
-
- Author, Oana Marocico, Seamus Mirodan & Rowan Ings
- Nafasi, BBC
Mtandao wa siri unaofadhiliwa na Urusi unajaribu kuvuruga uchaguzi ujao wa kidemokrasia katika eneo la Ulaya mashariki, BBC imegundua.
Kwa kutumia ripota wa siri, tuligundua mtandao huo uliahidi kuwalipa washiriki iwapo watachapisha propaganda zinazoiunga mkono Urusi na habari za uongo za kuhujumu chama tawala cha Moldova kinachounga mkono Umoja wa Ulaya kabla ya kura ya bunge ya Septemba 28 nchini humo.
Washiriki walilipwa ili kutafuta wafuasi kwa siri wa upinzani wa Moldova wanaounga mkono Urusi – na pia kufanya kile kinachojulikana kama kura ya maoni. Hili lilifanyika chini ya jina la shirika lisilokuwepo. Matokeo ya ya kura ya maoni, kwa mujibu wa mratibu yanaweza kuweka msingi wa kuhoji matokeo ya uchaguzi.
Matokeo ya kile kinachoitwa kura ya maoni, yanayopendekeza chama tawala kitashindwa, tayari yamechapishwa mtandaoni.
Lakini kura rasmi ya maoni inaonyesha Chama tawala Action and Solidarity (PAS) kilichoanzishwa na Rais Maia Sandu kwa sasa kiko mbele ya Kambi ya Vyama vinavyoiunga mkono Urusi (BEP).
Tumepata uhusiano kati ya mtandao wa siri na tajiri wa Moldova Ilan Shor – aliyewekewa vikwazo na Marekani kwa “kushirikiana na Urusi” na sasa yuko Moscow. Uingereza pia imemuwekea vikwazo kwa ufisadi.
Pia tumepata uhusiano kati ya mtandao huo na shirika lisilo la serikali (NGO) linaloitwa Evrazia.
Evrazia lina uhusiano na Bw Shor na aliwekewa vikwazo na Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya kwa madai ya kuwahonga raia wa Moldova ili wapige kura ya kupinga kujiunga na Umoja wa Ulaya mwaka jana. Kura ya maoni ya kujiunga ilipita, lakini kwa tofauti ndogo sana.
“Mwaka 2024 kampeni ya [Ilan Shor] ilitumia pesa. Mwaka huu inatumia taarifa potofu,” mkuu wa polisi wa Moldova, Viorel Cernauteanu, aliiambia BBC World Service.
Tuliwataka Ilan Shor na Evrazia kujibu matokeo ya uchunguzi wetu – lakini hawakutoa jibu.
Taarifa za uongo
Chanzo cha picha, GETTY
Moldova ni nchi ndogo, ipo kati ya Ukraine, na Romania mwanachama wa Umoja wa Ulaya, ina umuhimu wa kimkakati kwa Ulaya na Kremlin, wataalam wanasema.
Ripota wa BBC alipenya kwenye mtandao wa siri – ulioratibiwa kwenye Telegram – kupitia linki iliyotumwa kwetu na mtoa taarifa wa siri.
Hii ilitupa ufahamu muhimu kuhusu jinsi mtandao wa propaganda dhidi ya demokrasia unavyofanya kazi.
Ripota wetu wa siri Ana, na waajiri wengine 34, waliombwa kuhudhuria semina za siri za mtandaoni ili kwaandaa.
Semina hizo zilikuwa na maudhuti kama “Jinsi ya kutoka jikoni kwako hadi kwa kiongozi wa Kitaifa.” Ana na wengine walipaswa kufaulu mitihani ya kawaida juu ya yale waliyokuwa wamejifunza.
Kisha mwanahabari wetu alitafutwa na mratibu wa mtandao huo aitwaye Alina Juc. Wasifu wa Bi Juc kwenye mtandao wa kijamii unasema anatoka Transnistria, eneo linalotaka kujitenga la mashariki mwa Moldova ambalo lina ukaribu na Moscow, na Instagram yake inaonyesha kuwa amefanya safari nyingi nchini Urusi katika miaka michache iliyopita.
Bi Juc alimwambia Ana atalipwa lei 3,000 za Moldovan ($170, £125) kwa mwezi ili kutoa taarifa TikTok na Facebook kabla ya uchaguzi, na atatumiwa pesa hizo kutoka Promsvyazbank (PSB) – benki iliyowekewa vikwazo ya serikali ya Urusi ambayo inafanya kazi kama benki rasmi ya wizara ya ulinzi ya Urusi na ina hisa katika moja ya katika kampuni za Ilan.
Ana na waajiri wengine huchapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia ChatGPT. Lakini waliambiwa, wasitumie AI kupita kiasi ili kuhakikisha kuwa machapisho yanaonekana “ya kweli.”
Ndani ya kundi la Telegram, Ana na BBC walipata maelekezo ya awali yaliyotolewa kwa washiriki. Hapo awali, walitakiwa kuchapisha machapisho ya kizalendo kuhusu watu wa kihistoria katika historia ya Moldova – lakini polepole machapisho yakaanza kuwa ya kisiasa sana.
Ana aliombwa kuchapisha madai yasiyo na msingi – ikiwa ni pamoja na serikali ya sasa ya Moldova inapanga kughushi matokeo ya uchaguzi, uwezekano wa Moldova kupata uanachama wa EU utategemea nchi hiyo kubadilisha mwelekeo wake na kukubali LGBT, na Rais Sandu anashiriki katika biashara ya kusafirisha watoto.
Katika uchunguzi wetu wa siri na mtandao huo tulichapisha tu machapisho ambayo yalikuwa sahihi, na tulipunguza idadi yao.
Tulitaka kujua ni nani mwingine alikuwa kwenye mtandao huo, kwani tulikuwa na ushahidi kwamba uliundwa na watu wengi. Tulitafuta watu wanaochapisha taarifa zinazofanana na zetu kwenye akaunti zingine.
Mtandao huu, tulihitimisha, unajumuisha angalau akaunti 90 za TikTok – zingine zikijifanya kama vyombo vya habari – ambazo zimechapisha maelfu ya video zenye jumla ya maoni zaidi ya milioni 23 na kupendwa mara 860,000 tangu Januari. Idadi ya watu wa Moldova ni milioni 2.4 tu.
Tulipeleka matokeo yetu katika Maabara ya Uchunguzi wa masuala ya Kidijitali (DFRLab) yenye makao yake Marekani, na ilituambia uchanganuzi wake unaonyesha mtandao huo unaweza kuwa mkubwa zaidi. Kwani umekusanya maoni zaidi ya milioni 55 na zaidi ya watu milioni 2.2 wamelaiki kwenye TikTok tangu Januari, inasema DFRLab.
Maoni ya kughushi
Chanzo cha picha, GETTY
Mtandao haukuchapisha habari za uongo tu. Bi Juc pia alimpa Ana 200 lei za Moldova ($12, £9) ili kuendesha kura za maoni, kwa kuwahoji watu katika mji mkuu wa Moldova kuhusu wagombea wanaopendelea katika uchaguzi huo.
Kabla ya kufanya kazi hilo, washiriki walipewa mafunzo ya jinsi ya kuwashawishi wale wanaohojiwa.
Pia waliombwa kuwarekodi kwa siri waliohojiwa ambao walisema wanaunga mkono upinzani unaounga mkono Urusi.
Bi Juc alifichua kuwa hii ilikuwa “kuzuia kura isiibiwe” akipendekeza matokeo ya maoni na video za siri zitumike, iwapo PAS itashinda, ziwe ni kama ushahidi kwamba ilishinda isivyo haki.
Ushahidi wetu pia unaonyesha mtandao ambao mwanahabari wetu alijiunga nao unapokea pesa kutoka benki ya Urusi. Ana alisikia – na kurekodi – Alina Juc kwenye simu akiomba pesa kutoka Moscow.
“Sikiliza, unaweza kuleta pesa kutoka Moscow … ninahitaji tu kuwapa watu wangu mishahara yao,” tulimrekodi akisema.
Haikuwa wazi ni nani anatuma pesa hizo, lakini tumepata uhusiano kati ya mtandao huo na Ilan Shor kupitia NGO ya Evrazia.
Majibu ya wanaotuhumiwa
Ilan Shor na Evrazia hawakujibu matokeo ya uchunguzi wetu.
BBC ilipata picha za Alina Juc, kwenye tovuti ya Evrazia – na katika moja ya vikundi vya Telegram ambavyo aliwekwa.
Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza inasema Evrazia inafanya kazi “huko Moldova kwa niaba ya tajiri fisadi aliyetoroka Ilan Shor … ili kuvuruga demokrasia ya Moldova.”
Tulimwomba Alina Juc kutoa maoni juu ya matokeo yetu – hakujibu.
TikTok ilisema imetekeleza hatua za ziada za usalama na kabla ya uchaguzi na kuendelea “kukabiliana na tabia ya udanganyifu.”
Meta ya Facebook haikujibu maswali yetu.
Ubalozi wa Urusi nchini Uingereza ulikanusha kuhusika na habari za uongo na kuingiliwa uchaguzi na kudai ni EU ndio imekuwa ikiingilia uchaguzi wa Moldova.