AZAM FC tayari ipo Zanzibar ikijiandaa kuikaribisha Wydad Athletic kutoka Morocco katika mechi ya pili Kundi B la Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza mechi ya kwanza ugenini kwa mabao 2-0 mbele ya AS Maniema.

Kuelekea mechi dhidi ya Wydad itakayochezwa Ijumaa Novemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Kocha Mkuu wa Azam, Florent Ibenge amewapa maujanja wachezaji namna ya kutamba Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema, licha ya kwamba wamepoteza ila ni mapema kwa mastaa wa kikosi hicho kukata tamaa.

Alisema kuwa, mechi za hatua ya makundi haziwezi kuwa rahisi kwani hapo ndipo ndoto za timu nyingi zilipo, hivyo wanatakiwa kuhakikisha wanatumia nafasi ili kuwa bora.

“Nimewaambia wachezaji kama wanataka watambulike kwa ukubwa Afrika ni lazima wacheze kwa kujitolea mechi za makundi.

“Lakini pia wanatakiwa kuzichukulia kwa uzito mechi za hatua ya makundi ambazo hazitakuwa rahisi kama zile za hatua ya mtoano,” alisema Ibenge.

Kocha huyo aliongeza kuwa: “Kila mchezo wanatakiwa kuhakikisha wanatumia nafasi na hata maamuzi hayatakuwa rahisi hasa mechi za ugenini.

KUHUSU WYDAD

Ibenge alisema kuwa, mechi inayofuata ya nyumbani, wanakwenda kukutana na timu ngumu zaidi.

“Tumerudi nyumbani, tunakutana na timu ngumu ya Wydad, lakini lazima tujipange kushinda na tunatakiwa kama makamanda tusiache nafasi,” alisema kocha huyo.

“Kuna maeneo tunatakiwa kuwa imara zaidi, kama ukuta kwa akili kubwa lakini pia hata kama Wydad itafanya makosa kwenye ukuta wao hayatakuwa ya kujirudia kutokana na ubora mkubwa walionao.”

Azam itakuwa nyumbani kuwakaribisha Waarabu hao kutoka Morocco, ikiwa ni mechi ya pili hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika.

Ikumbukwe kuwa, Wydad imetoka kukutana na Nairobi United, Novemba 23, 2025 na kuitandika mabao 3-0, ikiwa uwanja wa nyumbani nchini Morocco, Stade Mohammed V uliopo Casablanca.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *