v

Chanzo cha picha, Getty Images

Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania hufanyika kila baada ya miaka mitano kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge na Madiwani kwa upande wa Tanzania Bara. Zanzibar watakuwa na nyongeza ya kuchagua Rais wa visiwa hivyo na Wawakilishi.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania (INEC), katika uchaguzi huu kuna majimbo mapya nane. Kutakuwa na majimbo ya uchaguzi 272 jumla. Kati ya majimbo hayo 222 yapo Tanzania Bara na majimbo 50 yapo Tanzania Zanzibar.

Kwa mujibu wa tume hiyo, pia kutakuwa na kata 3,960 zitakazofanya uchaguzi wa madiwani. Vituo vya kupigia kura vitakuwa 99,911 na waliojiandikisha kupiga kura ni watu 37,655,559.

Pia unaweza kusoma

Majimbo Mapya

F

Chanzo cha picha, Reuters

Mwezi Mei mwaka huu, INEC ilitangaza majimbo mapya nane na kubadilisha majina ya majimbo 12.

Tume ilieleza ilibadilisha majina ya majimbo na kuongeza baada ya kupokea maombi, sambamba na hilo walitumia vigezo vingine ikiwemo idadi ya watu, ambapo kwa majimbo ya mjini kigezo ni kuanzia watu 600,000 na majimbo ya vijijini ni kuanzia watu 400,000, uwezo wa ukumbi wa Bunge kwani kwa sasa una uwezo wa kuchukua wabunge wapya.

Tume hiyo ilitaja majimbo hayo kuwa ni Jimbo la Kivule amabalo limegawanywa kutoka Jimbo la Ukonga na Jimbo la Uchaguzi la Chamanzi ambalo limegawanywa kutoka Jimbo la Mbagala yote ya mkoani Dar es Salaam.

Mkoani Dodoma limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Dodoma Mjini limegawanywa na kuanzishwa jimbo jipya la Uchaguzi la Mtumba na Mkoani Mbeya limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Mbeya Mjini limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Uyole.

Mkoani Simiyu limeanzishwa jimbo jipya moja ambapo Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la uchaguzi la Bariadi Mjini. Mkoani Geita yameanzishwa majimbo mawili ambapo Jimbo la Uchaguzi la Busanda limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Katoro na Jimbo la Uchaguzi la Chato limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Chato Kusini.

Mkoani Shinyanga limeanzishwa jimbo jipya moja, ambapo Jimbo la Uchaguzi la Solwa limegawanywa na kuanzishwa Jimbo jipya la Uchaguzi la Itwangi.

Na kuhusu majimbo kumi na mbili (12) ya uchaguzi yaliyobadilishwa majina; majimbo hayo ni pamoja na Jimbo la Uchaguzi la Chato ambalo limebadilishwa jina kuwa Jimbo la Uchaguzi la Chato Kaskazini.

Jimbo la Uchaguzi la Nkenge limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Missenyi, Jimbo la Uchaguzi la Mpanda Vijijini limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Tanganyika na Jimbo la Uchaguzi la Buyungu limebadilishwa jina sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Kakonko.

Jimbo la Uchaguzi la Bariadi limebadilishwa jina, sasa litaitwa Jimbo la Uchaguzi la Bariadi Vijijini, Jimbo la Uchaguzi la Manyoni Mashariki limebadilishwa jina na kuwa Jimbo la Uchaguzi la Manyoni na Jimbo la Uchaguzi la Singida Kaskazini limebadilishwa jina na kuwa Jimbo la Uchaguzi la Ilongero.

Majimbo mengine ni Jimbo la Manyoni Magharibi kuwa Jimbo la Itigi, Jimbo la Singida Mashariki kuwa Jimbo la Ikungi Mashariki, Jimbo la Singida Magharibi kuwa Jimbo la Ikungi Magharibi, Jimbo la Tabora Kaskazini kuwa Jimbo la Uyui na Jimbo la Handeni Vijijini kuwa Jimbo la Handeni.

Upande wa Zanzibar

L

Tanzania ni nchi moja iliyozaliwa kutokana na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wakati Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ikisimamia chaguzi zote kwa upande wa Tanzania bara na visiwani. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), inasimamia uchaguzi wa uwakilishi na urais kwa upande wa Zanzibar pekee.

Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi, alitangaza kuwa Wazanzibari watapiga kura ya kumchagua Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani Oktoba 29 mwaka huu, huku pia tume hiyo ikitaganza Oktoba 28 ni siku ya kura ya mapema.

Wale ambao watapiga kura ya mapema ni watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi mkuu, wakiwemo; wasimamizi wa uchaguzi, wasaidizi wa wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wa vituo, Askari Polisi watakao kuwa kazini siku ya uchaguzi, wajumbe wa tume ya uchaguzi, watendaji wa tume na wapiga kura ambao watahusika na kazi ya ulinzi na usalama siku ya uchaguzi.

Baraza la Wawakilishi lililomaliza muda wake lilikuwa na jumla ya wajumbe 77, wakiwemo wajumbe 50 waliopatikana kwa kuchaguliwa majimboni, saba walioteuliwa na Rais, 18 wa viti maalum, mmoja akiwa Spika wa Baraza na mmoja Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Idadi hiyo inatarajiwa kubaki kama ilivyo katika uchaguzi wa 2025.

Kwa mujibu wa mtandao wa Nukta, ukinukuu INEC na ZEC, katika idadi jumla ya wapiga kura 37,655,559 – kati yao wanaume ni milioni 18,712,104 na wanawake ni milioni 18,943,455.

Tanzania Bara ina jumla ya wapiga kura milioni 36,929,683. Hii ni ongezeko la wapiga kura milioni 7.9 sawa na asilimia 26.6 kutokea wapiga kura milioni 29,754,696 waliosajiliwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Huku Zanzibar ikiwa na jumla ya wapiga kura 725,876 waliosajiliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *