
Chanzo cha picha, GETTY
Pavel Zarubin, ndiye mwandishi wa habari pekee kwa sasa anayeweza kumfikia Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa ukaribu na mara kwa mara. Warusi wengi wanajua maisha ya rais kupitia ripoti za Zarubin. Ni mtu muhimu katika propaganda za Urusi.
Kila Jumapili usiku, mamilioni ya Warusi husikiliza kipindi cha televisheni “Moscow. Kremlin. Putin.”
Kipindi hiki kinawapa watazamaji mtazamo wa karibu wa maisha ya kila siku ya Putin na ni mojawapo ya programu zinazotazamwa zaidi nchini Urusi. Mwendesha kipindi ni Pavel Zarubin, anatoa maelezo ya kina ya shughuli za rais za wiki baada ya wiki, kutoka mikutano muhimu hadi taarifa ndogo ndogo.
Kwa miaka saba iliyopita, mwanahabari huyo mwenye umri wa miaka 44 ametembea na Putin kila mahali.
Wakati wa mkutano wa kilele wa Trump-Putin huko Alaska, Zarubin alitoa maelezo kuhusu ndege ya rais wa Urusi, zulia jekundu alilopita Putin, na hata jinsi choo kilivyokuwa kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani ambako mkutano huo ulifanyika.
Tukio hilo lilikuwa “mafanikio ya kisiasa,” kulingana na Zarubin.
Katika vipindi vingine, Zarubin ameripoti kuhusu paka ambaye aliogopa kuvuka barabara mbele ya msafara wa Putin, brashi iliyotumika kusafisha ndani ya gari la Putin, na mfumo wa kuhifadhi hati za rais.
Kipindi kilichompa umaarufu

Chanzo cha picha, Instagram @zarubinreporter
“Moscow. Kremlin. Putin” kiliundwa mwaka 2018, wakati umaarufu wa kiongozi huyo wa Urusi ukishuka. Putin alikabiliwa na hasira ya umma juu ya mageuzi ya pensheni ambayo hayakupendwa sana, na wimbi la maandamano lilienea kote nchini.
Kremlin ilihitaji jambo jipya ili kurudisha ushawishi wake.
Chini ya Zarubin, shajara ya maisha ya rais ilianza. Moja ya sifa ya Zarubini, ni kuepuka dokezo lolote la masuala ya kisiasa yenye utata. Kadiri kipindi cha televisheni kilivyopata watazamaji, umaarufu wa Putin pia uliongezeka.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov aliiambia BBC “Moscow. Kremlin. Putin” lilikuwa ni wazo la shirika la utangazaji la Urusi VGTRK, na Zarubin alisaidia kuunda muundo wa kipindi hicho.
Zarubin ni “mwandishi wa habari mwenye kipawa sana” na “anashughulikia shughuli za rais kwa namna ya kuridhisha sana,” kulingana na Peskov.
Hata hivyo, vyanzo vitatu tofauti vimeiambia BBC kwamba kipindi hicho, kwa kweli, sio mpango uliobuniwa wa VGTRK, lakini ulianzishwa na maafisa wa Kremlin.
Kulingana na Dmitry Skorobutov, mfanyakazi wa zamani wa VGTRK, mijadala kuhusu kipindi hicho ilianza miaka miwili kabla ya kuzinduliwa kwake, wakati kura za maoni zikifichua kuwa ushawishi wa Putin kwa umma ulikuwa ukipungua.
“Tulihitaji kufufua ushawishi wa Putin kwa umma,” Skorobutov anasema, Zarubin ni “mtumwa anayefuata maagizo…”
“Unasema kitu na anafanya … Bila maswali, bila kutafakari. Lile litakalopendwa na ‘mtazamaji mkuu, kwani kipindi hicho ni kwa ajili yake, “Skorobutov aliongeza.
Neno “Mtazamaji Mkuu” ni jinsi wafanyakazi wa televisheni ya serikali wanavyomtaja Rais wa Urusi.
Kwa miaka mingi, hakuna ambalo katika kipindi cha televisheni cha Zarubin, limemchukiza “Mtazamaji Mkuu.”
Zarubun ni nani?

Chanzo cha picha, Instagram @zarubinreporter
Zarubin alizaliwa katika Jamhuri ya Urusi ya Bashkortostan, inayopakana na Kazakhstan, katika familia ya mafundi chuma.
Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Ural, alijiunga na Channel 4 huko Yekaterinburg, jiji la nne kwa ukubwa nchini Urusi, lenye televisheni zenye nguvu na zenye ushindani. Wakati huo, vyumba vya habari bado vilifurahia uhuru wa wastani.
Wenzake wa wakati huo wanamkumbuka kama mwandishi wa habari makini na mwenye ari. Inasemekana hata aliwakemea wanahabari wengine ikiwa aliamini wanafanya kazi zenye upendeleo.
Zarubin alifika Moscow mwaka 2003 kama mwanafunzi wa VGTRK. Wenzake wanamtaja kuwa mwenye bidii, asiye na mabishano, na mwenye heshima kwa wahariri—tabia ambazo baadaye zingempandisha cheo.
Kufikia 2005, tayari alikuwa sehemu ya kikundi cha waandishi wa habari wa rais. Mwandishi wa habari wa zamani katika kundi hilo anakumbuka Zarubin alimuuliza Putin swali “gumu.” Alipodhihakiwa kwa sababu ya swali hilo, Zarubin alijibu, “Sioni haya.”
Kufikia 2012, mambo katika televisheni ya shirikisho yalianza kubadilika.
Putin alirejea Kremlin baada ya miaka minne kama waziri mkuu, huku kukiwa na maandamano makubwa kote nchini.
Shinikizo kwenye vyombo vya habari liliongezeka katika miaka iliyofuata.
“Mimi mwenyewe nilipokea orodha ya kile ambacho kinaweza kujadiliwa hewani na kile ambacho hakiwezi kujadiliwa,” anasema Skorobutov, mfanyakazi wa zamani wa VGTRK.
BBC imeona nakala ya orodha hizo, ambayo ilipiga marufuku mijadala ya maandamano, kupanda kwa bei za bidhaa, na mwanasiasa wa upinzani marehemu Alexei Navalny, miongoni mwa mada nyingine nyingi.
Kuibuka kwake

Chanzo cha picha, Instagram @zarubinreporter
BBC ilizungumza na wanahabari kumi kutoka timu ya rais waliofanya kazi na Zarubin kwa nyakati tofauti. Takriban wote wanasema hakujitofautisha na wanahabari wengine walioripoti shughuli za Putin.
Mmoja wa waandishi wa habari alisema, katika miaka hiyo, Zarubin “hakumpenda Putin kama anavyompenda sasa,” kwa mfano, alikuwa akitania juu ya tabia ya rais wa Urusi ya kuchelewa kufika huku watu wakimsubiri kwa masaa kadhaa.
Mwaka 2015, Zarubin alizidi kupata umaarufu baada ya kufukuzwa katika mazungumzo ya amani ya Minsk, kufuatia kumzomea Rais wa Ukraine Petro Poroshenko, akiwashutumu wanajeshi wake kwa kuwashambulia raia huko Donbas, simulizi iliyokuzwa na Kremlin.
Mwaka mmoja baadaye, Lithuania iliifukuza timu ya Zarubin kwa kujaribu kuingia kwenye mkutano wa upinzani bila kibali. Tukio hilo liliongeza mgongano na bingwa wa chess na mkosoaji wa Kremlin Garry Kasparov.
Mwaka 2018, Zarubin alikua mwandishi wa habari wa VGTRK katika uchaguzi wa rais ambao ulimuweka Vladimir Putin katika muhula wa nne.
“Ni yeye pekee aliyeaminiwa kuripoti kile kilichotokea kabla ya kupiga kura, siku ya uchaguzi, na baadaye,” anasema mfanyakazi mwenza wa zamani katika VGTRK.
Wenzake walianza kuona mabadiliko ya Zarubini. Kulingana na chanzo kingine cha BBC, wakati huo Zarubin alikuwa ameacha kuamini maadili ya uandishi wa habari huru.
Ukaribu na Putin

Chanzo cha picha, GETTY
Janga la COVID-19 liliimarisha nafasi ya Zarubin kandoni mwa Putin.
Mwaka 2020, kumfikia rais kulizuiwa kwa sababu ya hofu ya kuambukizwa. Kremlin ilihitaji mwandishi ambaye angeweza kuishi ndani ya “eneo safi.” Zarubin aliwekwa karantini kwa miezi kadhaa ili kupata kumfikia rais, kulingana na waandishi wa habari wawili katika timu ya rais.
Kisha alianza kuwa mwandishi pekee aliyeweza kumfikia Putin. Tangu wakati huo, amealikwa kwenye hafla ambazo waandishi wengine wanazuiwa.
Alisimama nje ya ofisi ya Putin wakati wa mazungumzo na Donald Trump, akapanda gari la rais Aurus, na hata alipigwa picha akiwa katika ghorofa ya Kremlin, ambapo Putin alimpa vitafunwa.
Zarubin pia amealikwa kwenye safari za kimataifa. Majira ya joto yaliyopita, Zarubin alichuchumaa chini, wakati wa mkutano wa Putin na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un huko Pyongyang. Kawaida, matukio kama haya hufanyika nyuma ya milango iliyofungwa.
Nukuu za kipekee mara nyingi huonekana kwanza kwenye chaneli yake ya Telegraph, na kuwalazimisha waandishi kuzinakili habari hizo.
Kulingana na hati za kampuni ya uzalishaji zilizoonekana na BBC, mshahara wa kila mwezi wa Zarubin ni karibu rubles milioni moja, au dola za kimarekani 12,000.
Wakati wa janga la covid na baada ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi kwa Ukraine, kumfikia Putin imekuwa vigumu zaidi. Zarubin sasa ana fursa nyingi za kufanya hivyo kuliko hata maafisa wakuu.
Kuhusu uvamizi wa Ukraine, lugha ya Zarubin inafanana na ile ya Kremlin: anazungumza juu ya “uchokozi wa Ulaya” na anasema Kyiv ni “sehemu ya Ukraine ya watu wa Urusi.”
“[Zarubin] anafanya kazi yake vizuri na ana uhakika kwamba havunji kanuni zozote,” afisa mmoja wa Urusi anayemfahamu mwandishi huyo wa habari anasema.
Pavel Zarubin hakujibu maombi ya mara kwa mara ya kujibu maswali kutoka BBC.