KIUNGO wa Namungo, Abdulkarim Kiswanya amesema kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha timu hiyo si jambo jepesi kutokana na ubora wa nyota waliopo.

Kiswanya ambaye anaitumikia Namungo kwa mkopo akitokea Azam FC ambayo alipandishwa timu ya wakubwa msimu huu kutokea ile ya vijana chini ya miaka 20, alisaini mkataba wa miaka mitano utakaotamatika 2030 ndani ya Azam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kiswanya alisema kila anapopata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kocha Juma Mgunda, anajitoa kweli kweli ili kujihakikishia namba.

Aliongeza kuwa, kama kijana anayeanza kuchipukia ni hamasa na fursa kwake kujiuza hivyo kila nafasi kwake ni dhahabu kufanya kazi ya maana.

“Inanipa hamasa sana kupewa nafasi ya kuanza mbele ya wachezaji wengi wa kimataifa, kila kocha anaponipa maelekezo najitahidi kufuata ili angalau aendelee kuniamini na kunipa nafasi,” alisema Kiswanya na kuongeza. “Mimi sijawahi kucheza ligi kuu, Namungo ndiyo timu ya kwanza kuitumikia, kutoka timu ya vijana hadi kupewa nafasi hapa ni wazi fursa kwangu kuonyesha kile nilichoaminiwa na naamini naweza kutimiza malengo yangu.”

Hivi karibuni, kiungo huyo alipata nafasi ya kwenda QPR inayoshiriki Championship nchini England kufanya majaribio ambapo mwenyewe amezungumzia hilo na mustakabali wake akisema: “Ni kweli lakini nilipomaliza majaribio nilirudi kuendelea kucheza Namungo, sasa sijajua kinachoendelea baina ya viongozi wa Azam na QPR ambao walikuwa na mazungumzo.”

Kwenye ligi kuu msimu huu, kiungo huyo amecheza mechi tano kwa dakika zote 90, kati ya saba ilizocheza Namungo iliyoko nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi na pointi tisa ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *