Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Khatam Amer
- Nafasi, BBC News Arabic
“Siku moja, rafiki yangu alinipigia simu akihitaji msaada wa kuandaa mada ya uwasilishaji kwa somo la Kiarabu katika chuo kikuu. Nilimsaidia kuandika insha nzima.”
“Baadaye ndipo nilipogundua kuwa nilikuwa nimelala wakati wote wa mazungumzo hayo yaliyodumu kwa takriban dakika thelathini. Nilichokumbuka tu ni kwamba nilipokea simu yake.”
Salma (si jina lake halisi) alisimulia kisa hiki baada ya kugundua kuwa yeye ni miongoni mwa watu wanaozungumza usingizini.
Akizungumza na BBC, Salma alisema:
“Mara ya kwanza nilifahamu kuhusu hali hii kutoka kwa mama yangu, aliyeniambia kuwa huwa naongea usingizini. Nilimuuliza, ‘Je, yale maneno huwa yanaeleweka kwako au kwa ndugu zangu?’ Akajibu kuwa mara nyingi siyo ya kueleweka. Wakati mwingine naota ndoto na kujishtukia nikiwa nimeamka, bila kujua kama nilikuwa nikizungumza. Wakati mwingine pia huhisi kama nazungumza na mtu, lakini siwezi kutofautisha kama ni ndoto au hali halisi. Ninachokumbuka ni kwamba mara kadhaa hujibu maswali nikiwa usingizini, lakini siwezi kueleza nilichosema hasa. Wakati mwingine husahau kabisa kuwa nilizungumza na mtu.”
Salma ni mfano wa watu wengi wanaopatikana na hali hii ya kuongea usingizini. Huenda umewahi kusikia mtu akinong’ona au akitamka maneno yasiyoeleweka kwa sauti, hata akiwa katika usingizi mzito chumba jirani. Lakini anapoamka, hana kumbukumbu yoyote ya alichosema usiku kucha.
Swali ambalo wengi hujiuliza watu wanaopitia hali hii na hata wale wanaoishi nao ni,
Ni nini husababisha mtu kuzungumza akiwa amelala? Je, hali hii ni dalili ya tatizo la kiafya? Na iwapo ni hivyo, je, kuna tiba?
Chanzo cha picha, Getty Images
Kwanini watu huzungumza usingizini na je maongezi hayo hueleweka?
Dkt. Tareq Gharaibeh, mtaalamu wa magonjwa ya kifua na usingizi, alieleza katika mahojiano na BBC kuwa:
“Tabia ya kuzungumza wakati wa usingizi haina chanzo maalum kilichothibitishwa kisayansi. Hata hivyo, imebainika kuwa hali hii huongezeka miongoni mwa watu wanaokumbwa na hali ya kuchanganyikiwa, na usingizi mzito unaosababishwa na usafiri wa haraka katika maeneo ya saa kadhaa, ambayo huvuruga saa ya ndani ya mwili, au mdundo wa mzunguko (jet lag) kutokana na safari za mbali, au wale ambao hupata usingizi kwa viwango visivyo vya kawaida yaani, mtu analala kidogo sana kwa muda mrefu halafu baadaye analala kwa muda mrefu zaidi.”
Aliendelea kufafanua:
“Vichochezi vingine ni pamoja na kukosa pumzi wakati wa usingizi (sleep apnea), msongo wa mawazo, na wasiwasi wa kihisia. Vitu hivi vyote huongeza uwezekano wa mtu kuzungumza akiwa usingizini. Aidha, utafiti mmoja wa kisayansi umeonesha kuwa urithi wa kinasaba (genetics) huweza kuchangia. Ikiwa mzazi au ndugu yako wa karibu ana tabia ya kuongea usingizini, kuna uwezekano mkubwa nawe ukaipata.”
Kuhusu kama maneno yanayozungumzwa usingizini yana maana au la, Dkt. Gharaibeh alisema:
“Mara nyingi maneno hayo huwa yanaeleweka kimuundo lakini hayana maana yoyote halisi. Huwa ni kauli zisizo na muktadha, miito, au sauti za kawaida. Mtu hawezi kuyakumbuka kwa sababu hutokea katika hatua ya usingizi ambapo kumbukumbu haifanyi kazi kikamilifu.”
Je, hali hii ni dalili ya ugonjwa?
Dkt. Gharaibeh anasema kuwa:
“Kwa kawaida, kuongea usingizini si dalili ya ugonjwa wowote wa kiafya, isipokuwa kwa watu wa umri wa zaidi ya miaka 50. Ikiwa kuzungumza kunahusisha pia harakati nyingi za mwili katika hatua ya ndoto inayoitwa REM (Rapid Eye Movement), basi huenda ikawa ni dalili ya hali ya kiafya ijulikanayo kama REM Behavior Disorder.”
Hali hii huhusisha mtu kuigiza ndoto kwa kufanya harakati za ghafla na wakati mwingine za vurugu kwa mikono na miguu, na inaweza kuwa ishara ya ndoto za kutisha. Hali hiyo huweza kuthibitishwa kupitia uchunguzi wa kina wa usingizi (sleep study).
