SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeufungia Uwanja wa Mkwakwani uliopo Tanga kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo, leo Jumatano Novemba 26, 2025, imesema miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu.

“Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia uwanja mwingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka uwanja wao utakapofunguliwa, baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.

“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja,” imeeleza taarifa hiyo.

Uamuzi wa kuufungia uwanja huo umekuja muda mchache baada ya kumalizika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo wenyeji Coastal Union imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City.

Kufungiwa kwa Uwanja wa Mkwakwani, inailazimisha Coastal Union inayoshiriki Ligi Kuu Bara na African Sports ya Ligi ya Championship kutafuta viwanja vingine kwa ajili ya mechi za nyumbani.

Tangu kuanza kwa msimu huu 2025-2026, huu unakuwa uwanja wa nne kufungiwa na TFF kwani Oktoba 15, 2025, viwanja viwili vilifungiwa ambavyo ni Sokoine uliopo Mbeya na Liti wa Singida. Kabla ya hapo, Septemba 20, 2025 iliufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi unaopatikana mkoani Tabora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *