
Machar, ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa rais chini ya mkataba wa kugawana madaraka wa mwaka 2018, aliondolewa madarakani wiki iliyopita baada ya hapo awali kuwekwa chini ya kifungo cha nyumbani, akituhumiwa kuamuru shambulio la Machi lililoua zaidi ya wanajeshi 250.
Chama chake kimekanusha kuhusika, kikisema Rais Salva Kiir anatumia kesi hii kumdhoofisha kisiasa.
Katika tamko lililosainiwa na kaimu mwenyekiti Oyet Nathaniel Pierino, chama hicho kimesema kitaongoza mabadiliko ya utawala na kimewataka wafuasi wake kujiunga na jeshi kwa ajili ya “kulinda raia na taifa.”
Sudan Kusini, ambayo ilipata uhuru mwaka 2011, ilitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Kiir na Machar vilivyoua takriban watu 400,000 kabla ya kusainiwa kwa makubaliano ya 2018.
Uchaguzi uliowahi kupangwa kufanyika Desemba 2024, umeahirishwa hadi 2026, huku Umoja wa Mataifa ukionya mapema mwaka huu kwamba taifa hilo liko katika hali ya hatari ya kurudi nyuma kisiasa na kiusalama.