Utafiti wa kisayansi uliofanyika mwaka 2021 ulibaini kuwa baadhi ya watu wanaweza kujibu maswali ya sauti wakiwa katika usingizi wa REM, na hata kushiriki katika mazungumzo mafupi bila wao kujua.
Hadi miaka ya 1950, wataalamu walidhani usingizi ni hali ya kupumzika ambapo mwili na akili husitisha shughuli zake ili kupata nafuu.
Lakini tafiti za kisasa zimeonesha kuwa usingizi ni mchakato hai unaojumuisha kazi mbalimbali muhimu kama uchakataji wa kumbukumbu, udhibiti wa mfumo wa mwili, na usafishaji wa sumu kutoka kwenye ubongo.
Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu huongea usingizini angalau mara moja katika maisha yao.
Chanzo cha picha, Getty Images
Hali ya kuzungumza usingizini ni ya kawaida sana
Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2020 uliofanywa na American Academy of Sleep Medicine (AASM), hali ya kuzungumza usingizini ni ya kawaida sana.
Inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 60 hadi 65 ya watu wazima wamewahi kukumbwa nayo.
Kwa watoto, asilimia hufikia 50, ilhali kwa watu wazima hali hii hupungua hadi asilimia 5.
Rashad, mvulana mwenye umri wa miaka 13, aliambia BBC:
“Kaka yangu aliyelala nami alinieleza kuwa huwa naongea usingizini bila kujua. Alisema mara nyingi ninatamka maneno yasiyoeleweka.”
“Hii hutokea sana wakati wa vipindi vya mitihani shuleni, pengine kutokana na msongo wa mawazo. Baba yangu na mjomba wangu pia wana tabia kama hiyo, kwa hivyo huenda ni suala la kurithi.”
Alieleza kuwa alipozungumza na mtaalamu wa usingizi, alithibitishiwa kuwa hali hiyo ni ya kawaida na haina sababu ya kutia hofu.
Ndoto ni kama filamu ya akili
Dkt. Sahem Al-Rawabdeh, mtaalamu wa magonjwa ya akili na tiba ya uraibu, aliambia BBC kuwa:
“Usingizi ni sehemu muhimu ya maisha ya mwanadamu, na mahitaji ya usingizi hutegemea umri. Watoto huhitaji usingizi zaidi kuliko watu wazima. Usingizi hugawanyika katika hatua mbili: REM (harakati za macho) na non-REM (bila harakati za macho), ambazo zote huhusiana na michakato ya kibaolojia na ya kihisia.”
Alisema kuwa kila binadamu huota ndoto kila baada ya dakika 90, na kila ndoto hudumu kwa dakika 15.
“Hakuna binadamu asiyeota ndoto, tofauti ni kuwa wengi hukumbuka ndoto zilizotokea karibu na muda wa kuamka.”
Akaongeza:
“Ndoto inaweza kufananishwa na filamu fupi ambapo watu, wanyama, au vitu vingine hujitokeza na matukio mbalimbali hutokea. Katika filamu hii, mtu anaweza kusema maneno fulani, lakini maana ya maneno hayo hutegemea yaliyomo katika ndoto.”
Kwa mfano, katika ndoto za kutisha (jinamizi), mtu anaweza kupiga kelele, kuomba msaada, au kutoa sauti nyingine, kulingana na hofu anayopitia usingizini.
Sababu nyingi huathiri aina na ubora wa ndoto:
- Hali ya mwili (njaa, kushiba kupita kiasi, homa, kichwa kuuma)
- Hali ya kimazingira (chumba kuwa na joto au baridi, kitanda kisicho na starehe)
- Hali ya kiakili na kihisia (wasiwasi, huzuni, mfadhaiko)
- Na sababu za kina za kisaikolojia, kama vile matamanio yaliyofichika au hisia za uhasama zilizozimwa ndani ya nafsi.
Chanzo cha picha, Getty Images
Jinsi ya kupunguza tabia ya kuzungumza usingizini
Kwa mujibu wa Dkt. Tareq Gharaibeh, kuzungumza usingizini kwa kawaida si hali inayohitaji matibabu maalum, isipokuwa iwapo itakuwa ya mara kwa mara na kuathiri usingizi wa mtu au wa wengine wanaolala karibu naye.
“Watu wanaokumbwa na tabia hii wanashauriwa kuhakikisha wanapata usingizi wa kutosha takribani saa 6 hadi 8 kila usiku na kwa ratiba inayofuatwa kwa uthabiti. Pia ni vyema kuepuka vinywaji vyenye kafeini kama vile kahawa, chai nzito, na baadhi ya vinywaji baridi,” alieleza.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupunguza viashiria vya msongo wa mawazo na wasiwasi wa kihisia, ambavyo mara nyingi huchangia kuongezeka kwa hali ya kuzungumza usingizini.
Dkt. Sahem Al-Rawabdeh naye alikubaliana na maoni haya, na kuongeza kuwa:
“Kwa hakika, hakuna sababu ya kutibu hali hii endapo haiingilii utaratibu wa kawaida wa usingizi au haihusishi hisia kali kama kupiga kelele au kufanya harakati za ghafla. Iwapo hali hii itajitokeza kwa namna hiyo, basi ni busara kumuona mtaalamu wa afya ya akili kwa ajili ya tathmini na, ikihitajika, ushauri nasaha au tiba ya kisaikolojia.”
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid