Chanzo cha picha, Reuters
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alipokutana na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, mjini Riyadh, walikumbatiana kwa ishara ya mshikamano.
Mkutano huo ulifanyika mara tu baada ya mataifa hayo mawili kusaini mkataba wa kimkakati wa ulinzi wa pamoja – hatua inayozidi kuikaribisha Pakistan, nchi pekee ya Kiislamu yenye silaha za nyuklia, kwa Saudi Arabia, taifa lenye nguvu kubwa kwenye eneo la Ghuba.
Afisa mmoja mwandamizi wa Saudi Arabia aliieleza Reuters kuwa ”mkataba huu ni njia ya kurasimisha ushirikiano wa muda mrefu uliokuwepo.”
Lakini kwa upande wa India, hali ni tofauti, wengi wanauona kama tishio.
India imekuwa ikijenga uhusiano wa karibu na Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni.
Hata hivyo, mkataba huu umekuja wakati ambapo uhusiano kati ya India na Pakistan umekuwa wa mvutano mkubwa, hasa baada ya mzozo wa kijeshi wa siku nne mapema mwaka huu.
Kwa kuwa India na Pakistan ni majirani wenye silaha za nyuklia na wamewahi kupigana vita kadhaa juu ya Kashmir, hatua ya Saudi Arabia kuonesha mshikamano wa kijeshi na Pakistan inaleta wasiwasi mkubwa New Delhi.
Kilicholeta hofu zaidi kwa wachanganuzi wa India ni kipengele cha mkataba kinachosema kuwa “shambulio dhidi ya nchi moja kati ya hizi mbili litachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya zote mbili.”
Mtaalamu wa masuala ya kimkakati wa India, Brahma Chellaney, aliandika kwenye X (zamani Twitter):
“Riyadh ilijua India ingeona mkataba huu kama tishio kwa usalama wake, lakini bado ikaendelea. Hatua hii haiashirii nguvu za Pakistan, bali inaonesha ndoto za Saudi Arabia za kuwa na ushawishi mkubwa wa kijeshi.”
Anaongeza kuwa Saudi Arabia inaitumia Pakistan kama mshirika tegemezi kwa kupata wanajeshi wake na pia “bima ya nyuklia” huku ikionesha kwa India, Marekani, na mataifa mengine kuwa sasa inachukua msimamo wake wa kujitegemea katika masuala ya usalama.
Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa India, Kanwal Sibal, aliuita mkataba huu “kosa kubwa la kimkakati” kwa upande wa Saudi Arabia, na akaonya kuwa huenda ukaathiri usalama wa taifa la India.
“Pakistan ni nchi isiyo na utulivu wa kisiasa na inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Kuiona kama mshirika wa usalama ni hatari,” bwana Sibal aliandika kwenye X.
“Kwa mvutano uliopo kati ya India na Pakistan, hatua ya Saudi Arabia ni ya hatari kimkakati.”
Kwa upande wake, serikali ya India chini ya Waziri Mkuu Narendra Modi imechukua msimamo wa utulivu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisema kuwa serikali inafanya tathmini ya athari za mkataba huo kwa usalama wa kitaifa na uthabiti wa kikanda na kimataifa.
India pia ilieleza matumaini kwamba Saudi Arabia itazingatia maslahi na hisia za pande zote mbili.
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Je, mkataba huu ni tishio halisi?
Si wachambuzi wote wanaoamini kuwa huu ni mkataba wa kutia hofu.
Baadhi yao wanasema India inaweza kuwa inakisia mambo kupita kiasi, kwa sababu Saudi Arabia bado inathamini uhusiano wake mzuri na India ambayo ni mshirika wake wa pili kwa biashara na mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Saudi Arabia.
Michael Kugelman, mchambuzi wa sera za kimataifa, aliiambia BBC kuwa:
“Mkataba huu hauiathiri India moja kwa moja. Saudi Arabia haitachukua hatua za uhasama dhidi ya India, hasa ikizingatiwa uhusiano wake mpana na New Delhi.”
Hata hivyo, Kugelman anaongeza kuwa kwa kuiweka Pakistan ndani ya mfumo wa usalama wa Mashariki ya Kati, Saudi Arabia inaipa Pakistan nguvu mpya ya kisiasa.
”Sasa Pakistan inaungwa mkono na China, Uturuki ambao waliipatia silaha wakati wa mzozo na India na sasa Saudi Arabia imeingia kundini.” Kugelman aendelea kueleza.
Wachambuzi wengine wanasema kuwa mkataba huu hauonyeshi hatari ya moja kwa moja kwa India, lakini unaashiria mabadiliko ya ushawishi wa kisiasa na kijeshi katika eneo hilo.
Husain Haqqani, balozi wa zamani wa Pakistan na sasa mchambuzi wa Hudson Institute, alisema India inapaswa kuwa na wasiwasi kwa sababu mkataba huu unaweza kuifanya Saudi Arabia kuwa kama ilivyokuwa Marekani kwa Pakistan wakati wa Vita Baridi yaani taifa lenye uwezo wa kusaidia Pakistan kujijenga kijeshi dhidi ya India.
Lakini yote yanategemea namna maneno kama “ushambulizi” au “mshambuliaji” yatakavyofasiriwa na kama Riyadh na Islamabad watakuwa na mtazamo sawa juu ya hali yoyote ya hatari.
Lakini si kila mtu anauona mkataba huo kama mabadiliko makubwa.
Chanzo cha picha, Reuters
“Ni rasmi tu, lakini ni mwendelezo wa uhusiano wa muda mrefu kati ya Saudi Arabia na Pakistan tangu miaka ya 1960,” Dk. Md. Muddassir Quamar kutoka Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru anasema.
Kwa hakika, nchi hizo mbili zinashiriki uhusiano thabiti unaotokana na uhusiano wa kiulinzi.
Tangu wakati huo, Pakistan imetuma wanajeshi Saudi Arabia, na maafisa wake wamesaidia kulijenga Jeshi la Anga la Saudi.
Pakistan pia ilisaidia kukabiliana na tukio la uvamizi wa msikiti wa Mecca mwaka 1979.
Mwaka 2017, Riyadh ilimteua mkuu wa zamani wa jeshi la Pakistan kuongoza muungano wa kijeshi dhidi ya ISIS.
Bw Haqqani anabainisha kuwa uungwaji mkono wa kisiasa, kiuchumi na kijeshi wa Saudia umeimarisha utegemezi huu kwa miongo kadhaa.
“Tangu miaka ya 1970, Saudi Arabia imekuwa ikiunga mkono Islamabad mara kwa mara, ikishirikiana nayo wakati wa vita vya 1965 na 1971 na India, kupanua misaada ya kiuchumi wakati wa shida, kuruhusu malipo ya mafuta yaliyoahirishwa, na kudumisha ushirikiano wa karibu wa kijeshi,” anasema.
Kulingana na wachambuzi mkataba huu pia unaashiria kuwa Saudi Arabia inazidi kupunguza utegemezi wake kwa Marekani katika masuala ya ulinzi.
Mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel, yaliyoisumbua Qatar na mataifa mengine ya Ghuba, yamemfanya Mfalme wa Saudi kujiuliza kama Marekani bado ni mlinzi wa kweli.
Ahmed Aboudouh wa Chatham House anasema mkataba huu hauhusiani na vita moja kwa moja, bali ni ujumbe wa kisiasa:
“Saudi Arabia inaonesha kuwa inatafuta ushirikiano mpya wa usalama bila kukatisha ushirikiano wake wa kijeshi na Marekani.” bwana Aboudouh aiambia BBC.
“Ingawa kina cha utendakazi wa mpango huo hauko wazi, inaonyesha mabadiliko katika mtazamo wa vitisho vya Saudi Arabia, kuona Iran na Israeli kama tishio, na kunufaika na hadhi ya nguvu ya nyuklia ya Pakistan ili kuongeza uzuiaji.”
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kwa India, mkataba huu hauleti tishio la kijeshi kwa sasa, lakini unaweza kuathiri mikakati ya muda mrefu ya kieneo, hasa mikakati yake ya kukuza biashara, uwekezaji, na ushawishi katika mataifa ya Ghuba. Bwana Aboudouh aongezea.
Hatari ya kweli, aliiambia BBC, iko mahali pengine: muungano uliopanuliwa unaweza kuwa mgumu katika “Nato ya Kiislamu”, na kutatiza mkakati wa Delhi wa ‘kuwa na ukuruba na Magharibi’ katika biashara, uwekezaji na ukanda wa kimkakati katika Ghuba.
Kwa upande wa Pakistan, mkataba huu unaiwezesha kupata msaada wa kifedha na kisiasa kutoka Saudi Arabia jambo ambalo linaipa nguvu zaidi dhidi ya India.
Kugelman anasema, “India inaweza kutegemea uhusiano wake mzuri na nchi kama Urusi, Israel, mataifa ya Ghuba, na washirika wa Magharibi kama Ufaransa. Lakini hali hii inaonesha kuwa Pakistan inazidi kupata nguvu mpya.”
Hata kama mkataba huu hauna athari za haraka, wachambuzi wanasema si picha nzuri kwa diplomasia ya India.
Ni mapema kujua athari zake kamili, lakini bila shaka India itaendelea kufuatilia kwa karibu.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid