
Nchi kadhaa duniani zikiongozwa na Marekani zinapigana vikumbo katika kuiga na kutengeneza nakala za ndege isiyo na rubani ya Shahed ya Iran, ambayo si ghali lakini yenye ufanisi na usahihi wa hali ya juu.
Katika ripoti yake ya Jumatano, Jarida la Wall Street la Marekani limesema kwamba mashirika tofauti nchini Marekani, China, Ufaransa na Uingereza yanatengeneza nakala ya droni hiyo ya Iran iitwayo Shahed.
Taarifa ya jarida la Wall Street Journal pia imesema: “Marekani na washirika wake wanapigana vikumbo na wanashindana hivi sasa kutengeneza droni ya Shahed ya Iran ambayo ni ya gharama za chini na inakwenda masafa marefu.”
Ripoti hiyo ya jarida maarufu la Marekani pia imebainisha kuwa droni zinazofanana na droni ya Shahed ya Iran zimeanza kuonekana nchini Marekani ikiwa ni pamoja na zile zilizopachikwa majina ya LUCAS na Arrowhead zilizotengenezwa na makampuni ya SpectreWorks na Griffon Aerospace ya Marekani.
Sehemu nyingine ya ripoti ya jarida hilo la Wall Street Journal la Marekani imesema: “Droni za Shahed na aina zake mbalimbali zimeenea sana hivi sasa duniani na hasa katika nchi za Ulaya na Magharibi kiasi kwamba mashirika kama Griffon na Saab ya Uswisi yanauza hata droni za mazoezi zinazofanana na za Iran.”
Ndege isiyo na rubani ya Shahed ya Iran ni miongoni mwa droni zenye uwezo wa hali ya juu zaidi duniani. Ina uwezo wa kipekee wa kufanya upelelezi, ufuatiliaji na kuendesha operesheni zake wa ufanisi wa hali ya juu. Gharama ya utengenezaji wake ni nafuu sana. Zinaweza kuzima mifumo ya ulinzi wa anga ya adui zinapotumwa kwa idadi kubwa.