gg

Chanzo cha picha, Serenity Strull/ BBC

Hofu ni mbinu ya kiasili ya kujilinda na kuendelea kuishi. Hata hivyo, kuna watu wachache sana walio na hali ya nadra inayowafanya wasihisi hofu kabisa. Je, maisha bila hofu huwa vipi?

Fikiria kuruka kutoka kwenye ndege bila kuhisi chochote hakuna msisimko wa adrenalini, wala mapigo ya moyo kuongezeka.

Huo ndio uhalisia wa maisha ya Jordy Cernik, Muingereza ambaye aliondolewa tezi zake za adrenal ili kupunguza wasiwasi uliosababishwa na ugonjwa wa Cushing, hali adimu ambapo tezi za adrenal huzalisha kiwango kikubwa mno cha cortisol, homoni ya msongo wa mawazo.

Matibabu hayo yalifanya kazi, lakini kwa kiwango kisichotarajiwa.

Jordy aliacha kuhisi wasiwasi lakini pia akaacha kuhisi hofu kabisa.

Katika safari yake ya kwenda Disneyland mwaka 2012, alipanda treni ya mteremko (rollercoaster) na kugundua kuwa hakuhisi hofu hata kidogo.

Baada ya hapo, aliruka kwa parachuti kutoka angani, akateleza kwa kamba (zipline) kutoka Daraja la Tyne huko Newcastle, na kushuka kwa kamba kwenye jengo la The Shard jijini London yote haya bila hata mshtuko mdogo wa moyo.

Tukio la Jordy ni la kipekee, lakini si la kipekee kabisa.

Linafanana na hali inayowapata watu wachache sana duniani wenye ugonjwa wa Urbach-Wiethe unaojulikana pia kama lipoid proteinosis.

Ni ugonjwa wa kurithi adimu sana, na hadi sasa, ni watu takriban 400 tu waliowahi kugundulika kuwa nao duniani kote.

Mmoja wa wagonjwa maarufu zaidi wa Urbach-Wiethe ni mgonjwa anayefahamika kwa kifupi kama SM, ambaye amekuwa akifanyiwa utafiti katika Chuo Kikuu cha Iowa, Marekani, tangu katikati ya miaka ya 1980.

Katika miaka ya 2000, Justin Feinstein, aliyekuwa mwanafunzi wa uzamili, alijiunga na timu ya watafiti waliokuwa wakimchunguza SM akianza kutafuta njia mbalimbali za kumtia hofu.

“Tulimwonyesha kila filamu ya kutisha tuliyoweza kupata,” anasema Feinstein, ambaye sasa ni mwanasaikolojia wa kitabibu katika Float Research Collective, taasisi inayopendekeza tiba ya kupunguza msisimko wa mazingira kwa njia ya kuogelea kimya kimya (Floatation REST) kama tiba ya maumivu, msongo na hofu.

Lakini hata baada ya kuonyeshwa filamu kama The Blair Witch Project, Arachnophobia, The Shining, na Silence of the Lambs, SM hakuhisi hofu yoyote.

Ziara katika Waverley Hills Sanatorium, jumba la kihistoria linalodaiwa kuwa la kutisha, pia haikumletea mshituko.

“Tulimkutanisha na vitisho vya moja kwa moja kama nyoka na buibui. Lakini si tu kwamba hakuonyesha hofu alikuwa na hamu ya kuwakaribia na kuwatambua,” anasema Feinstein. “Alionyesha udadisi wa kipekee alitaka kuwagusa na kujihusisha nao.”

Utafiti wa wale walio na amygdala zilizoharibiwa unatuonyesha sio wote hofu ni sawa - majibu yetu kwa vitisho vya nje vinavyotambulika ni sehemu ya silika yetu ya kuishi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Ugonjwa wa Urbach-Wiethe husababishwa na mabadiliko kwenye jeni ya ECM1, inayopatikana kwenye kromosomu ya 1.

Jeni hii huzalisha protini muhimu inayosaidia kushikilia seli na tishu za mwili pamoja kupitia extracellular matrix (ECM).

Uharibifu wa ECM1 husababisha mkusanyiko wa kalsiamu na kolajeni, hali inayopelekea kifo cha seli.

Eneo moja la ubongo linaloathirika sana ni amygdala, sehemu yenye umbo la mlozi inayojulikana kwa kuchakata hisia za hofu.

Kwa SM, hofu ilikoma kabisa pale ugonjwa huo ulipoharibu amygdala yake.

“Kitu cha ajabu ni kwamba hasara hiyo ni maalumu kwa hofu tu lakini uwezo wake wa kuhisi furaha, huzuni au hasira bado uko sawa,” anasema Feinstein.

Soma pia:

Aina za hofu

Hata hivyo, utafiti umebaini kuwa amygdala haishughulikii kila aina ya hofu kwa kiwango sawa.

Inaonekana inahusika zaidi katika mazoea ya kujifunza kuogopa (fear conditioning).

