BAADA ya kuvuna pointi tatu dhidi ya waajiri wake wa zamani wa Mbeya City, kocha wa Mashujaa, Salum Mayanga amezisifu timu pinzani na kuwakingia kifua washambuliaji kwa kuzipa timu zao ushindi wa mabao kiduchu.
Mayanga amefunguka hayo baada ya Jumamosi kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City akiweka wazi kuwa ubora wa safu ya ulinzi ya timu pinzani ndio uliowanyima ushindi wa mabao mengi.
“Tuwasifu wapinzani pia. Ukifuatilia msimu huu ushindi mkubwa ni mabao mawili (ukiacha mechi chache ambazo timu zimeshinda kwa mabao matatu na moja pekee ya Yanga iliyoshinda 4-1 dhidi ya KMC). Huwezi kusema washambuliaji ni wabovu hapo sifa ziende kwa mabeki na makipa ambao wamekuwa wakizuia kuhakikisha timu pinzani hazipati mabao,” amesema Mayanga na kuongeza;
“Mechi yetu iliyopita dhidi ya Mbeya City haikuwa, rahisi ulikuwa ngumu nimekutana na timu tofauti na niliyoifundisha, ilikuja na mbinu tofauti. Nawapongeza wachezaji wangu walikuwa bora tukapata ushindi.”
Mayanga amesema ubora wa Ligi Kuu msimu huu ndio imekuwa changamoto kwa timu nyingi kushinda kwa zaidi ya mabao matatu tifauti na misimu miwili nyuma ambapo timu zilikuwa zinashinda mabao matano na zaidi.
“Ugumu huo haina maana kwamba timu hazifungiki. Ni kazi zetu makocha kutafuta mbinu mbadala ambazo zitafungua ngome za wapinzani. Hili nitalifanyia kazi kabla ya kukutana na mpinzani mwingine.
“Washambuliaji pia wana kazi kubwa kuhakikisha wanazishinda mbinu za wapinzani ili kuweza kupata ushindi wa zaidi ya mabao mawili.”
Mashujaa kwa sasa ipo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 11 kutokana na mechi saba na inajiandaa kuipokea Dodoma Jiji Ijumaa hii pale Lake Tanganyika, Kigoma.