Mil 200/- kutoa elimu utunzaji mazingiraMil 200/- kutoa elimu utunzaji mazingira

DAR ES SALAAM: ZAIDI ya Sh milioni 200 zinatarajiwa kutumika kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira na kuendeleza misitu katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa MJUMITA, Rahima Njair jana alipowasili nchini akitokea London Uingereza, alipokwenda kupokea tuzo ya kimataifa ya uhifadhi ya TUSK – Tusk Award for Conservation Excellence, inayojulikana pia kama TUSK Conservation Award.

Tuzo hiyo ilitolewa na Prince William, Mkuu wa TUSK Trust, siku ya Jumatano jijini London, ikiwa na lengo la kutambua wahifadhi walioleta matokeo makubwa barani Afrika.

Kwa ushindi huo, Njaidi ameweka historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda tuzo hiyo barani Afrika, akichaguliwa kati ya washindani 13 waliokuwa wamefikia hatua za mwisho kutoka nchi mbalimbali Afrika.

Njaidi alisema kuwa kilichomtofautisha na wahifadhi wengine ni mkakati wa MJUMITA wa kuunganisha uhifadhi wa misitu na maslahi ya jamii, badala ya uhifadhi unaosimamia miti na misitu pekee bila kuzingatia maisha ya wananchi wanaoizunguka.

“Sisi hatuishii kusema uifadhi, uifadhi tu, sisi tunaangalia pia namna wananchi wanaoishi pembezoni mwa misitu wanavyonufaika na misitu yao. Tunahakikisha misitu inalindwa, lakini pia inaleta manufaa kwa wenye misitu hiyo jamii,” alisema Njaidi.

Alisema kuwa ustawi wa uhifadhi wa MJUMITA umejikita katika uwajibikaji wa jamii, ikiwapa nafasi wananchi, wanawake na vijana kushiriki moja kwa moja katika kulinda misitu yao pamoja na kuwekeza katika matumizi mbadala ya nishati.

Alisisitiza kuwa mojawapo ya changamoto kubwa inayoendelea kuathiri misitu nchini ni matumizi ya mkaa na kuni, hasa kwenye maeneo ya mijini na vijijini, ambapo watu wengi bado wanategemea misitu kupata nishati na kipato.

Alisema kuwa wananchi wengi hukata miti kwa ajili ya kuni, wengine huzalisha mkaa kama biashara, na wengine huingilia misitu kupanua mashamba baada ya ardhi yao kuchoka, hali inayosababisha kuongezeka kwa uharibifu wa misitu.

Hata hivyo, aliueleza umma kuwa MJUMITA haipuuzi changamoto hizo kwa kuwa inatambua kuwa mwananchi anahitaji kula, kupata kipato na kuishi maisha ya kawaida.

“Tunafahamu wananchi wanahitaji kuishi, wanahitaji kula na kupata kipato. Ndiyo maana tunawasaidia kufanya shughuli zao kwa njia endelevu bila kuharibu misitu,” alisema.

Njaidi amesema kuwa ili kupunguza misukumo hiyo, MJUMITA inatekeleza mikakati mbalimbali ikiwamo kutoa elimu ya kilimo endelevu, kusambaza majiko banifu ya kuni, na kusaidia kudhibiti uzalishaji wa mkaa kwa sheria na miongozo maalum ya matumizi ya ardhi na uvunaji wa misitu ya jamii

Alisema kwamba kupitia majiko banifu, mama wa kaya anaweza kubeba mzigo mmoja wa kuni na ukatumika hadi wiki nzima tofauti na zamani ambapo alilazimika kwenda msituni kila siku kuokota kuni.

“Sasa mama habebi tena mzigo wa kuni kila siku. Anabeba mzigo mmoja leo na inamwezesha kuitumia kwa muda mrefu bila kukata miti kila mara,” alisema.

Njaidi alisema pia kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi za serikali zimekuwa bega kwa bega na MJUMITA katika kusukuma ajenda ya uhifadhi misitu ya jamii nchini.

Alitoa shukrani kwa serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya kisera na kisheria, yanayoruhusu mashirika ya kiraia, vijana, na wadau wa uhifadhi kushiriki kikamilifu katika kulinda maliasili za nchi.
Bi Njaidi amesema, “tunashukuru kwa mwongozo wa serikali, sheria na sera zilizowekwa zinatusaidia sisi kama mashirika ya jamii kutekeleza uhifadhi kwa ufanisi.”

Alisema kuwa ushindi wa tuzo hiyo sasa unafungua ukurasa mpya kwa MJUMITA kimataifa, baada ya wadau na wafadhili jijini London kuonesha nia ya kusaidia, kushirikiana na kuunga mkono miradi ya uhifadhi wa misitu ya jamii Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *