Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya mbio za baiskeli yanayolenga kukusanya zaidi ya Sh100 milioni kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wanaotoka katika mazingira magumu mkoani Dodoma.
Mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza jijini Dodoma, yameandaliwa mahsusi kuunga mkono juhudi za kuinua elimu katika kaya zenye kipato duni, sambamba na kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo.
Akizungumza leo Jumatatu Novemba 24, 2025 jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Meneja wa Springhill Academy, Caren Billington, amesema lengo kuu la mbio hizo ni kuhakikisha watoto wenye uhitaji wanapata nafasi sawa ya kufikia elimu bora bila vikwazo vya kiuchumi.
“Tunataka kuona kila mtoto, bila kujali mazingira anayokulia anapata nafasi ya kusoma, kukua na kutimiza ndoto zake. Kiasi tunachotarajia kukusanya kitaelekezwa moja kwa moja katika mahitaji ya kielimu kwa watoto kutoka kaya duni,” amesema Billington.
Kwa upande wake, Balozi wa Springhill Academy, Vicent Njau ‘Kiredio’, ametoa wito kwa wananchi, wadau wa elimu na wapenda michezo kujitokeza kwa wingi kushiriki au kuchangia kupitia mashindano hayo.
“Hili ni tukio la kijamii. Ushiriki wenu utaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watoto ambao leo hii wanateseka kupata haki yao ya msingi elimu,” amesema Kiredio.
Mashindano hayo ya mbio za baiskeli yanatarajiwa kufanyika Novemba 29, 2025 katika barabara za Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma, na yamepewa matumaini makubwa ya kuvutia washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini.