
Ripoti hii inaonesha kuwa zaidi ya watu milioni 59 wameokolewa na chanjo ya surua tangu mwaka huo, ikieleza maendeleo makubwa katika kukabiliana na ugonjwa huu .
Hata hivyo, ripoti ya shirika hilo inakadiriwa kuwa watu 95,000 wengi wao wakiwa watoto wa chini ya umri wa miaka 5 walifariki dunia kutokana na surua mwaka wa 2024. Ingawa idadi hii ni miongoni mwa viwango vya chini zaidi vilivyowahi kurekodiwa tangu mwaka wa 2000, kila kifo kutokana na ugonjwa unaoweza kuzuiwa kwa chanjo salama, ya bei nafuu na yenye ufanisi mkubwa ni jambo lisilokubalika.
Licha ya kupungua kwa vifo, WHO inasema maambukizi ya surua yanaongezeka duniani, na inakadiriwa kuwa kulikuwa na maambukizi milioni 11 mwaka 2024, ongezeko la takribani maambukizi 800,000 zaidi kuliko viwango vya kabla ya janga la coronavirus“>COVID-19 mwaka 2019.
“Surua ni virusi vinavyoambukiza zaidi duniani, na takwimu hizi zinaonesha kwa mara nyingine jinsi inavyoweza kutumia upungufu wowote katika ulinzi wetu wa pamoja dhidi yake, Surua haiheshimu mipaka, lakini kila mtoto katika kila jamii anapopewa chanjo, milipuko yenye gharama kubwa inaweza kuepukwa, maisha yanaweza kuokolewa, na ugonjwa huu unaweza kutokomezwa kabisa katika mataifa.” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO.
Katika mwaka wa 2024, visa vya surua viliongezeka kwa asilimia 86 katika Ukanda wa Mediterranean ya Mashariki wa WHO, asilimia 47 katika Ukanda wa Ulaya, na asilimia 42 katika Ukanda wa Asia ya Kusini-Mashariki ikilinganishwa na mwaka wa 2019.
Hata hivyo, Ukanda wa Afrika ulipungua kwa asilimia 40 katika maambukizi na kupungua kwa asilimia 50 katika vifo katika kipindi hiki, kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha chanjo.
Licha ya milipuko kutokea maeneo yenye lishe bora na huduma za afya, walioambukizwa bado wako katika hatari ya madhara makubwa ya kudumu kama upofu, kichomi au nimonia na encephalitis.
Chanjo haitoshelezi kulinda jamii zote
Mwaka wa 2024, inakadiriwa kuwa asilimia 84 ya watoto walipata dozi yao ya kwanza ya chanjo ya surua, na asilimia 76 pekee walipata dozi ya pili, kulingana na makadirio ya WHO na Shirika la Umoja wa Mtaifa la kuhudumia Watoto UNICEF.
Hii ni ongezeko dogo kutoka mwaka uliotangulia, na watoto milioni 2 zaidi walichanjwa. Kwa mujibu wa mwongozo wa WHO, angalau asilimia 95 ya chanjo ya dozi mbili inahitajika ili kusitisha maambukizi na kulinda jamii dhidi ya milipuko.
Zaidi ya watoto milioni 30 walibaki bila kinga kamili dhidi ya surua mwaka wa 2024. Robo tatu ya watoto hawa wanaishi katika kanda za Afrika na Mediterranean Mashariki, mara nyingi katika maeneo hatarishi, yenye migogoro au mazingira dhaifu.
Mapitio ya Kati ya Ajenda ya Chanjo 2030 (IA2030), yaliyotolewa pia leo, yanasisitiza kuwa surua mara nyingi ndiyo ugonjwa wa kwanza kurudi wakati kiwango cha chanjo kinaposhuka.
WHO imesema kuongezeka kwa milipuko ya surua kunadhihirisha udhaifu katika mipango ya chanjo na mifumo ya afya duniani, na kunatishia maendeleo kuelekea malengo ya IA2030, ikiwemo kutokomeza surua.
Kuongezeka kwa milipuko
Mwaka wa 2024, Kwa mujibu wa WHO na UNICEF nchi 59 ziliripoti milipuko mikubwa ya surau karibu mara tatu ya idadi ya nchi zilizoripoti mwaka 2021 na idadi kubwa zaidi tangu kuanza kwa janga la COVID-19. Kanda zote isipokuwa Amerika zilikuwa na angalau nchi moja yenye mlipuko mkubwa mwaka 2024. Hali ilibadilika mwaka 2025, ambapo nchi nyingi katika Amerika zilikuwa zinakabiliana na milipuko.
Juhudi za kuboresha uchunguzi wa surua zimeimarisha uwezo wa WHO na nchi kutambua na kukabiliana na milipuko, na kusaidia baadhi ya nchi kufikia kutokomeza ugonjwa.
Mwaka 2024, zaidi ya maabara 760 zinazoshiriki katika Mtandao wa Kimataifa wa Maabara za Surua na Rubela (GMRLN) zilichunguza sampuli zaidi ya 500,000, ongezeko la asilimia 27 kutoka mwaka uliotangulia.
Upungufu wa ufadhili kwa GMRLN na programu za chanjo unatabiriwa kuongeza mapengo ya kinga na kusababisha milipuko zaidi. Kuhakikisha ufadhili wa kudumu na kupata washirika wapya ni muhimu kufikia dunia isiyo na surua limesisitiza shirika la WHO.
Kuendeleza dunia isiyo na surua
Lengo la dunia la kutokomeza surua, kama lilivyoainishwa katika IA2030, bado liko mbali kutimizwa limesema shirika hilo la afya duniani.
Kufikia mwisho wa mwaka 2024, nchi 81 sawa na asilimia 42 zilikuwa zimefanikiwa kutokomeza surau, ni nchi tatu tu zaidi tangu kabla ya janga la COVID-19.
Maendeleo zaidi yamepatikana mwaka 2025, ambapo visiwa vya Pasifiki vilithibitishwa Septemba 2025, na Cabo Verde, Mauritius na Seychelles kuthibitishwa mwezi huu kuwa nchi za kwanza katika Kanda ya Afrika ya WHO kufanikiwa kutokomeza surua. Hii inaleta jumla ya nchi zilizotokomeza surua kufikia 96.
Kanda ya Amerika ilirejesha hadhi ya kutokomeza surua mwaka wa 2024 kwa mara ya pili ikiwa ndiyo kanda pekee kuwahi kuthibitishwa lakini ilipoteza hadhi hiyo tena Novemba 2025 kutokana na maambukizi yanayoendelea nchini Canada.
Surua imeongezeka tena kwa sababu chanjo imeshuka chini ya asilimia 95. Hata ikiwa kiwango cha kitaifa ni cha juu, maeneo yenye chanjo duni bado yanaweza kupata milipuko na maambukizi endelevu.
WHO imesisitiza kuwa Kutokomeza surua kunahitaji dhamira ya kisiasa, uwekezaji endelevu, dozi mbili za chanjo kwa kila mtoto, na mifumo bora ya uchunguzi.
Mapitio ya kati ya IA2030 yanasisitiza kuimarisha chanjo ya kawaida, uchunguzi, ujasiri wa kukabiliana na milipuko, na kampeni zenye ubora pale ambapo kinga ya kawaida haijatosheleza.