
Chanzo cha picha, Margaret Murphy
-
- Author, Emily Holt
- Nafasi, BBC News
Kuishi kwenye nyumba tofauti na mwenzi wako si jambo geni katika nyakati hizi.
Kuna hata jina lililofupishwa rasmi inayotumika kuelezea hali hii – LAT, yaani Living Apart Together – wenzi wanaoishi maisha yao kwa kutengana kimazingira, lakini bado wakiwa kwenye uhusiano wa ndoa au kimapenzi.
Margaret ameishi kwenye nchi tofauti na mume wake kwa miaka 15.
Yeye anaishi Uingereza, huku mume wake, Peter, akiishi Australia.
Umbali huu wa mabara unamaanisha kuwa huonana mara moja kwa mwaka au kila baada ya miezi 18.
Licha ya muda mrefu bila kuonana ana kwa ana, Margaret na Peter wanasema bado ni wenzi waaminifu na wenye furaha.
“Nimepata marafiki wengi wapya na ninaishi peke yangu katika nyumba yangu ndogo ya kustarehesha jijini London. Nimefanya haya yote bila kuacha kuwa mke wa mtu, imekuwa safari ya kipekee,” aliiambia BBC kupitia kipindi cha Woman’s Hour.
Hata hivyo, kwa mujibu wa takwimu rasmi, ni asilimia 3% tu ya watu walio katika ndoa au ushirika rasmi wanaoishi maisha haya.
Margaret anaamini kuwa ndoa inaweza kuwa yenye maana na mafanikio hata kama wenzi hawaishi pamoja.
Watu maarufu pia wamewahi kuzungumza waziwazi kuhusu maamuzi ya aina hii.

Chanzo cha picha, Getty Images
Muigizaji Gwyneth Paltrow na mume wake, mwandishi na muongozaji Brad Falchuk, waliishi kwenye nyumba tofauti kwa miaka ya mwanzo ya ndoa yao. Kwa mujibu wa Paltrow, hali hiyo ilisaidia kudumisha mapenzi yao.
Mwanamitindo Ashley Graham na mume wake Justin Ervin, walidumisha uhusiano wa mbali kwa miaka mingi.
Vivyo hivyo, muigizaji Helena Bonham Carter na muongozaji Tim Burton waliishi kwa kutengana wakati wa uhusiano wao wa miaka 13.
Hivi majuzi, mwigizaji wa Abbott Elementary Sheryl Lee Ralph alifichua kwamba yeye na mumewe wamekuwa wakiishi katika pwani tofauti za Marekani kwa karibu miaka 20, kwani kazi yake inamhitaji kuishi Hollywood na mumewe, seneta wa jimbo la Pennsylvania, anahitaji kuwa Philadelphia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Maisha kabla ya kuhamia London
Miaka 15 iliyopita, Margaret alikuwa anaishi Australia.
Hakufanya kazi ya nje, alihusika na malezi ya watoto wao wanne, wakati mume wake, Peter, alikuwa daktari wa muda wote aliyebeba jukumu la kifedha.
Alipofikisha miaka 57, aliamua kurejea chuoni na kisha kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika isimu tumizi.
Watoto walipoondoka nyumbani na masomo yakiwa yamekamilika, aliona ni wakati wa kuanza maisha mapya.
Akachukua hatua ya kuhamia London.
“Ilionekana wazi kuwa mimi na Peter tulikuwa na malengo tofauti katika hatua hii ya maisha. Yeye alitaka kubaki nyumbani na kuendelea kufanya kazi, lakini mimi niliona fursa ya kujijenga upya,” anasema Margaret.
Sasa yeye ni Afisa Elimu katika Chuo cha Royal cha Madaktari wa Upasuaji.
“Nilikuwa naendelea kitaaluma wakati wengine walikuwa wakifikiria kustaafu. Ndiyo, inawezekana kupata kazi ya muda wote ukiwa na miaka 60. Ndiyo, unaweza kuhamia nchi nyingine, hata bara jingine, na kuanza upya maisha yako kwa mafanikio.”

Chanzo cha picha, Margaret Murphy
Changamoto na namna wanavyodumisha uhusiano
Licha ya mafanikio haya, Margaret anakiri kuwa maisha haya hayajakosa changamoto.
“Kwa Peter, changamoto ni kwamba bado anaishi kwenye nyumba ya zamani ya familia huko Brisbane, hana marafiki wengi na hapendi kutoka sana anaweza kujisikia mpweke. Kwa upande wangu, changamoto ni ukosefu wa kuwa na mwenzi karibu. Simwoni kila siku.”
Hata hivyo, anasisitiza kuwa siri ya mafanikio yao ni mawasiliano ya wazi na ya mara kwa mara:
“Namwambia Peter kila kitu kuhusu maisha yangu hapa London kuanzia kazi, marafiki wapya, safari zangu. Naye anapokuja London, hupata mtazamo mpya wa maisha. Anapapenda sana.”
Mifano mingine ya maisha ya LAT
Kerry, mmoja wa wasikilizaji wa Woman’s Hour, alishiriki uzoefu wake:
Amesema amekuwa na mwenzi wake kwa miaka mitatu, na tangu mwanzo walikubaliana wasikae pamoja ili kudumisha uhuru na hali yao binafsi.
“Tulinunua nyumba karibu karibu na tunaishi na watu wengine ili kusaidia gharama za mikopo ya nyumba.”
Wana mpango wa kuoana siku za usoni, lakini hata wakioana, Kerry hatarajii kubadilisha mfumo wao wa maisha:
“Hali hii inatufaa wote wawili, na kwa kweli, huu ndio uhusiano wenye nguvu zaidi tuliowahi kuwa nao.”
Mtazamo wa wataalamu kuhusu LAT
Ammanda Major, mkurugenzi wa Ubora wa Kliniki katika shirika la ushauri wa wanandoa la Relate, anasema kwamba mfumo huu wa LAT haumaanishi ukosefu wa mapenzi:
“Unatoa nafasi binafsi – mahali pa kurejea ambapo mtu anaweza kudumisha maslahi yake, utambulisho wake binafsi.”
Anasisitiza kuwa kwa wanandoa wengine, kuishi mbali kunaweza kuwa njia ya kudumisha uhusiano imara.
“Inaweza kuwasaidia watu kujisikia kuwa, ingawa nimeoa au kuolewa, bado nina nafasi yangu, maisha yangu, na ninakutana na mwenzi wangu kwa wakati tunaokubaliana wote.”
Siri ya kukaa kwa ndoa ambayo mwenzi wako mbali na wewe
Mambo muhimu ya kuzingatia ikiwa mnataka kuishi kila mmoja kwenye nyumba yake lakini mkaendeleza uhusiano ni pamoja na,
- Hakikisha ni uamuzi wa hiari kwa pande zote mbili – hakuna anayeshurutishwa.
- Wekeni makubaliano ya wazi kuhusu maisha yenu, na yazungumzwe kwa kina kabla ya kutekelezwa.
- Kagua mara kwa mara kama mfumo huo bado unafanya kazi kwa wote wawili.
- Hii ni pamoja na kupanga muda wa kukutana, kudumisha uhusiano wa kimapenzi, au kugawana majukumu ya kulea watoto iwapo wapo.
- Dumisheni mawasiliano ya wazi, ya mara kwa mara, na yenye uaminifu.
Ushauri huu umeusiwa na Mkurugenzi wa Ubora wa Kliniki wa Relate.