“Ndoto ya maisha yangu, mimi na cherehani yangu. Ndoto yangu ni kuwa mbunifu maarufu nchini Tanzania ili niweze kuwasaidia vijana wengi walio kwenye hali ngumu,” Anasema Antini kutoka mkoani Kigoma. Yeye amekuwa uti wa mgongo wa familia yake. Baada ya kumpoteza baba yake akiwa mdogo, alichukua jukumu lililo mbali na umri wake, akihudumiamama yake na dada zake wawili wadogo, huku akijenga ndoto zake upya kutoka mwanzo. Anaeleza siku yake inavyokuwa
“Siku yangu ya kawaida huanza kwa kuamka mapema na kufanya kazi za nyumbani kama kufuanguo, kuchota maji, na kuwatayarisha wadogo zangu kwenda shule. Nikimaliza, naenda sokoni kufanya biashara.”
Antini kutoka mkoani Kigoma nchini Tanzania, mmoja wa wanufaika wa ufadhili wa kuwawezesha vijana kiuchumi uitwayo “Safe Youth” kutoka UNICEF.
Mama wa Antini amekuwa tegemezi kwa kuwa ni mjane anakumbuka maisha kabla na baada ya kumpoteza mume wake
“Mume wangu alikuwa mkulima. Maisha yalikuwa mazuri, tulifanya kazi pamoja shambani na tulibarikiwa kupata watoto watano. Lakini alipoaga dunia, maisha yakabadilika. Changamoto ikawa kubwa, nikawa mimi ndiye baba na mama, kuhakikisha kila kitu kinaendelea nyumbani.”
Kwa changamoto zote zilizompata, Antini hakuwahi kupoteza matumaini ya kujitengenezea fursa mpya maishani.
“Nilipoacha shule, nilihisi vibaya sana. Lakini ndani yangu kulikuwa na kitu kingine nilichotamani kukifanya ambacho ni wito wa kushona kwa kutumia cherehani. Nilipata nafasi baada ya kujiunga na Ujana Salama, na hapo nikaweza kununua cherehani yangu ya kwanza.”
Ujana Salama ni programu inayoungwa mkono na UNICEF, inayojumuisha ruzuku ya fedha, mafunzo, ushauri na elimu ya afya ili kuwawezesha vijana. Hemedi, Mratibu wa Ujana Salama anasema
“Kupitia Ujana Salama tunajifunza mambo mengi. Mbali na stadi za maisha na ujasiriamali, tunapata elimu kuhusu afya na afya ya uzazi, masuala ya ukatili na ukatili wa kijinsia, pamoja na uelewa wa VVU na UKIMWI. Kwa kweli, ni programu yenye mafunzo mengi na muhimu kwa maisha ya vijana.”
Kupitia msaada wa fedha kutoka UNICEF, Antini anasema ameweza kununua mashine yake ya kushona na, kikundi hicho kimebadilisha maisha yake na kumpa matumaini mapya ya ndoto kubwa zaidi.Akisema shilingi 200 au 300 ni sawa na dola sent 20 au 30 za Marekani
“Kwa kweli, si rahisi kusaidia familia. Lakini kwa hela ndogo ninazopata, kama shilingi mia mbili au mia tatu ni lazima nizitumie kuwasaidia wadogo zangu waende shule. Ninapokaa mbele ya mashine yangu ya kushona, ninajisikia kuhamasika sana.Ninataka kuwa fundi mkuu na kuona watu wakivaa nguo nilizoshona na kuzifurahia. Natamani siku moja kushona mavazi kwa wasanii maarufu na watu mashuhuri, na kuwavalisha wale walio na umaarufu mkubwa.”