Duru rasmi za utawala wa Kizayuni wa Israel zimemnukuu mmoja wa maafisa wake wa kijeshi walioendesha operesheni ya kigaidi ya kuishambulia Doha, mji mkuu wa Qatar akikiri kwamba, Tel Aviv ilifeli na kushindwa vibaya katika shambulio hilo. Hii ni mara ya kwanza kwa Israel kukiri hadharani kufeli vibaya operesheni hiyo.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu afisa huyo wa jeshi la Israel akisema kama zilivyoripoti duru rasmi za Israel kwamba: “Sasa naweza kusema rasmi kuwa tulishindwa katika shambulio dhidi ya Qatar.”

Inafaa kuashiria kuwa, Jumanne jioni ya Septemba 9, utawala ghasibu wa Israel ulishambulia eneo la mkutano wa timu ya mazungumzo ya Hamas mjini Doha kwa kutumia ndege 15 za kivita na makombora 12.

Ingawa hakuna kiongozi yeyote wa Hamas aliyedhurika katika shambulio hilo, lakini wanachama kadhaa wa Hamas na raia, akiwemo raia wa Qatar, waliuawa shahidi.

Baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya shambulio hilo la kigaidi huko Doha, mji mkuu wa Qatar, Waziri Mkuu wa Misri alisema kwamba nchi yake nayo inalengwa katika njama za kuchora upya ramani ya eneo la Asia Magharibi na kuna hatari ikagawika vipande vipande.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Kamal Madbouly alisema kwamba hofu hiyo iko katika ngazi ya ndani na kimataifa na ni katika changamoto za kikanda na kimataifa zinazoikabili Misri na eneo hili zima. Amesema hayo mbele ya viongozi waandamizi wa vyombo vya habari vya Misri. 

Alisema anaamini kwamba hivi sasa dunia inapitia kipindi cha “kuzaliwa ramani mpya ya kijiografia na kisiasa na kwamba eneo la “Mashariki ya Kati” liko kwenye kitovu cha mabadiliko hayo.

Waziri Mkuu wa Misri alisisitiza kuwa, nchi yake sawa na nchi nyingine, inakabiliwa na changamoto tata zinazohitaji welewa wa umma na mshikamano wa ndani ili kulinda utulivu na usalama kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *