Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake Stéphane Dujarric, Alhamisi jioni Jijini New York Marekani, Katibu Mkuu amesema ana “wasiwasi mkubwa na matukio yanayoendelea” na akaonya kuwa jaribio lolote la kupuuzia matokeo ya kura ya wananchi ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya misingi ya demokrasia.

“Kudharau mapenzi ya watu waliopiga kura kwa amani ni ukiukaji usiokubalika wa misingi ya demokrasia,” amesema, akisisitiza kuwa hatua ya wanajeshi inadhoofisha utawala wa kikatiba na uthabiti wa nchi.

Alitaka pia kuachiliwa mara moja kwa maafisa wote waliokamatwa wakiwemo wasimamizi wa uchaguzi, viongozi wa upinzani na wanasiasa wengine akisema kukamatwa kwao hakuna msingi na kunaweka hatarini taasisi dhaifu za kidemokrasia za nchi hiyo.

Chonde chonde kuweni watulivu

Kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amewataka wadau wote kuwa watulivu na kuepuka kuchochea mzozo zaidi. “Wadau wote wanapaswa kutetea taasisi za kidemokrasia na utawala wa sheria, na kuheshimu mapenzi ya wananchi,” taarifa imesema, ikisisitiza kwamba tofauti zozote lazima zitatuliwe kupitia

mazungumzo ya amani, jumuishi na kwa njia za kisheria.”

Guterres pia amethibitisha msaada kamili wa Umoja wa Mataifa kwa taasisi za kikanda zinazojitahidi kurejesha utulivu. “Umoja wa Mataifa unaunga mkono kikamilifu juhudi za ECOWAS, Muungano wa Afrika na Jukwaa la Wazee wa Afrika Magharibi katika kulinda demokrasia, kuimarisha uthabiti na kusaidia Guinea-Bissau kukamilisha mchakato wa uchaguzi kwa amani,” amesema.

Wito wa Katibu Mkuu unakuja wakati shinikizo la kimataifa likiongezeka kwa waasisi wa mapinduzi, huku viongozi wa kanda wakitaka kurejeshwa haraka kwa utawala wa kikatiba katika taifa hilo la Afrika Magharibi, ambalo limekumbwa na misukosuko ya kisiasa kwa miongo kadhaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *