Jeshi la Algeria limeua magaidi sita wakati wa operesheni ya kukabiliana na ugaidi wiki hii katika mkoa wa Tebessa, yapata kilomita 700 mashariki mwa mji mkuuu, Algiers.

Hayo yametangazwa na Wizara ya Ulinzi wa Taifa ya Algeria na kusisitiza kwa kusema: Operesheni hiyo iliyoendeshwa katika Mkoa wa Tano wa Kijeshi nchini humo pia ilipelekea kukamatwa bunduki sita aina ya Kalashniko.

Akiwa katika ziara mkoani humo, Mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Algeria, Said Chanegriha, aliisifu operesheni hiyo kuwa ni ya kishujaa na kuwasilisha pongezi za Rais Abdelmadjid Tebboune kwa wanajeshi.

Alitoa wito wa kuendelea jitihada za kulinda “usalama wa taifa na raia wake” na kupambana na mabaki ya magaidi “kwa mori, ushujaa na kujitolea kwenye jukumu hilo takatifu.”

Jeshi la Algeria mara kwa mara hufanya operesheni za kusafisha milima na misitu ya kaskazini mwa Algeria, ambayo ni ngome ya magenge ya kigaidi ambayo wakati fulani yalikuwa tishio kubwa la usalama katika miaka ya 1990.

Mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Wizara ya Ulinzi ya Algeria ilitangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limeangamiza magaidi wawili wenye silaha katika operesheni inayoendelea ya kukabiliana na magenge ya kigaidi katika mkoa wa mashariki wa Khenchela, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Tunisia.

Taarifa ya wizara hiyo iliongeza kuwa, operesheni hiyo ilifanyika katika eneo la Oued Boudhkane, takriban kilomita 500 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Algiers. Wanajeshi walikamata bunduki mbili aina ya Kalashnikov na risasi kwenye eneo la tukio.

Wizara hiyo imeongeza kuwa, operesheni hiyo inaonesha kwamba hatari za kuzuka upya vitendo vya kigaidi ndani ya Algeria bado ipo lakini vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo viko macho na vimeazimia kikweli kuwasaka na kuwasafisha kabisa magaidi waliosalia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *