Y

    • Author, Pual Adams
    • Nafasi,

Uingereza, Canada na Australia, ambao wote ni washirika wenye nguvu na wa muda mrefu wa Israeli, sasa wamechukua hatua ya kulitambua taifa la Palestina.

Zaidi ya nchi 150 zinalitambua taifa la Palestina lakini kuwepo kwa Uingereza na nchi nyingine katika orodha kunaonekana na wengi kama wakati muhimu.

“Palestina haijawahi kuwa na nguvu duniani kama ilivyo sasa,” anasema Xavier Abu Eid, afisa wa zamani wa Palestina.

Lakini kuna maswali magumu ya kujibu, ikiwa ni pamoja na Palestina ni nini na kuna serikali ya kuitambua?

Pia unaweza kusoma

Vigezo vya nchi

Ili nchi iwe nchi, kuna vigezo vinne vimeorodheshwa katika Mkataba wa Montevideo wa 1933. Palestina inaweza kutoa madai kuwa ina vigezo viwili: ina watu wa kudumu na uwezo wa kuingia katika uhusiano wa kimataifa.

Jambo la tatu ni mipaka. Bila makubaliano juu ya mipaka ni vigumu kujua kwa uhakika maana ya Palestina.

Kwa Wapalestina wenyewe, nchi yao ambayo wanaitamani sana, ina sehemu tatu: Jerusalem Mashariki, Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza. Maeneo haya yote yanashikiliwa na Israel tangu Vita vya Siku Sita vya 1967.

Hata mtazamo wa haraka haraka kwenye ramani unaonyesha shida zinaanzia wapi.

Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza zimetenganishwa kijiografia na Israel kwa robo tatu ya karne, tangu uhuru wa Israel 1948.

Hiyo ni miaka 77 ya mgawanyiko wa kijiografia na miaka 18 ya mgawanyiko wa kisiasa.

Ndani ya Palestina kwenyewe. Uchaguzi wa mwisho wa rais na wabunge ulikuwa mwaka 2006, ina maana hakuna Mpalestina aliye chini ya umri wa miaka 36 aliyewahi kupiga kura katika Ukingo wa Magharibi au Gaza.

Ikikabiliwa na vifo vya maelfu ya raia wake, Mamlaka ya Palestina ya Abbas, inayotazama kutoka makao makuu yake katika Ukingo wa Magharibi, haina la kufanya.

Mivutano ya ndani

F

Chanzo cha picha, Reuters

Wakati mwenyekiti wa PLO, Yasser Arafat, aliporejea kutoka uhamishoni kuongoza Mamlaka ya Palestina; uvumi wa rushwa miongoni mwa watu wake wa karibu haukusaidia sana kuongeza sifa ya PA.

Mbaya zaidi, Mamlaka mpya ya Palestina ilionekana kutokuwa na uwezo wa kusitisha ukoloni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan wala kutimiza ahadi ya uhuru iliyotolewa baada ya kupeana mkono wa kihistoria kati ya Arafat na waziri mkuu wa zamani wa Israel, Yizhak Rabin, kwenye uwanja wa White House mnamo Septemba 1993.

Miaka iliyofuata kulikuwa na mipango ya amani iliyofeli, kuendelea kupanuka kwa makazi ya Wayahudi, ghasia za watu wenye itikadi kali za pande zote mbili, Israel kukumbatia siasa za mrengo wa kulia na ule mgawanyiko mkali mwaka 2007 kati ya Hamas na Fatah.

Nani ataiongoza Palestina?

dc

Chanzo cha picha, Getty Images

Mtu mmoja ametajwa mara kadhaa: Marwan Barghouti.

Alizaliwa na kukulia katika Ukingo wa Magharibi, akiwa na umri wa miaka 15 alianza kazi katika Fatah, kikundi cha PLO kinachoongozwa na Arafat.

Barghouti aliibuka kama kiongozi maarufu wakati wa uasi wa pili wa Wapalestina, kabla ya kukamatwa na kushtakiwa kwa kupanga mashambulizi mabaya ambapo Waisraeli watano waliuawa.

Daima amekuwa akikana mashtaka lakini amekuwa katika jela ya Israel tangu 2002.

Bado Wapalestina wanapozungumza kuhusu viongozi wa siku zijazo, wanaishia kuzungumza juu ya mtu ambaye amefungwa kwa karibu robo karne.

Kura ya maoni ya hivi karibuni ya Kituo cha Utafiti wa Sera cha Palestina chenye makao yake katika Ukingo wa Magharibi, kinasema 50% ya Wapalestina wangemchagua Barghouti kama rais, mbele ya Abbas, ambaye ameshikilia wadhifa huo tangu 2005.

Licha ya kuwa mwanachama mkuu wa Fatah, ambayo kwa muda mrefu imekuwa katika mzozo na Hamas, jina lake linadhaniwa kuwekwa katika orodha ya wafungwa ambao Hamas inataka kuachiliwa huru kama malipo ya kuachiliwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza.

Lakini Israeli haijaonesha nia ya kumwachilia.

Katikati ya Agosti, video iliibuka, ikionyesha Barghouti dhaifu mwenye umri wa miaka 66 akikejeliwa na waziri wa usalama wa Israel, Itamar Ben Gvir.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Barghouti kuonekana hadharani baada ya miaka mingi.

Upinzani wa Netanyahu

EFD

Chanzo cha picha, Reuters

Hata kabla ya vita vya Gaza, upinzani wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu dhidi ya taifa la Palestina umekuwa wazi.

Februari 2024, alisema, “kila mtu anajua mimi ndiye ambaye kwa miongo kadhaa nimezuia kuanzishwa taifa la Palestina ambalo lingehatarisha uwepo wetu.”

Licha ya wito wa kimataifa kwa Mamlaka ya Palestina kuanza tena udhibiti wa Gaza, Netanyahu anasisitiza hakutakuwa na udhibiti wa PA katika ukanda wa Gaza, akisema Abbas hajalaani mashambulizi ya Hamas ya 7 Oktoba.

Mwezi Agosti, Israel ilitoa kibali cha mwisho kwa mradi wa makazi katika Ukingo wa Magharibi.

Mipango ya nyumba 3,400 uliidhinishwa, huku waziri wa fedha wa Israel Bezalel Smotrich akisema mpango huo utazika wazo la taifa la Palestina “kwa sababu hakuna kitu cha kutambua na hakuna mtu wa kumtambua.”

Hatma ya Hamas

dcx

Chanzo cha picha, Getty Images

Jambo moja ni hakika: kama taifa la Palestina litaibuka, Hamas haitakuwa inaliendesha.

Tamko lililotolewa mwezi Julai mwishoni mwa kongamano la siku tatu lililofadhiliwa na Ufaransa na Saudi Arabia lilitangaza kuwa “Hamas lazima isitishe utawala wake huko Gaza na kukabidhi silaha zake kwa mamlaka ya Palestina.”

“Tamko la New York” liliidhinishwa na mataifa yote ya Kiarabu na baadaye kupitishwa na wajumbe 142 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake, Hamas inasema iko tayari kukabidhi mamlaka huko Gaza kwa utawala huru.

Ishara ya kutambuliwa inatosha?

FDC

Chanzo cha picha, Shutterstock

Barghouti akiwa jela, Abbas akikaribia umri wa miaka 90, Hamas na Ukingo wa Magharibi wanaangamia vipande vipande, ni wazi kwamba Palestina haina uongozi na mshikamano. Lakini hiyo haimaanishi kuwa kutambuliwa kimataifa hakuna maana.

“Kwa kweli linaweza kuwa na maana sana,” anasema Diana Buttu, Wakili wa Palestina, “inategemea nini nchi hizi zinafanya hivyo na nia gani.”

Afisa wa serikali ya Uingereza, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, aliniambia ishara tu ya kulitambua haitoshi.

Azimio la New York liliahidi waliotia saini ikiwa ni pamoja na Uingereza watachukua “hatua kwa ajili ya suluhu la amani la suala la Palestina.”

Maafisa huko London wanaashiria tamko la kuunganishwa kwa Gaza na Ukingo wa Magharibi, uungaji mkono kwa PA na uchaguzi wa Palestina (pamoja na mpango wa ujenzi wa Gaza) kama hatua zinazohitaji baada ya kutambuliwa.

Israel inasalia kuwa na upinzani mkali na imetishia kulipiza kisasi kupitia unyakuzi rasmi wa sehemu au maeneo yote ya Ukingo wa Magharibi.

Wakati huo huo, rais wa Marekani Donald Trump ameweka wazi kutofurahishwa kwake na suala hilo, akisema siku ya Alhamisi: “Sikubaliani na waziri mkuu kuhusu hilo.”

Mwezi Agosti, Marekani pia ilichukua hatua isiyo ya kawaida ya kubatilisha au kuwanyima viza makumi ya maafisa wa Palestina, na huenda ni ukiukaji wa sheria za Umoja wa Mataifa.

Marekani inashikilia kura ya turufu katika Umoja wa Mataifa kuhusu kutambuliwa kwa taifa la Palestina na Trump na bado anaonekana anataka “Mpango wa Riviera” ambapo Marekani itachukua umiliki wa Gaza.

Mpango huo hausemi chochote kuhusu Mamlaka ya Palestina.

Mustakabali wa wa Gaza upo mahali fulani, kati ya Azimio la New York, mpango wa Trump na mpango wa ujenzi wa Gaza kutoka nchi za Kiarabu.

Lakini kwa Wapalestina kama Diana Buttu, jambo kubwa zaidi ni kwa nchi hizi kuzuia mauaji zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *