Ousmane akibusu tuzo za Ballon d'Or baada ya kutangazwa mchezaji bora duniani mwaka 2025

Chanzo cha picha, Getty Images

“Akijitahidi ipasavyo, anaweza kuwa mchezaji bora duniani.”

Hii ilikuwa kauli ya ujasiri iliyotolewa na kocha wa zamani wa Barcelona, Xavi, mwaka 2021, kauli ambayo Ousmane Dembélé alikuwa akiisikia mara kwa mara katika maisha yake ya soka.

Lakini kwa wengi, ilikuwa vigumu kuamini.

Dembélé, ambaye mwaka 2017 alisajiliwa na na klabu ya Barcelona kutoka Borussia Dortmund Ujerumani kwa ada ya pauni milioni 135.5 na kuwa mchezaji wa pili ghali zaidi duniani, hakuweza kufikia matarajio hayo kwa muda mrefu.

Maisha yake Camp Nou yaligubikwa na majeraha ya mara kwa mara, kukosa utulivu wa kiwango, na maswali kuhusu nidhamu na mtazamo wake.

Lakini sasa, akiwa na umri wa miaka 28, hatimaye ametimiza unabii huo kwa kutwaa Ballon d’Or, tuzo ya mchezaji bora wa mwaka duniani, ndoto aliyoiota kwa miaka mingi.

Wakati wa kupokea tuzo hiyo jijini Paris, Dembélé alishindwa kuzuia machozi alipowashukuru familia yake kwa kujitolea kwao.

Ilikuwa ni taswira halisi ya safari ya mchezaji aliyeanzia chini, akapitia changamoto lukuki, na hatimaye kufika kileleni.

Katika msimu wa 2024-25, Dembélé aling’ara vilivyo akiwa na Paris Saint-Germain (PSG).

Aliongoza timu kutwaa mataji matatu makubwa: Ligue 1, Coupe de France, na UEFA Champions League, na pia kufika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu.

Kwa ujumla, alifunga mabao 35 na kutoa pasi za mabao 14, huku akitajwa kuwa mshambuliaji bora zaidi barani Ulaya kuanzia mwanzo wa mwaka.

Kwa mara ya kwanza katika taaluma yake, alizidi kiwango cha wachezaji wakubwa kama Mohamed Salah (aliyehusika kwenye mabao mengi zaidi Ulaya), Kylian Mbappé (aliyeongoza kwa mabao), na vipaji wa Barcelona kama Lamine Yamal na Raphinha.

Mabadiliko ya Dembélé yalianza polepole akiwa Barcelona, lakini yalikamilika alipohamia PSG mwaka 2023 kwa ada ya pauni milioni 43.5.

Akiwa chini ya kocha Luis Enrique, alipewa nafasi na majukumu mapya. Kocha alimwambia wazi, “Sasa bila Mbappé, tunahitaji mabao kutoka kwako. Kuwa mbinafsi. Uwe mchezaji mwenye njaa.”

Wakufunzi waliendelea kumwambia ‘Ballon d’Or, Ballon d’Or, Ballon d’Or’.

Jinsi Dembele alivofaidika baada ya kuondoka kwa Mbappe

Ousmane Dembele

Chanzo cha picha, Getty Images

Mnamo Agosti 2023, PSG ilimnunua mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa pauni milioni 43.5 tu, na alifunga mabao sita na kutengeneza mengine 14 huku PSG ikishinda ligi na kikombe mara mbili.

Hakuwa mchezaji wa kutegemewa hata hivyo huku mfungaji bora katika historia ya klabu hiyo Mbappe akifunga mabao 44 kwenye mashindano yote katika msimu uliokuwa bora kwake kati ya misimu saba aliyoichezea PSG. ulikuwa msimu wake wa mwisho, baada ya hapo Real Madrid ikamsajili

PSG iliyo na mwonekano mpya ilihitaji kiongozi mpya na mshambuliaji. Dembele akajitokeza.

Na kweli alipiga hatua kubwa. alihusika katika mabao 51, idadi ambayo ni mara mbili zaidi ya aliyowahi kufikisha katika uchezaji wake wote, huku akifunga mabao 35, ambayo ni 21 zaidi ya aliyofunga hapo awali

Msimu uliopita, kocha Luis Enrique alimwambia Dembele kwamba anahitaji mabao mengi na mchango mkubwa kutoka kwake kufuatia kuondoka kwa Mbappe – akipewa uhuru wa kuwa mchoyo kwa kutoa pasi chache na kuwa na ari ya kufunga.

Kwa siri, Wasaidizi wa Kocha wamekuwa wakimwambia ikiwa atafanikiwa kufunga asilimia kubwa ya nafasi anazopata basi ataleta ufanisi kwa timu na pia kwake yeye binafsi

Dembele alijitwika jukumu hilo na kufurahia nafasi yake mapya kiufundi

Katika msimu wa 2023-24, alikuwa akichezeshwa sana upande wa kulia. hakukuwa na nafasi ya kumuondoa Mbappe katika nafasi yake ya kati

Hivi sasa yeye hucheza kama mchezaji nambari tisa asiye asili, ndani, ambapo hupata mpira mara nyingi, anafurahia uhuru wa kupokea pasi na kuhusika katika mchezo akipata nafasi nyingi za kufunga mabao

majukumu mapya na mchezaji mpya

Soma pia:

Je, nini kilimbadilisha Dembélé?

Mabadiliko ya Dembélé hayawezi kuhusishwa na kuondoka kwa Mbappé pekee.

Kwa kweli, hatua hiyo ilikuwa ya mwisho katika mchakato wa mabadiliko ya maisha yake ndani na nje ya uwanja.

Wakati akiwa Barcelona, alikumbwa na majeraha ya misuli mara 14 na alikosa takribani siku 784 kwa sababu ya kuwa majeruhi.

Masuala ya nidhamu pia yalimkosesha nafasi.

Alijulikana kwa kuchelewa mazoezini, mara nyingi kwa sababu ya kukesha akicheza michezo ya video, na kuwa mchezaji aliyepigwa faini nyingi zaidi klabuni.

Lakini mwaka 2021, maisha yake yakachukua mwelekeo mpya.

Alifunga ndoa kwa siri na mpenzi wake Rima nchini Morocco, kisha wakapata mtoto.

Hatua hiyo ya kuwa baba ilimfanya aanze kuona maisha kwa jicho la tofauti.

Akaanza kujitunza, kuajiri mtaalamu wa viungo na mtaalamu wa lishe kutoka Ufaransa, na kuacha maisha yasiyo na utaratibu.

Alifanya mazoezi ya kinga dhidi ya majeraha, na akaweka kipaumbele kwenye lishe bora na usingizi wa kutosha.

Alipunguza usiku wa kuchelewa, akajenga tabia ya nidhamu, na hatimaye, mwili na akili yake vikawa tayari kwa mafanikio.

Kwa muda mrefu, dunia iliamini kuwa PSG ingewania ubingwa wa Ulaya kwa kutegemea shujaa wa Ufaransa na wengi walidhani huyo angekuwa Kylian Mbappé.

Lakini hatimaye, waliokuwa sahihi… walikuwa sahihi kwa jina tofauti.

Shujaa huyo alikuwa Ousmane Dembélé, aliyebadilika kutoka kinda asiye na mwelekeo hadi mchezaji aliyekomaa, aliyepevuka kiakili, na hatimaye mchezaji bora duniani.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *