cx

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Joseph Kabila
amehukumiwa kifo bila kuwepo mahakamani kwa uhalifu wa kivita na uhaini.

Mashtaka hayo yanamshutumu Kabila kuunga mkono kundi la M23, kundi la
waasi ambalo limesababisha uharibifu katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Kabila alitiwa hatiani siku ya Ijumaa na mahakama ya kijeshi kwa uhaini,
uhalifu dhidi ya ubinadamu, na uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji,
unyanyasaji wa kingono, mateso na uasi.

Alikana mashtaka, lakini hakufika mahakamani kujitetea. Pia Kabila aliikataa
kesi hiyo na kusema mahakama inatumiwa kama “chombo cha
ukandamizaji”. Kwa sasa hajulikani alipo.

Mzee huyo mwenye umri wa miaka 54 aliiongoza DR Congo kwa miaka 18,
baada ya kumrithi babake Laurent, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi mwaka 2001.

Kabila alikabidhi madaraka kwa Rais Félix Tshisekedi mwaka 2019, lakini
baadaye walitofautiana na akaenda uhamishoni mwaka 2023.

Mwezi Aprili mwaka huu, rais huyo wa zamani alisema anataka kusaidia
kutafuta suluhu ya mgogoro katika eneo la mashariki na aliwasili katika mji
unaoshikiliwa na M23 wa Goma mwezi uliofuata.

Rais Tshisekedi alimshutumu Kabila kwa nyuma ya M23 na maseneta walimwondolea
kinga yake ya kisheria, na ikawa rahisi kufunguliwa mashitaka.

Mapema mwaka huu M23 ilitwaa udhibiti wa maeneo makubwa ya mashariki
yenye utajiri wa madini, ikiwa ni pamoja na Goma, jiji la Bukavu na viwanja
viwili vya ndege.

Umoja wa Mataifa na nchi kadhaa za Magharibi zimeishutumu nchi jirani ya
Rwanda kwa kuunga mkono M23, na kutuma maelfu ya wanajeshi wake nchini DR
Congo.

Lakini Kigali inakanusha mashtaka hayo, na inazuia mzozo huo kusambaa
katika eneo lake.

Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya waasi na serikali yalifanyika
mwezi Julai, lakini umwagaji damu umeendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *