Mwendokasi warejea Ubungo kwenda mjiniMwendokasi warejea Ubungo kwenda mjini

DAR ES SALAAM: WAKALA wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es salaam (DART) imerejesha huduma za usafiri wa umma katika awamu ya kwanza, kuanzia Ubungo Terminal kuelekea Gerezani, Kivukoni na Muhimbili.

Huduma hiyo imerejea rasmi leo Novemba 28,2025 katika maeneo tajwa ikiwa ni hatua ya mwanzo ya kurejea kwa huduma baada ya uharibifu mkubwa wa miundombinu uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa DART, William Gatambi ameeleza hayo akitoa ufafanuzi wa kuanza kurejea kwa huduma hizo baada ya tathmini iliyofanyika ili kubaini maeneo salama kwa ajili ya kurejesha huduma.

Gatambi amesema wamefanya hivyo wakati ukarabati katika vituo vilivyoathiriwa ukiendelea kwa awamu ili kuhakikisha mfumo mzima unarejea kikamilifu, huku akikiri kuwa kusitishwa kwa huduma kuliathiri sana wananchi, huku wengi wakilazimika kuhangaika kupata usafiri wa uhakika.

“Wananchi wamepitia changamoto kubwa ya usafiri na tunatambua hilo. Kama Serikali, tumehakikisha tunafanya juhudi zote kurejesha huduma kwa haraka, hata kama ukarabati kwenye vituo vingine bado unaendelea,” amesema Gatambi.

Katika hatua nyingine amesema bado baadhi ya vituo havijaanza huduma kutokana na mifumo yake ya umeme kuteketezwa kwa moto, hali inayozuia uthibitisho wa kiufundi kuhusu usalama na uimara wa miundombinu.

Alivitaja baadhi ya vituo hivyo kikiwemo Kituo cha Morocco, ambako mtandao wa umeme uliharibiwa, hivyo kuwafanya wahandisi washindwe kutathmini usalama wa miundombinu iliyoharibiwa kwa wakati.

“Morocco bado haijaanza huduma, siyo kwa kupenda, bali kwa sababu mfumo wa umeme uliunguzwa moto. Bila umeme, hatuwezi kuthibitisha kama miundombinu iliyoharibika ni salama kuanza kutumika. Hata hivyo, kazi ya ukarabati inaendelea bila kusimama, na ndani ya siku kumi zijazo, njia zote zitakuwa zimerejeshwa,” amefafanua.

Ameongeza pia kuwa uharibifu haukuishia kwenye vituo tu, bali uliathiri mifumo ya uendeshaji ikiwemo ukusanyaji wa data na mtandao wa umeme, hatua iliyolazimu huduma kusitishwa kwa muda ili kufanyika kwa tathmini ya kina ya usalama na kiufundi.

“Uharibifu haukuishia kwenye vituo pekee na hii ndiyo sababu haikuwezekana kuendelea na huduma kabla ya kufanya tathmini ya usalama,” amesema Gatambi.

Pamoja na kurejea kwa huduma hizo DART ilitoa onyo kwa bodaboda, bajaji na magari binafsi kutumia barabara za mwendokasi, ikisema kuwa matumizi hayo yanakiuka sheria na kuhatarisha usalama wa wasafiri.

Akisisitiza barabara hizo zimetengwa mahususi kwa ajili ya mabasi ya DART pekee, hivyo wanatoa mwito kwa watuaji wa vyombo vingine vya usafiri kuacha mara moja tabia hiyo kwa sababu siyo halali na inahatarisha usalama wa watumiaji.

Pia amesema baadhi ya wafanyabiashara wadogo kuvamia vituo vya mwendokasi na kufanya biashara kiholela, hasa maeneo ya Kimara juu na Kimara chini, hali inayoweza kuvuruga mpangilio na usalama wa vituo hivyo. Aliwataka kuacha mara moja, kwani havikujengwa kwa ajili ya biashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *