Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina imetoa taarifa mpya na kusema kuwa, Muqawama utaendelea kuwepo madamu ardhi za Palestina zinaendelea kukaliwa kwa mabvu na Wazayuni na imelaani vikali matamshi ya Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Sehemu moja ya ya taarifa ya Hamas inasema: “Muqawama ni jukumu la kitaifa na kimaadili linalopata uhalali wake kutoka kwa watu wa Palestina.”

Imeongeza kuwa, madai ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwamba harakati ya Hamas haitakuwa na nafasi yoyote katika serikali ni shambulio la wazi dhidi ya haki isiyoweza kubatilishwa na ya kihistoria ya watu wa Palestina ya kuamua wenyewe hatima yao.

Taarifa ya Hamas pia inaeleza kwa uwazi kwamba maadamu uvamizi wa Wazayuni unaendelea kuwa janga kwa ardhi yetu, hakuna anayeweza kulizuia taifa la Palestina kubeba silaha na kuendesha mapambano ya ukombozi.

Inakumbukwa kuwa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina alitoa mwito wa kupokonywa silaha Hamas na makundi ya Muqawama wa Palestina katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Siku chache zilizopita pita, Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, ilipongeza hatua ya kutambuliwa taifa la Palestina na mataifa ya Uingereza, Australia na Kanada, ikieleza kuwa hiyo ni hatua muhimu katika kuthibitisha haki ya Wapalestina juu ya ardhi yao.

Katika taarifa hiyo HAMAS iliitaka jamii ya kimataifa pamoja na Umoja wa Mataifa kuutenga utawala wa wa Kizayuni Israel na kusitisha aina zote za ushirikiano na utawala huo wa katili na wa kibeberu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *