Dar es Salaam. Novemba 24, mwaka huu lilianza agizo la kufunguliwa kanisa lake, siku sita baadaye, ikatolewa amri ya kukomesha mipango ya kutafutwa na kukamatwa kwake, ili ajitokeze kushirikiana kurudisha umoja wa kitaifa.
Huo ni mfululizo wa matukio ya siku za karibuni, yaliyofanywa na Serikali yakimlenga Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, hivyo kuibua swali kwamba, kwanini Gwajima?
Wanaohoji swali hilo wanajengea msingi kwamba, mwelekeo wa matukio ya karibuni unaonesha wazi Serikali imewekeza nguvu katika kuliponya pengo lililojitokeza kati yake na kiongozi huyo wa kiroho.
Miongoni mwa matukio ya karibuni ni lile la Novemba 24, mwaka huu Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alipoagiza kufunguliwa kwa kanisa hilo lililofutiwa usajili Juni 2, mwaka huu.
Novemba 25, mwaka huu, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando alikwenda kulikabidhi kanisa hilo mikononi mwa viongozi wake, lakini Askofu Gwajima hakuwepo.
Novemba 30, mwaka huu, Dk Mwigulu akiwa ziarani mkoani Arusha pia alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza kiongozi huyo wa kiroho asitafutwe na vyombo vya dola, aachwe ajitokeze ili ashikamane kujenga umoja wa kitaifa.
“Mwacheni ajitokekeze tujenge umoja wa kitaifa, tushikamane kurudisha umoja wa kitaifa. Tumekutana na TEC, viongozi wa dini, wa mila na viongozi mbalimbali. Twendeni sote kwenye jambo hili, tujitokeze tuhamasishe Tanzania yenye amani, huu ndio wito wa kiongozi wetu wa nchi,” alisema Dk Mwigulu.
Wakizungumza leo Jumatatu, Desemba mosi, 2025 kwa nyakati tofauti, wachambuzi wa kada mbalimbali wamesema katika maeneo ambayo Askofu Gwajima amekuwa akihubiri kwa miongo kadhaa, jina lake limejengeka kama nembo ya ushawishi.
Wamesema sio tu kwa wafuasi wa kanisa lake, bali pia kwa sehemu fulani ya jamii ambayo imekuwa ikimwona kama msemaji wa masuala ya kiroho yanayogusa maisha ya kawaida ya mwananchi.
Wachambuzi hao wamesema, ukubwa huo wa hadhira ndiyo unaoifanya Serikali kuona umuhimu wa kupunguza joto la tofauti lililotokea kati yake na askofu huyo.
Nguvu ya ushawishi
Mchambuzi wa siasa, Dk Asumpta Chigugu amesema nguvu ya ushawishi wa kiongozi yeyote wa dini huwa na uzito mkubwa katika nchi ambayo jamii inaamini masuala ya kiroho.
“Kiongozi anapokuwa na ufuasi mpana katika maeneo ya mijini na pembezoni, anageuka kuwa sehemu muhimu ya mnyororo wa utulivu wa Taifa. Serikali inapochukua hatua za kutafuta kuelewana naye, inalenga kutuliza matabaka yote yanayomsikiliza,” amesema.
Mwanazuoni huyo ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kisiasa katika moja ya taasisi za kimataifa duniani, amesema ndiyo maana mara kadhaa imeshuhudiwa kauli za viongozi wa Serikali zikionesha nia ya kumaliza tofauti hizo kwa njia za mazungumzo badala ya misimamo.
Kwa upande mwingine, Dk Asumpta amesema katika kipindi ambacho mitandao ya kijamii imekuwa chanzo kikuu cha taarifa, vurugu ndogo ya kidini inaweza kugeuka hoja ya kitaifa ndani ya saa chache.
“Ndiyo maana Serikali imeamua kumaliza tofauti mapema ili kuondoa hatari ya hoja za kidini kuchukua sura ya kisiasa na kuongeza mivutano,” amefafanua.
Mchambuzi mwingine wa siasa na utawala, Profesa Abdulrahman Mrema amesema inavyoonekana kiongozi huyo wa kiroho ana wafuasi wengi, hasa kutokana na mtandao wa makanisa yake nchi nzima.
Katika moja ya hotuba zake, Askofu Gwajima alisema kanisa lake lina mtandao wa makanisa 2,000 na jumla ya waumini milioni nne nchi nzima.
Kwa nguvu hiyo ya ushawishi, Profesa Mrema amesema chochote kinachofanywa na Serikali dhidi yake, kinaibua hasira ya wafuasi wake na akiwekwa karibu, inakuwa rahisi kuwashawishi wafuasi wake.
“Viongozi wa kiroho sio watu wa kawaida kwenye ulimwengu wa dini nchini. Wanapokuwa na tofauti na Serikali, hoja hii inaanza kugusa watu wengi kuliko ilivyotarajiwa.
“Serikali inatambua ukimya unaweza kutengeneza taswira mbaya zaidi kuliko hatua za wazi za kutafuta suluhu,” amesema Profesa Mrema.
Amemchambua Askofu Gwajima kuwa, mtu ambaye mara nyingi hutoa kauli kali zinazogusa mioyo ya wafuasi na wakosoaji kwa wakati mmoja.
Kwa miaka mingi, amesema askofu huyo amejijengea taswira ya kiongozi anayesema bila kupepesa, hali ambayo mara nyingine imepingana moja kwa moja na msimamo wa Serikali.
Ameeleza tofauti zinapozuka kati yake na mamlaka, akisema athari hupenya mbali zaidi ya uwanja wa dini, ndiyo maana suluhisho linalotafutwa, linachukuliwa kama hatua ya kimkakati ili kulinda utulivu wa kijamii unaohitajika kwa maendeleo ya Taifa.
Mkakati kuleta maridhiano
Mtaalamu wa Utawala, Dk Haruni Amao amesema hakuna nchi duniani inayopenda kuwa na mgogoro wa wazi na kiongozi wa dini mwenye ushawishi, kwa sababu athari zake huwa hazitabiriki.
Dk Amao amesema si kila hatua inayoonesha upole wa Serikali ina sababu za siasa za muda mfupi. “Wakati mwingine Serikali huangalia picha kubwa ya nchi, maadili ya Taifa, utulivu na taswira yake kimataifa.
“Kiongozi wa dini anapokuwa na sauti inayoweza kugawanya au kutuliza, busara huwa kutafuta njia ya kumaliza tofauti, sio kuziongezea uhalali,” amesema Dk Amao.
Dk Amao amesema hatua hizo hazilengwi kwa Askofu Gwajima pekee, bali ni sehemu ya mchakato wa kurejesha imani ya viongozi wa dini na waumini kwa Serikali.
“Kwa mtazamo mpana, hatua ya Serikali kuonesha utayari wa kusikiliza ni jaribio la kujenga upya misingi ya mazungumzo, kuondoa mizengwe, kutoaminiana na kuweka msingi wa utulivu katika kipindi ambacho Taifa linahitaji mshikamano kwenye masuala ya kiuchumi na kijamii,” amesema Dk Amao.
Zinaepukwa tofauti za kidini
Mtaalamu wa Sosholijia, Dk Emmanuel Kilatu amesema mara nyingi katika masuala ya dini, mgogoro mdogo unaweza kuchukua sura kubwa ikiwa utamuinua mtu mwenye ushawishi mkubwa kwenye mzozo.
“Kwa kuamua kutafuta maridhiano mapema, Serikali inahakikisha kuwa, sauti yenye wafuasi wengi haijengi mazingira ya mgawanyiko. Hii ni njia ya kuzima moto kabla haujawaka,” amesema Dk Kilatu.
Kwa mtazamo wa Dk Kilatu, hatua ya kufungua kanisa na kuweka wazi kuwa asiwe sehemu ya rada za vyombo vya dola ni njia ya kupunguza shinikizo katika jamii.
“Watu wengi kwa kawaida hujenga hisia kali wanapoona kiongozi wao wa kiroho akipitia changamoto kutoka kwa mamlaka, jambo ambalo linaweza kusababisha misimamo mikali isiyotabirika. Anaamini Serikali imeamua kutotengeneza taswira hiyo,” ameeleza Dk Kilatu.
Mwanasosholojia kutoka Taasisi ya Taaluma za Jamii, Profesa Regina Mwangalika amesema faida nyingine ni kuzuia ajenda za kidini kuchukua mkondo wa kisiasa.
Amesema pale kiongozi wa dini anapokuwa na wafuasi wanaogusa watu wa kada mbalimbali, mgogoro wake na Serikali unaweza kuzaa tafsiri potofu zinazojenga misimamo mikali.
“Kwa kumlenga yeye (Askofu Gwajima), Serikali inalinda mazingira ya kisiasa yasipoteze utulivu wake. Tanzania imekuwa nchi ya umoja wa kimtazamo, lakini tofauti ndogo katika eneo la dini inaweza kubadili hali hiyo kwa haraka,” amesema Mwangalika.
Aidha, amesema anaamini hatua za Serikali zimelenga kuzuia vikundi vinavyoweza kutumia mgogoro kama huo kujijenga kisiasa, kuleta taharuki au kufanya kampeni za kimtandao kwa kutumia jina la kiongozi huyo.
Amesema kuondoa kizingiti mapema kunamaliza hoja ambazo zingetumika vibaya na watu wenye malengo binafsi.
Mtaalamu wa mikakati ya mawasiliano, Dk Hilda Mvungi amesema viongozi wa dini wanapokubaliana na Serikali, hutengeneza mazingira mazuri ya maadili, mshikamano na ustaarabu katika jamii.
Dk Mvungi amesema, “kwa kumsikiliza Askofu Gwajima na kumuwekea nafasi ya kutekeleza shughuli zake, Serikali inatuma ujumbe kwa viongozi wote wa dini kwamba mazungumzo ndiyo njia bora kuliko malumbano.”
Amesema maridhiano ya aina hiyo hujenga daraja kati ya Serikali na taasisi za dini ambazo mara nyingi zimekuwa nguzo ya utulivu katika nchi.
“Kwa hiyo, kuimarisha uhusiano kupitia suluhisho na Askofu Gwajima kunamaanisha pia kuimarisha uhusiano na makundi ikiwamo makanisa mengine na uislamu,” amesema.