Katika majaribio ya wanyama, panya anayepigwa shoti ya umeme kila mara baada ya sauti hujifunza kuihofia sauti hiyo peke yake.

Ingawa SM anajua kutogusa sufuria moto, hawezi kufundishwa kuogopa kwa njia hiyo yaani, hatetemeki wala kupata msisimko anapokumbana na kitu kilichowahi kumsababishia maumivu.

Pia, hawezi kutambua nyuso za watu walioko katika hofu, japokuwa anaweza kutambua hisia za huzuni au furaha.

Ni mtu wa watu na hupenda mazungumzo, lakini ana shida kutambua hatari.

Mara kadhaa, amewahi kutishiwa kwa visu na bunduki.

Katika utafiti mwingine, ilibainika kuwa SM anapendelea watu kuwa karibu sana naye kimwili yaani umbali wa wastani wa sentimita 34 tu karibu nusu ya umbali unaopendelewa na watu wengine.

“Katika hali hiyo, watu kama SM wenye uharibifu wa amygdala hukaribia hata watafiti wasiofahamu vizuri jambo ambalo watu wenye amygdala inayofanya kazi hawafanyi kamwe,” anasema Profesa Alexander Shackman, wa Chuo Kikuu cha Maryland, Marekani.

Mara nyingi tunahisi makali ikiwa tunafikiwa kwa karibu sana; wale walio na amygdala zilizoharibiwa hawahisi hii kwa ukali

Chanzo cha picha, Getty Images

Licha ya yote hayo, kuna aina ya hofu inayoweza kutokea hata bila amygdala.

Katika jaribio moja, Feinstein na timu yake walimfanya SM avute hewa yenye viwango vya juu vya dioksidi ya kaboni (CO₂) hali inayowafanya watu wengine kuhisi hofu ya kufa au kukosa pumzi.

Kwa mshangao wao, SM alipatwa na hofu kali.

Wagonjwa wawili wengine wenye uharibifu wa amygdala pia walihisi vivyo hivyo.

“Kwa SM, ilikuwa ni shambulio kamili la hofu (panic attack) hofu kali zaidi aliyowahi kuhisi katika maisha yake ya utu uzima,” anasema Feinstein.

Ugunduzi huu uliwaongoza watafiti kuelewa kuwa kuna njia mbili tofauti za hofu katika ubongo moja hushughulikia vitisho vya nje (kama nyoka, mwizi, au kiumbe wa kutisha), nyingine hushughulikia vitisho vya ndani (kama hisia ya kukosa pumzi).

Katika vitisho vya nje, amygdala huchochea muundo mdogo lakini muhimu ndani ya ubongo ambao hufanya kama kituo cha udhibiti wa mwili hypothalamus, ambayo huwasiliana na tezi ya pituitari, kisha kusababisha tezi za adrenal kutoa adrenalini na cortisol homoni za msisimko wa “pigana-au-kimbia”.

Mhusika SM aliruka kutoka kwenye ndege kwenye anga na hakuhisi hofu kwa sababu ya hali yake

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa vitisho vya ndani kama kuongezeka kwa CO₂, ubongo huchochea hofu kupitia muundo unaofanana na bua unaounganisha ubongo na uti wa mgongo, uliotengenezwa na ubongo wa kati, poni, na medula oblongata brainstem sehemu ya ubongo inayosimamia kupumua na kazi nyingine za mwili zisizo na hiari.

Katika hali hii, amygdala huwa kama breki, ikiizuia hofu.

Kwa hiyo, watu waliopoteza amygdala kama SM hukumbwa na hofu kali zaidi kwa sababu hakuna kinachozuia mwitikio huo wa ndani.

“Ugunduzi huu ni wa maana sana,” anasema Shackman.

“Unatuonyesha kuwa amygdala si lazima kwa kila aina ya hofu, wasiwasi au mshuko wa moyo. Inaonekana kuwa muhimu zaidi kwa kutambua vitisho vya nje lakini si kwa kuanzisha hofu inayotokana na vitisho vya ndani.”

Je, hofu inahitajika tena?

Bila shaka, SM ni mtu mmoja tu, hivyo si rahisi kuhitimisha kuwa hali yake inawakilisha wote.

Lakini kinachofanya hadithi yake kuwa ya kipekee ni kwamba ugonjwa wake uliharibu amygdala kabisa, huku sehemu nyingine za ubongo zikibaki salama.

Hata hivyo, watu hupokea jeraha la ubongo kwa namna tofauti, kulingana na umri na mazingira.

Lakini simulizi la SM linatufundisha kwanini hofu ilibuniwa na mabadiliko ya viumbe.

Wanyama wote wenye uti wa mgongo wakiwemo mamalia, ndege, samaki na reptilia wana amygdala.

Ni chombo muhimu sana kwa kuendelea kuishi.

“Ukiharibu amygdala ya mnyama kisha ukamrudisha porini, mara nyingi hufa.

unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *