.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Mpango wa Donald Trump wa kumaliza vita huko Gaza umekubaliwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, wakati Hamas bado haijatoa jibu rasmi.

Tunakufahamisha kwa ukamilifu mpango huo kama ulivyotolewa na Ikulu ya White House:

1. Gaza itakuwa eneo lisilo na ugaidi na ambalo sio tishio kwa majirani zake.

2. Gaza itaendelezwa upya kwa manufaa ya watu wa Gaza, ambao wameteseka vya kutosha.

3. Ikiwa pande zote mbili zitakubaliana na pendekezo hili, vita vitamalizika mara moja. Vikosi vya Israel vitaondoka kujiandaa kuachiliwa kwa mateka. Wakati huu, shughuli zote za kijeshi, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga, zitasitishwa, hadi masharti yatimizwe ya kujiondoa kabisa hatua kwa hatua.

4. Ndani ya saa 72 baada ya Israeli kukubali hadharani makubaliano haya, mateka wote, walio hai na waliokufa, watarudishwa.

5. Mara tu mateka wote watakapoachiliwa huru, Israel itawaachilia wafungwa 250 waliohukumiwa kifungo cha maisha pamoja na Wagaza 1,700 ambao walizuiliwa baada ya tarehe 7 Oktoba 2023, wakiwemo wanawake na watoto wote waliozuiliwa katika mazingira hayo. Kwa kila mateka wa Israel aliyekufa atakayeachiliwa huru, Israel itaachilia raia 15 wa Gaza waliokufa.

6. Mara tu mateka wote watakaporudishwa, wanachama wa Hamas wanaojitolea kuishi pamoja kwa amani na kuweka silaha chini watasamehewa. Wanachama wa Hamas wanaotaka kuondoka Gaza watapewa njia salama ya kuondoka hadi nchi watakazoenda.

7. Baada ya kukubalika kwa makubaliano haya, msaada kamili utatumwa mara moja katika Ukanda wa Gaza. Kiasi cha chini zaidi cha misaada kitalingana na kile kilichojumuishwa katika makubaliano ya 19 Januari 2025 kuhusu misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu (maji, umeme, maji taka), ukarabati wa hospitali na maeneo ya kutengeneza mikate, na kuingia kwa vifaa muhimu vya kuondoa vifusi na kufungua barabara.

8. Kuingia na usambazaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza kutaendelea bila kuingiliwa na pande hizo mbili kupitia Umoja wa Mataifa na mashirika yake, na Shirika la Msalaba Mwekundu, pamoja na taasisi nyingine za kimataifa zisizohusishwa kwa namna yoyote na upande wowote. Kufungua kivuko cha Rafah katika pande zote mbili kutategemea utaratibu ule ule ulioko chini ya makubaliano ya tarehe 19 Januari 2025.

9. Gaza itaongozwa chini ya utawala wa mpito wa muda wa kamati ya wataalamu, ya kisiasa ya Wapalestina, yenye kujukumika na uendeshaji wa kila siku wa huduma za umma na manispaa kwa watu wa Gaza. Kamati hii itaundwa na Wapalestina waliohitimu na wataalam wa kimataifa, na usimamizi wa chombo kipya cha mpito cha kimataifa, “Bodi ya Amani,” ambayo itaongozwa na Rais Donald J. Trump, na wajumbe wengine na wakuu wa nchi watakaotangazwa, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair. Chombo hiki kitaweka mfumo na kushughulikia ufadhili wa maendeleo ya Gaza hadi wakati ambapo Mamlaka ya Palestina imekamilisha mpango wake wa mageuzi, kama ilivyoainishwa katika mapendekezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mpango wa amani wa Rais Trump mwaka 2020 na pendekezo la Saudi-Ufaransa, na inaweza kuchukua udhibiti wa Gaza kwa ufanisi. Chombo hiki kitatoa wito wa viwango bora vya kimataifa ili kuunda utawala wa kisasa wenye ufanisi wa kuhudumia watu wa Gaza na unaofaa kuvutia uwekezaji.

10. Mpango wa maendeleo ya uchumi wa Trump wa kujenga upya Gaza utaundwa kwa kuitisha jopo la wataalamu ambao wamesaidia katika ukuzaji wa baadhi ya miji inayostawi ya kisasa katika Mashariki ya Kati. Mapendekezo mengi ya kuvutia ya uwekezaji na mawazo ya kusisimua ya maendeleo yataundwa na makundi ya kimataifa yenye nia njema, na yatazingatiwa ili kuunganisha mifumo ya usalama na utawala ili kuvutia na kuwezesha uwekezaji huu ambao utaunda nafasi za ajira, fursa, na matumaini kwa Gaza ya baadaye.

11. Ukanda maalum wa kiuchumi utaanzishwa na ushuru unaopendekezwa vitajadiliwa na nchi zinazoshiriki.

12. Hakuna mtu atakayelazimishwa kuondoka Gaza, na wale wanaotaka kuondoka watakuwa huru kufanya hivyo na uhuru wa kurudi. Watu watahimizwa kubaki na kuwapa fursa ya kujenga Gaza bora.

13. Hamas na makundi mengine yakubali kutokuwa na jukumu lolote katika utawala wa Gaza, moja kwa moja, kwa njia isiyo ya moja kwa moja, au kwa namna yoyote ile. Miundombinu yote ya kijeshi, ugaidi na ya kufanya mashambulizi, ikijumuisha mahandaki na vituo vya utengenezaji wa silaha, vitaharibiwa na havitajengwa upya. Kutakuwa na mchakato wa kuondoa jeshi la Gaza chini ya usimamizi wa wachunguzi huru, ambao utajumuisha silaha kutotumiwa tena kupitia mchakato uliokubaliwa wa usitishaji matumizi, na kuungwa mkono mpango unaofadhiliwa kimataifa wa kununua na kurejesha tena mipango yote iliyothibitishwa na wachunguzi huru. Gaza mpya itajitolea kikamilifu kujenga uchumi wenye ustawi na kuishi pamoja kwa amani na majirani zao.

14.Dhamana itatolewa na washirika wa kikanda ili kuhakikisha kwamba Hamas, na makundi mengine, yanatii wajibu wao na kwamba Gaza mpya haileti tishio kwa majirani zake au watu wake.

15. Marekani itafanya kazi na washirika wa Kiarabu na kimataifa ili kuunda Kikosi cha muda cha Kimataifa cha Utulivu (ISF) kitakachopelekwa mara moja Gaza. ISF itatoa mafunzo na kutoa msaada kwa vikosi vya polisi vya Palestina vilivyohakikiwa huko Gaza, na itashauriana na Jordan na Misri ambao wana uzoefu mkubwa katika upande huu. Kikosi hiki kitakuwa suluhisho la usalama wa ndani wa muda mrefu. ISF itashirikiana na Israel na Misri kusaidia usalama wa maeneo ya mpakani, pamoja na askari wapya wa polisi wa Palestina waliopata mafunzo. Ni muhimu kuzuia zana za kivita kuingia Gaza na kuwezesha mtiririko wa haraka na salama wa bidhaa ili kujenga upya na kuhuisha Gaza. Utaratibu wa kumaliza migogoro utakubaliwa na wahusika.

16. Israeli haitaikalia wala kuiunganisha Gaza. Wakati ISF inapoweka udhibiti na uthabiti, Vikosi vya Ulinzi vya Israeli (IDF) vitajiondoa kwa kuzingatia viwango, hatua muhimu, na muda uliowekwa unaohusishwa na uondoaji wa kijeshi ambao utakubaliwa kati ya IDF, ISF, wadhamini na Marekani, kwa madhumuni ya Gaza salama ambayo haileti tishio tena kwa Israeli, Misri, au raia wake. Kiuhalisia, IDF itaendelea kukabidhi eneo la Gaza inalokalia kwa ISF kulingana na makubaliano watakayofanya na mamlaka ya mpito hadi watakapoondolewa kabisa kutoka Gaza, isipokuwa uwepo wa eneo salama litakaloendelea kuwepo hadi Gaza iwe salama ipasavyo kutokana na tishio lolote la ugaidi linaloweza kuzuka tena.

17. Iwapo Hamas itachelewesha au kukataa pendekezo hili, yaliyo hapo juu, ikijumuisha oparesheni iliyoongezwa, itaendelea katika maeneo yasiyo na ugaidi ambayo IDF imekabidhi kwa ISF.

18. Mchakato wa mazungumzo baina ya dini mbalimbali utaanzishwa kwa kuzingatia maadili ya kuvumiliana na kuishi pamoja kwa amani ili kujaribu kubadilisha mawazo na masimulizi ya Wapalestina na Waisraeli kwa kusisitiza faida zinazoweza kupatikana kutokana na amani.

19. Wakati maendeleo mapya ya Gaza yanapoendelea na wakati mpango wa mageuzi ya PA unafanywa kwa uaminifu, hatimaye, hali inaweza kuwa ya kuaminika ya kujitawala kwa Wapalestina na kuwa taifa, jambo ambalo tunatambua kama matarajio ya watu wa Palestina.

20. Marekani itaanzisha mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina ili kukubaliana juu ya upeo wa kisiasa wa kuishi pamoja kwa amani na ustawi.

Imefasiriwa na Asha Juma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *