kukata tamaa tuna mechi nyingine tano za makundi.”
Sowah mwenye mabao mawili katika Ligi Kuu, huku akiwa na rekodi ya kufunga mabao 14 kupitia mechi 15 za msimu uliopita za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA), licha ya kiwango alichonacho, amekuwa akianzia benchini mara nyingi katika mechi za kimataifa na katika ligi ni mechi moja tu alitumika kwa dakika 90 dhidi ya Fountain Gate.
Simba inajiandaa kuifuata Stade Malien ya Mali kwa ajili ya mechi ya pili ya Kundi D kisha kusubiri mwishoni mwa Januari na mwanzoni mwa Februari mwakani kuvaana na Esperance ya Tunisia katika mechi mbili mfululizo za kundi hilo, ikisaka nafasi ya kutinga robo fainali.