
Uchambuzi wa hivi karibuni wa takwimu uliofanywa kwa ushirikiano wa UNICEF na shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi, UNAIDS unaonyesha kuwa, endapo ufikiaji wa programu utapungua kwa nusu, watoto wengine 1.1 milioni wanaweza kuambukizwa VVU, na 820,000 zaidi wanaweza kufariki kutokana na sababu zinazohusiana na UKIMWI kufikia mwaka 2040 na hivyo kusukuma jumla ya maambukizi miongoni mwa watoto hadi milioni 3 na vifo vinavyohusiana na UKIMWI hadi milioni 1.8.
Hata kudumisha kiwango cha huduma kilichopo sasa bado kitasababisha maambukizi mapya milioni 1.9 na vifo 990,000 vinavyohusiana na UKIMWI miongoni mwa watoto kufikia mwaka 2040 kutokana na kasi ndogo ya maendeleo, kwa mujibu wa uchambuzi huo.
“Dunia ilikuwa inapiga hatua katika kukabiliana na VVU, lakini mapengo yalibaki hata kabla ya kupunguzwa ghafla kwa ufadhili wa kimataifa ambao uliathiri huduma,” anasema Anurita Bains, Mkurugenzi Msaidizi katika shirika la UNICEF anayehusika na VVU na UKIMWI. “Ingawa nchi zilichukua hatua za haraka kupunguza athari za kupunguzwa kwa ufadhili, kutokomeza UKIMWI kwa watoto sasa kuko hatarini bila hatua makini. Uamuzi uko wazi tuchangie leo au tukubali kurudisha nyuma maendeleo ya miongo kadhaa na kupoteza mamilioni ya maisha ya vijana.”
Hatari hizi zilizotabiriwa zinaendana na matokeo kutoka takwimu za kimataifa za 2024, kabla ya kupunguzwa ghafla kwa ufadhili kuathiri huduma nyingi duniani:
- Watoto 120,000 (wenye umri wa miaka 0–14) waliambukizwa VVU, na wengine 75,000 walifariki kutokana na sababu zinazohusiana na UKIMWI, takriban vifo 200 kwa siku.
- Kati ya vijana wa miaka 15–19, 150,000 waliambukizwa VVU, ambapo asilimia 66 walikuwa wasichana. Katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, asilimia 85 ya maambukizi mapya katika kundi hili ni miongoni mwa wasichana.
- Ni asilimia 55 tu ya watoto wanaoishi na VVU waliopata tiba ya kupunguza makali ya virusi (ART), ikilinganishwa na asilimia 78 ya watu wazima, na kuwaacha takriban watoto 620,000 bila matibabu.
- Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inabeba mzigo mkubwa zaidi, ikichangia asilimia 88 ya watoto wanaoishi na VVU, asilimia 83 ya maambukizi mapya ya VVU kwa watoto, na asilimia 84 ya vifo vinavyohusiana na UKIMWI kwa watoto.
- Katika Afrika Mashariki na Kusini, uchunguzi wa mapema wa watoto wachanga walio katika hatari ulifika asilimia 74 na matibabu yalifikia asilimia 93 ya wanawake wajawazito wanaoishi na VVU, ikilinganishwa na asilimia 31 na asilimia 56, mtawalia, katika Afrika Magharibi na Kati.
- Hata hivyo, maendeleo yanawezekana iwapo kutakuwa na dhamira ya kudumu. Kati ya mwaka 2000 na 2024, huduma za VVU zilizuia takriban maambukizi milioni 4.4 na vifo milioni 2.1 vinavyohusiana na UKIMWI kwa watoto.
- Kufikia mwisho wa 2024, nchi na maeneo 21 yalikuwa yamethibitishwa kuwa yametokomeza maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto ya VVU na/au kaswende, huku Maldives ikiwa ya kwanza kutokomeza maambukizi ya wima ya VVU, kaswende na homa ya ini B. Botswana na Namibia zilitambuliwa kuwa ziko kwenye njia ya kutokomeza maambukizi licha ya kiwango kikubwa cha VVU.
UNICEF inahimiza serikali na wadau kulinda na kuipa kipaumbele huduma za VVU kwa mama, watoto na vijana, kuongeza juhudi za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto na matibabu ya watoto, na kuunganisha huduma za VVU katika mifumo mipana ya afya pamoja na kuhakikisha ufadhili wa wafadhili unaoongezeka na unaotabirika kupitia mbinu endelevu na bunifu za kifedha.