Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amekaribisha ‘ujumbe wa wazi’ uliotolewa na rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye juma hili alionekana kubadili msimamo kuhusu vita ya Ukraine, akidai kuwa nchi hiyo inaweza kurejesha kwenye himaya yake miji iliyochukuliwa na Urusi.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Katika mahojiano na RFI pamoja na televisheni ya France 24 jijini New York, Macron amesema tangazo la Trump ni ‘muhimu sana’ na linatoa uelekeo mpya kuhusu vita ya Ukraine, wakati huu Kiev ikihitaji kila aina ya msaada wa silaha kutoka Marekani.

Huu ni ujumbe wa wazi kutoka kwa rais wa Marekani kwamba, Urusi ni dhaifu na haina uwezo kama wengi walivyosema”, alisema rais Macron.

Tangazo hili ‘litaifanya Ukraine ijibu mashambulizi kwa nguvu na hata kuchukua miji yake”, amesema rais Macron ambaye yuko New York akihudhuria mkutano wa umoja wa Mataifa unaoendelea.

Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii baada ya kukutana kwa mazungumzo na rais Volodymry Zelensky kuwa, Ukraine kwa msaada wa umoja wa Ulaya na nchi yake, iko katika nafasi nzuri ya ‘kurejesha maeneo yake yote yaliyochukuliwa na Urusi’.

Mwaka 2014 Urusi iliuchukua mji wa Crimea na sasa inadhibiti maeneo kadhaa ya mashariki na kusini mwa Ukraine, baada ya kuanzisha vita mwezi Februari mwaka 2022.

Hivi karibuni Urusi imelaumiwa kwa matumizi mabaya ya anga la nchi za Ulaya, ambapo jumuiya ya NATO iliionya Moscow baada ya kurusha ndege zisizo na rubani kwenye anga la nchi za Poland, Estonia na Romania, rais Macron akisema jumuiya yao italazimika kujibu kwa nguvu uchokozi wowote unaoendelea kufanywa na Urusi.

Rais Macron alisema “hii ina maana kuwa ikiwa mtu atakuchokoza tena, lazima ujibu na tena ujibu kidogo kwa nguvu”, bila hata hivyo kuweka wazi namna ambavyo nchi za NATO zitajibu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *