Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
Wakenya wako katika hatari kubwa ya maambukizi ya malaria kutokana na mbu aina ya Anopheles funestus kubadilika kitabia na kijenetiki.
Utafiti mpya umeonyesha kuwa mbu hawa sasa wanakwepa vyandarua kwa kuuma mchana wakiwa nje na pia wameanza kustahimili viua-viwadudu.
Wanasayansi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu ya Kenya (KEMRI) wamegundua mabadiliko makubwa ya kijeni katika mbu wa aina ya Anopheles funestus.
Ugunduzi huo umetokana na ushirikiano wa mataifa 13 ya Afrika, yaliyoshiriki katika ukusanyaji na uchambuzi wa jeni za mbu.
Cambria, mojawapo ya taasisi zilizoshiriki imetoa mchango muhimu katika utafiti huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Cambria, Profesa Elijah Songok, amepongeza utafiti huo, akisema kuwa ni ushahidi wa wazi kwamba ushirikiano wa kisayansi unaweza kuokoa maisha.
Cambria pia ilikuwa ya kwanza kubaini uwepo wa mbu wa aina ya Anopheles stephensi nchini Kenya.
Anopheles stephensi ni mbu anayestawi katika mazingira ya vijijini na mijini, hali inayohitaji mikakati maalum ya kudhibiti malaria kwa ufanisi zaidi.
Daktari Mara Lawniczak, mwandishi mkuu wa utafiti na Kiongozi Mkuu wa Kikundi katika Taasisi ya Wellcome Sanger, alisema:
“Tumebaini kuwa baadhi ya makundi ya mbu yanabadilishana vinasaba kwa urahisi kote Afrika, huku mengine yakiwa majirani wa karibu lakini yakiwa tofauti kabisa kijeni. Hii inaleta changamoto kubwa katika juhudi za kudhibiti mbu. Hata kama kundi la Gambiae Complex lingetoweka leo, malaria ingeendelea kuenea barani Afrika hadi An. funestus atakapotambuliwa na kudhibitiwa ipasavyo. Tunatarajia kuwa ufahamu huu wa kina juu ya utofauti wa kijeni na muundo changamano wa makundi ya mbu utasaidia kuanzisha mbinu mahiri za ufuatiliaji na udhibiti wa mbu.”
Jinsi utafiti ulivyofanywa
Watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu ya Kenya (KEMRI) walichambua mamia ya sampuli za mbu zilizokusanywa kutoka nchi 16 za Afrika, zikiwemo sampuli za kihistoria zilizohifadhiwa tangu mwaka wa 1927.
“Timu yetu imepata maarifa ya kipekee kuhusu utofauti wa kijeni wa mbu hao, muundo wa idadi zao, pamoja na jinsi wanavyokabiliana na mbinu mbalimbali za udhibiti kama vile dawa za kuua mbu,” KEMRI ilieleza.
Utafiti huo ulibaini kuwa mbu wanaopatikana katika maeneo ya Ikweta barani Afrika wana uhusiano wa karibu sana wa kijeni, ilhali walioko Afrika Magharibi wana tabia za kipekee.
Tofauti hii inaeleza kwa nini mikakati ya udhibiti wa malaria hufanikiwa katika baadhi ya maeneo lakini hushindwa katika mengine, licha ya kuwa ni aina hiyo hiyo ya mbu.
Dkt. Eric Ochomo, aliyesimamia utafiti huo kwa upande wa Kenya, alisema kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari:
“Utafiti wetu umeonesha kuwa mabadiliko ya kijeni yanayohusiana na usugu wa dawa yalikuwepo tangu miaka ya 1960, na yamezidi kuimarika kwa muda. Hili linadhihirisha uwezo mkubwa wa mbu huyu kuzoea mbinu mpya za udhibiti.”
Zaidi ya hayo, watafiti waligundua lengo maalum la kijeni katika Anopheles funestus, ambalo kwa sasa linatumika katika majaribio ya teknolojia ya kisasa ya gene drive kwa mbu wa Anopheles gambiae, aina nyingine ya mbu wa malaria.
Chanzo cha picha, Getty Images
Mabadiliko ya vijidudu
Hii sio mara ya kwanza vijidudu vya Malaria kuwa sugu dhidi ya dawa za kupambana na ugonjwa wa Malaria.
Mwaka 2020 mwezi Agosti utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Nature, ulibaini kuwa vijidudu vilionesha usugu dhidi ya dawa ya artemisinin- dawa iliyo mstari wa mbele ya kupambana na ugonjwa wa Malaria nchini Rwanda.
wanasayansi wametahadharisha kuwa vijidudu vya malaria ambavyo vilikuwa sugu dhidi ya dawa za awali ” zilikisiwa kusabisha ongezeko la mamilioni ya vifo vya watoto barani Afrika katika miaka ya 1980.”
Wakati dawa ya kwanza ya malaria, chloroquine ilipotengenezwa, wanasayansi walifikiri kuwa ugonjwa huo utatokomezwa ndani ya miaka kadhaa.
Lakini tangu miaka ya 1950 vijidudu hivyo vimekuwa vikijitengenezea usugu dhidi ya dawa hizo zilizoonesha mafanikio katika kupambana na vijidudu vya malaria.
Mchambuzi na mwanahabari wa masuala ya afya James Gallagher anasema kuwa hali hii inaogopesha.
Chanzo cha picha, gettyImages
Malaria ni nini?
Chanzo cha picha, Getty Images
Malaria ni ugonjwa unaosababishwa na vijidudu kitaalamu viitwavyo Plasmodium.
Husambaa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine baada ya kuumwa na mbu jike wanaokuwa wakitafuta damu kwa ajili ya chakula.
Mtu anapoumwa huugua homa kali.
Vijidudu hivyo huathiri seli kwenye ini na chembechembe nyekundu za damu, na kusababisha dalili nyingine ikiwemo upungufu wa damu.
Hatimaye ugonjwa huathiri mwili mzima, ikiwemo ubongo na unaweza kuua.
Takriban watu 435,000- wengi wao watoto- hufa kutokana na malaria kila mwaka.
Kusambaa kwa ugonjwa unaoua
Itakuwa vigumu kupambana na vijidudu vya Malaria kwani dunia bado imeendelea kuchemka kwa kiwango cha nyuzijoto 31.8 °C kilirikodiwa katika kituo kilichopo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNIA) mnamo tarehe 2 na 3 Juni, 2025.
Lengo la dunia ni kutaka ongezeko la viwango vya joto vibakie katika nyuzijoto 1.5 au chchini yake kwa kupunguza hewa ya kaboni.
“Viwango vya juu zaidi ya joto huongeza uwezo wa mbu kubeba vimelea wa malaria ambavyo vinaweza kusababisha ugonjwa ,” anasema Dkt Isabel Fletcher, meneja wa teknolojia ya data za kisayansi katika taasisi ya Wellcome Trust charity.
“Mabadiliko ya tabia nchi yatafanya maeneo mengi zaidi ya dunia kuwa mahala panapofaa kwa ajili ya usambazaji wa mbu. Kwasababu dunia itakuwa na joto zaidi , malaria inatarajiwa kupanuka zaidi katika maeneo ya nyanda za juu, ambayo kwa sasa yanaweza kuwa baridi sana kiasi kwamba mbu hawawezi kusambaza ugonjwa ,” alitahadharisha.
Changamoto za kukabiliana na Ugonjwa wa Malaria
Chanzo cha picha, Getty Images
Hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kusaini agizo la kuiondoa nchi hiyo katika Shirika la Afya Duniani (WHO) inapangua mikakati ambayo ilikuwa imeanza kuonyesha ufanisi kupambana na ugonjwa huu hatari kwa binadamu
Athari hizo zinatokana na Marekani kuwa mchangiaji mkubwa wa kifedha wa WHO na programu mbali mbali zilizopo chini ya shirika hilo na taasisi nyingine kubwa za kiafya duniani.
Mbu wanaosababisha Malaria waliobadilisha tabia ya kuvamia binadamu na kuanza kunyonya damu mchana inahofiwa kuongeza idadi ya ugonjwa huo wakati ambapo hakuna ufadhili wa kutosha wa kununua dawa za kunyunyiziwa mchana ili kukabiliana nao.
Profesa Charles Wondji kutoka Chuo cha Tiba ya Kitropiki cha Liverpool na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza nchini Cameroon, alisema:
“Kwa muda mrefu sana An. funestus amepuuzwa licha ya umuhimu wake mkubwa katika usambazaji wa malaria barani Afrika. Nafurahi kuwa utafiti huu wa kitaifa unaochunguza vinasaba vyote vya An. funestus umechapishwa sasa. Timu yangu inajivunia kuchangia hatua hii kubwa itakayorahisisha utekelezaji wa mikakati ya baadaye ya kudhibiti mbu huyu muhimu.”
Kwa sasa, wanasayansi nchini Kenya wanaendelea kuboresha mbinu ya kuhariri vinasaba vya mbu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kimataifa za kutokomeza malaria kabisa.