.

Chanzo cha picha, Getty Images

Serikali ya Marekani imefungwa baada ya wabunge wa Republican na Democratic kushindwa kutatua mkwamo wa bajeti.

Mgogoro huo unaathiri ufadhili wa shughuli za serikali hadi Oktoba na baadaye na unakaribia kusababisha usumbufu mkubwa kwa Wamarekani katika maeneo kuanzia safari za ndege hadi kutembelea mbuga za wanyama.

Mtazamo wa kisiasa pia unatarajiwa kuweka 40% ya wafanyikazi wa shirikisho – takriban watu 800,000 – kwenye likizo za bila malipo.

Hivi ndivyo athari yake itakavyoonekana kote nchini.

Pia unaweza kusoma

Kuahirishwa kwa safari za ndege

Kufungwa kwa serikali kutaathisri usafiri wa ndege kwa njia mbalimbali, na hivyo kusababisha foleni ndefu, na ucheleweshaji unaosababishwa na wadhibiti wa trafiki wa anga ambao hawajalipwa hivyobasi kuwalazimu kukaa nyumbani badala ya kufanya kazi bila malipo.

Wafanyikazi wa Udhibiti wa trafiki ya anga na Utawala wa Usalama wa Usafiri (TSA) wanachukuliwa kuwa “muhimu”, kwa hivyo wataendelea kwenda kazini endapo serikali itafungwa.

Lakini hawatalipwa hadi serikali ifungue tena shughuli zake. Mara ya mwisho serikali ilipofungwa mnamo 2018-2019, wafanyikazi hawa walizidi kuwa wagonjwa , na kusababisha ucheleweshaji wa uwanja wa ndege.

Athari pia itahisiwa na Wamarekani wanaopanga kusafiri nje ya nchi, huku mashirika ya pasipoti ya Marekani yakionya kwamba inaweza kuchukua muda mrefu kuliko kawaida kuchakata hati za kusafiri.

Hakuna kazi – au malipo – kwa wafanyikazi wa shirikisho

Wafanyikazi wa shirikisho wanatarajiwa kuathirika zaidi, kwani hawatapokea hundi yoyote ya malipo wakati kufungwa kwa serikali kunaendelea.

Wafanyikazi wengine wanaweza kuchagua kuchukua kazi za pili, kama walivyofanya wakati wa kufungwa hapo awali. Wafanyikazi ambao hawachukuliwi kuwa muhimu watalazimika kukaa nyumbani. Katika siku za nyuma, wafanyakazi hawa wamekuwa wakilipwa moja kwa moja.

Mashirika kadhaa, kama vile Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa na Taasisi za Kitaifa za Afya zina uwezekano wa kuwaachisha kazi wafanyikazi wengi, na kuathiri utafiti unaoendelea na majaribio ambayo tayari yanaendelea.

Rais Donald Trump, ambaye amepunguza matumizi ya serikali na kukata kazi za shirikisho tangu aingie madarakani, alionya mara kwa mara kwamba kufungwa kwa serikali kunaweza kuongeza kasi ya kuachishwa kazi zaidi na kumruhusu kupunguza huduma na programu anazosema ni muhimu kwa Wanademokrasia.

Wakandarasi, wanaofanya kazi kwa mashirika ya shirikisho lakini hawajaajiriwa moja kwa moja na serikali, watakosa kazi pia. Wafanyakazi hawa kihistoria hawajapokea malimbikizi yoyote, kulingana na Kamati ya Bajeti ya Serikali inayowajibika.

Hifadhi za Taifa zisizo na wafanyakazi

Ardhi za Shirikisho, pamoja na Hifadhi za Kitaifa na Misitu ya Kitaifa, zimefungwa kwa wageni wakati wa kufungwa hapo awali, kwani walinzi na wafanyikazi wengine walitakiwa kukaa nyumbani.

Wakati serikali ilipofungwa mara ya mwisho, utawala wa Trump ulifanya uamuzi wa kuacha mbuga wazi, na wafanyikazi wachache wa shirikisho .

Kulingana na watetezi wa hifadhi hiyo, uamuzi huo ulisababisha uharibifu katika bustani, kwani wageni waliendesha gari kwenye mandhari iliyohifadhiwa, kupora maeneo ya kihistoria, na kuchafua maeneo.

Kundi la wasimamizi zaidi ya 40 wa zamani wa mbuga hiyo wametoa wito kwa Ikulu ya White House kufunga kabisa mbuga iwapo serikali itafungwa.

“Hatuachi majumba ya makumbusho wazi bila watunzaji, au viwanja vya ndege bila wadhibiti wa trafiki ya anga – na hatupaswi kuacha mbuga zetu za kitaifa wazi bila wafanyikazi wa Huduma ya Hifadhi ya Kitaifa,” Emily Thompson wa Muungano wa Kulinda Hifadhi za Kitaifa za Marekani alisema.

Ziara za bustani za wanyama

Makavazi maarufu ya Taasisi ya Smithsonian ya Washington DC yatakaa wazi hadi angalau Jumatatu ijayo, 6 Oktoba.

Kwenye wavuti wa Smithsonian, shirika hilo lilisema lilikuwa na pesa za miaka iliopita kusaidia kukaa wazi.

Wanyama katika Mbuga ya Wanyama ya Kitaifa “wataendelea kulishwa na kutunzwa,” kulingana na Smithsonian, ambayo inaendesha bustani hiyo.

Lakini kamera za wavuti maarufu zitazimwa, kwani zimechukuliwa kuwa sio muhimu na wafanyikazi wa bustani.

Kusimamishwa kwa matangazo hayo kutavuruga watazamaji kutazama panda, simba, tembo na panya wa mbuga hiyo.

Huduma ya afya kwa wazee na maskini

Medicare na Medicaid, programu za afya ya jamii kwa wazee na maskini, zitaendelea, lakini uhaba wa wafanyakazi unaweza kusababisha kukatizwa kwa baadhi ya huduma hizo.

Msaada wa afya ya dharura pia unatarajiwa kwa kiasi kikubwa kutoathiriwa, hata hivyo kazi nyingine zinazofanywa na mashirika ya dharura zitaathirika.

Mpango wa Kitaifa wa Bima ya Mafuriko utafungwa, na hivyo kuchelewesha baadhi ya rehani kwa mali zinazohitaji sera kutoka kwa mpango unaoendeshwa na serikali.

Lakini ikiwa kufungwa kutaendelea, kuna uwezekano kwamba Utawala wa Shirikisho wa Usimamizi wa Dharura (Fema) unaweza kukosa pesa za Hazina yake ya Kusaidia dharura.

Programu za usaidizi wa chakula pia zitaathiriwa, huku Mpango wa Lishe ya Ziada kwa Wanawake, Watoto wachanga na Watoto (WIC) ukitarajiwa kukosa fedha kwa haraka.

Mpango wa Usaidizi wa Lishe ya Ziada (uliojulikana zamani kama stempu za chakula) unatarajiwa kuendelea kwa muda mrefu, lakini pia uko katika hatari ya kukosa ufadhili.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *