
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa Iran inatarajia China kuchukua hatua madhubuti kutekeleza mpango ilioupendekesza kuhusu utawala wa kimataifa, ili kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi na kukabiliana na siasa za upande mmoja.
Akizungumza na Televisheni ya Kitaifa ya China (CCTV) katika mahojiano maalum alipokuwa ziarani mjini Beijing kuhudhuria Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), Rais Pezeshkian alieleza kuvutiwa kwake na maono ya Rais Xi Jinping kuhusu utawala wa dunia, akisema yanasisitiza usawa wa mahusiano baina ya mataifa bila kujali ukubwa au utajiri wao.
Pezeshkian amesema: “Iran na China zinapaswa kushikamana kuhusu utawala, au mapendekezo yaliyowahi kutolewa awali kuhusu usalama, amani, maendeleo na ustaarabu wa dunia na kuyatekeleza kwa vitendo.”
Aliongeza kuwa China, kama kinara wa sera hiyo, inapaswa kuweka mazingira ya kufanikisha malengo yake makuu. Vinginevyo, ameonya, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wataendelea na siasa zao za kichokozi, wakishambulia wapinzani na kuwaua viongozi wa kisiasa, raia wa kawaida na wanasayansi.
Rais Pezeshkian amekumbusha kuwa uhusiano wa kihistoria kati ya Iran na China unarudi nyuma maelfu ya miaka, na kwamba mataifa haya mawili yana ustaarabu wa kale na wenye mizizi imara.
Akizungumzia ubaguzi wa kimataifa, Pezeshkian amesema: “Utawala wa Kizayuni unakiuka kila sheria na kufanya lolote, lakini hakuna anayeukemea.” Amesisitiza kuwa mataifa mengine yakijaribu kuchukua hatua, mashirika ya kimataifa na nchi za Ulaya hujitokeza haraka kuyatuhumu kwa kukiuka sheria na haki za binadamu.
Amekemea vikali kitendo cha utawala wa Israel cha kuzuia watu wa ardhi fulani kupata maji, chakula na mkate mbele ya macho ya dunia, na kuwaacha wafe kwa udhaifu. Rais Pezeshkian amewalaumu wale wanaodai kuwa watetezi wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa kwa kuunga mkono utawala huo badala ya kuzuia uhalifu wake na kuongeza kuwa: “Ubaguzi huu wa wazi haukubaliki kabisa.”
Amesisitiza kuwa pendekezo la Rais wa China kuhusu utawala wa dunia ni miongoni mwa misingi ya kuheshimu sheria.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Rais Pezeshkian alibainisha kuwa Iran haina matatizo na Mkataba wa Kuzuia Ueneaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) wala ukaguzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo, alilalamikia shirika hilo kwa kutoa taarifa zisizo sahihi na ripoti za kupotosha kuhusu Iran, akidai kuwa lilifanya hivyo chini ya shinikizo kutoka kwa nchi za Ulaya na mitandao yao ya ushawishi, hali inayosababisha maazimio yasiyo halisi na kuharibu taswira ya Jamhuri ya Kiislamu.