
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergey Lavrov amesema, mgogoro wa Ukraine ulipangwa na nchi za Magharibi kwa sura ya vita dhidi ya Russia vinavyopiganwa na Kiev.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Russia ameyasema hayo wakati wa mkutano wa mawaziri wa G20 uliofanyika kando ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Lavrov amesema, kukataa kufuata Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambalo ni dhihirisho la “matamanio ya ukoloni mamboleo,” huchochea vita vya kikanda na kuibua mvutano wa kimataifa na kusababisha migogoro ambayo haijatatuliwa kwa miongo mingi barani Afrika na kwingineko.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema: “mfano mwingine wa wazi mgogoro uliochochewa na nchi za Magharibi ni wa Ukraine, ambako shirika la kijeshi la NATO na Umoja wa Ulaya zinataka kutangaza – bali tayari zimeshatangaza – vita halisi dhidi ya nchi yangu na zinashiriki moja kwa moja katika hilo”.
Moscow imekuwa imekuelezea mara kwa mara mzozo wa Ukraine kuwa ni vita vya wakala au niaba vya Magharibi dhidi ya Russia, ambapo vikosi vya Kiev vinatumiwa kama “askari wa mhanga.”
Viongozi wa Russia wanasisitiza pia kuwa nchi za Magharibi zimekuwa zikizidisha mvutano katika eneo hilo kwa miaka mingi, na kupuuza wasiwasi wa muda mrefu wa Moscow juu ya upanuzi wa shirika la kijeshi la NATO kuelekea upande wa mashariki…/