o

    • Author, Justin Rowlatt
    • Nafasi, BBC

Mwanzilishi wa kampuni ya Cleankill, Clive Bury – iliyopewa jukumu la kudhibiti wadudu kwenye mashamba kusini mwa Uingereza, anasema ameona ongezeko “la ajabu” la panya, na kukadiria ongezeko la 20% katika miaka miwili iliyopita.

Ongezeko linaripotiwa kote nchini Uingereza. Shirika la Kudhibiti Wadudu waharibifu Uingereza (BPCA) linasema zaidi ya nusu ya makampuni ya kudhibiti wadudu ambayo ni wanachama wa shirika hilo, wameona ongezeko la panya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kwa sababu panya huishi kwenye mifereji ya maji, mitaro na mashimo, na hujitokeza zaidi usiku, kuwahesabu ni jambo gumu, kwa hivyo makadirio ya idadi ya panya hutofautiana. Huko Uingereza idadi inaweza kuwa kati ya milioni 10 hadi milioni 120.

Kinachojulikana ni kwamba zaidi ya panya nusu milioni waliripotiwa kwa halmashauri za Uingereza, kati ya 2023 na katikati ya mwaka huu, kulingana na kampuni ya kutengeneza mifereji ya maji, Drain Detectives.

Lakini sio tu Uingereza. Idadi ya panya inaripotiwa kuongezeka katika miji kadhaa ya Marekani, ikiwa ni pamoja na Washington DC, San Francisco na New York City, pamoja na Amsterdam na Toronto.

Ingawa kwa asili panya si wanyama wachafu, lakini hukimbilia katika mifereji ya maji machafu na mapipa ya taka na wanaweza kuambukiza magonjwa hatari kwa wanadamu.

Homa ya Mgunda (Leptospirosis) huambukizwa kupitia mkojo wa panya, na maambukizi ya virusi vya Hanta kutoka kwa panya, unaweza kuvipata kwa njia ya hewa kupitia kinyesi kilichoambukizwa. Panya pia hula mazao ya shambani na kuchafua chakula.

Swali ni kwamba, kipi kimechangia panya kuongezeka?

Kupanda kwa joto

O

Chanzo cha picha, Bobby Corrigan

Niall Gallagher, meneja wa ufundi katika kampuni ya BPCA, anasema, matumizi yaliyoongezeka ya chakula cha makopo, baadhi ya halmashauri hukusanya taka mara chache, pamoja na kazi za barabara na ujenzi zinazovuruga miundo mbinu ya maji taka, zote zinachangia.

Lakini kuna ushahidi kwamba kupanda kwa joto kunaweza pia kuwa sababu. Ushahidi wa kisayansi umegundua kwamba idadi ya panya huongezeka kutokana na halijoto.

Dk Dr Bobby Corrigan, mtaalamu wa wadudu jamii ya panya, ambaye alifanya kazi katika Idara ya Afya ya Jiji la New York kama mwanasayansi wa utafiti, pamoja na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Richmond, Virginia, waliamua kutafiti ikiwa kuongezeka kwa shughuli za panya kunahusiana na ongezeko la joto.

Utafiti wao ulichunguza miji 16, hasa Amerika Kaskazini, na matokeo, yaliyochapishwa katika jarida la Science Advances mapema mwaka huu, yaligundua miji 11 yalirikodi ongezeko kubwa la shughuli za panya katika kipindi cha kati ya miaka saba na 17.

Huko Washington DC ongezeko la panya lilikuwa karibu 400%, huko San Francisco ni 300%, Toronto 180% na New York 160%. Miji mitatu pekee iliyoshuhudia kupungua kwa panya, ni pamoja na Tokyo na New Orleans.

“Miji inayokumbwa na ongezeko kubwa la joto, ilirikodi ongezeko kubwa la panya,” utafiti uligundua. Ongezeko hilo lilikaribia 2C katika baadhi ya maeneo wakati wa kipindi cha utafiti.

Dk Corrigan anaamini – mradi halijoto inaendelea kuongezeka, na hasa majira ya baridi kali kuwa na joto – ongezeko la idadi ya panya huenda likaendelea.

Na halijoto ya kimataifa kwa hakika inatazamiwa kupanda kati ya nyuzijoto 1.9C na 2.7C juu ya wastani wa kabla ya viwanda kufikia 2100, kulingana na Climate Action Tracker, kundi la watafiti huru wa hali ya hewa.

Panya hawawezi kudhibiti joto la miili, hivyo wanapopatwa na baridi, wanaweza kufariki moja kwa moja au kuwafanya wazae watoto wachache.

Kwa kawaida panya anaweza kuzaa watoto mara sita kwa mwaka, na kila mara moja anaweza kuzaa watoto 12. Panya wanaweza kuanza kuzaliana baada ya wiki tisa ya kuzaliwa.

Watafiti wanasema idadi ina uwezekano mkubwa wa kuongezeka katika miji. Hiyo ni kwa sababu lami na majengo, huhifadhi joto kuliko maeneo ya vijijini.

Na mtindo wa watu kuhama kutoka maeneo ya mashambani hadi mijini unachangia pia, kulingana na Dk Corrigan.

“Ardhi inatoweka, na tunapojenga majengo, tunapunguza makazi yao [panya] porini,” anasema.

Majengo yakiwa mengi, inamaanisha mabomba na mifereji ya maji machafu hoongezeka na kuwapa panya sehemu ya kuishi.

Nguvu ya panya

V

Moja ya ukweli wa ajabu kuhusu panya – kwa nini sumu mara nyingi hazifanyi kazi – ni kwa sababu hawawezi kutapika.

Kinadharia hii ina maana kwamba mara sumu ya panya inapomezwa, hawawezi kutapika na kuitoa. Lakini panya pia wanaogopa mambo mapya, kulingana na Profesa Steven Belmain, profesa wa ikolojia katika Chuo Kikuu cha Greenwich.

“Panya wanapokutana na chakula hawavamii tu nakula. Watajaribu kidogo tu. Kwa hivyo wakishaelewa kuwa hawajisikii wagonjwa, ndio wataendelea kula.”

“Mtazamo huu wa tahadhari kuhusu maisha unawasaidia vyema,” anasema.

Dk Alan Buckle wa Chuo Kikuu cha Reading ametumia miaka 30 akifanya kazi ya kutengeneza sumu mpya ya panya lakini – ananiambia kwa kicheko – “nimeshindwa.”

Ikiwa sumu ina ladha mbaya au husababisha usumbufu au maumivu kwa panya, hawatakula. Ndiyo maana sumu zinazouwa polepole – kama dawa zinazofanya damu iwe nyepesi, ndio hutumiwa.

Sumu za aina hiyo huchukua hadi wiki kufanya kazi, na paya huwa na muda wa kutosha kula dozi ya kuua sumu. Lakini hiyo ni njia ya kikatili ya kuuwa panya, kusababisha kutokwa na damu ndani.

Zaidi ya hayo, katika miaka ya hivi majuzi panya wametengeneza mabadiliko ya chembe za urithi ambazo huwapa kinga fulani kwa dawa hizi zenye nguvu.

Watafiti wengine wanaangalia uwezekano wa kutumia uzazi wa mpango, kama njia mbadala, kuzuia idadi ya panya kukua zaidi.

Kipi cha kufanya?

K

Chanzo cha picha, New York

Badala ya kuweka takataka za mitaani kwenye mifuko ya plastiki, sasa wakazi wengi wa New York wanalazimika kuweka taka zao kwenye mapipa ili kuzuia panya.

“Kukata chanzo cha chakula cha panya ni ufunguo wa kupunguza idadi ya panya,” anasema Kathleen Corradi, Mwalimu wa zamani ambaye aliteuliwa na Meya wa New York, kutoa elimu kuhusu panya katika jiji hilo mwaka 2023.

Ni vigumu kudhibiti panya ikiwa kuna chakula kingi mtaani. Na mara tu mapipa haya yanapo vamiwa na panya, wakusanyaji taka hawataki tena kuchukua taka hizo.

Halijoto inaweza kuongezeka idadi ya panya lakini mapipa yaliyofurika taka, kupenda chakula cha makopo, vyote hivyo huongeza changamoto ya kudhibiti panya.

Nchini Uingereza kuna watu wengi zaidi kuliko hapo awali. Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya idadi ya watu inasema watu wameongezeka kutoka milioni 67.6 mwaka 2022 hadi milioni 72.5 ifikapo 2032, huku idadi ya wanaoishi mijini ikiongezeka pia.

“Ikiwa tutatunza mazingira ya jiji letu, basi hatutakuwa na wasiwasi juu ya panya,” anasema Dk Corrigan.

“Kwa kutowapa panya fursa ya kupata chakula, basi haitokuwa lazima tuwape sumu na kuwaua na kuwatesa,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *