Mamia ya Wayahudi wa madhehebu ya Othodoksi wamefanya maandamano katika jiji la New York kupinga ushiriki wa waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu katika mikutano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa itakayofanyika wiki ijayo.

Katika mkusanyiko ulioandaliwa kupitia tovuti ya “Israel dhidi ya Uyahudi,” waandamanaji walikusanyika jana Jumatano mbele ya jengo la ubalozi mdogo wa Israel ulioko mjini Manhattan.

Wayahudi hao wa madhehebu ya Othdokosi walifika mapema mbele ya jengo la ubalozi huo wakiwa kwenye mabasi ya skuli, huku wamebeba maberamu yaliyoandikwa: “Netanyahu na Ben Gvir: Adui Nambari 1 wa Wayahudi,” “Kupinga Uzayuni si Kupinga Uyahudi” na “Acheni kuwalazimisha Wayahudi Kuingia Katika jeshi la Kizayuni.”

Bango lenye maandishi makubwa lililokuwa nyuma ya jukwaa zilikotolewa hotuba kwa lugha ya Kiyidi lilitoa mguso mkubwa kutokana na maandishi yake yasemayo: “Netanyahu: huzungumzi kwa niaba yetu”.

Mmoja wa waandamanaji, Rabi David Feldman amesema, ziara ya Netanyahu ya Umoja wa Mataifa “itapotosha ulimwengu ufikiri kwamba anawakilisha Wayahudi wote na kwamba matendo ambayo amefanya yanakubaliwa kwa namna fulani na dini ya Kiyahudi.”

“Kila kitu ambacho Israel na Benjamin Netanyahu wanakisimamia kinapingana kikamilifu na Uyahudi na ni chanzo halisi cha aibu na fedheha kwa watu wetu,” ameeleza Feldman. 

Akitoa mfano wa Torati, kiongozi huyo wa Uyahudi amesema, dini halisi ya Kiyahudi inataka kuwepo na upinzani dhidi ya dola la Israel.

“Tumekatazwa kuanzisha vita au shambulio dhidi ya taifa lolote. Kurejea kwenye ardhi takatifu na kufanya uhamiaji mkubwa ni marufuku.”

Huku akiyaelezea matukio ya Ghaza kuwa ni kitu “kisichokubalika,” Feldman amesema inasikitisha sana kushuhudia mauaji, unyakuzi wa ardhi na ukandamizaji wa watu wote huko Palestina.

Amesisitiza kuwa sio huko New York pekee bali ulimwenguni kote, Wayahudi wengi wanapinga kila inachokisimamia Israel.

“Ili kuweka wazi ni kwamba, hatumpingi Netanyahu tu mwenye misimamo ya kufurutu ada, bali aina zote za Uzayuni, uwe wa misimamo ya wastani au uliochupa miaka” amesisitiza Feldman.

Ameongeza kuwa maandamano yao yataendelea wakati Netanyahu atakapowasili New York.

Waandamanaji hao baadaye waliandamana kuelekea Umoja wa Mataifa kuhitimisha maandamano yao…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *