CHAUMMA/CCM

Chanzo cha picha, CHAUMMA/CCM

“Kampeni za mwaka huu hazina mvuto ukilinganisha na miaka iliyopita,” anasema mchambuzi wa siasa za ndani, Mohamed Issa, akieleza hali ya kisiasa inavyoendelea nchini Tanzania mwezi mmoja tangu kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi mkuu Agosti 28, 2025.

Kwa sasa, picha kubwa inayoonekana ni chama tawala CCM kutawala anga la kisiasa kwa nguvu kubwa, likijaza viwanja vya mikutano na kuonekana peke yake katika sehemu nyingi za nchi. Vyama vingine vidogo vya upinzani vinavyoendelea na kampeni vimekosa rasilimali, nguvu na hata ufanisi wa kushawishi umma kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita.

Chama kikuu cha upinzani, Chadema, kilitangaza mapema kuwa hakitashiriki uchaguzi huu, hatua iliyosababisha pengo kubwa na kuondoa mvuto uliokuwa ukionekana miaka iliyopita. Kwa upande wa chama kingine cha upinzani chenye ukubwa, mgombea wake urais Dk. Luhaga Mpina bado hajaanza kampeni kutokana na kuenguliwa kwake na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kesi yake ikiendelea Mahakamani kupinga hatua hiyo.

Kwa mujibu wa rekodi za INEC, kati ya vyama 19 vilivyosajiliwa nchini, ni Chadema pekee kimeamua kutoshiriki uchaguzi wa mwaka huu, huku vyama vingine 18 vikijitosa, 17 vikisimamisha wagombea urais. Hali hii inafanya uchaguzi huu wa Oktoba 29 kuwa wa kipekee tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka1992 na uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995, kwani ni mara ya kwanza chama kikuu cha upinzani kinajitoa kabisa kushiriki uchaguzi mkuu.

“Hakuna upinzani imara”

A

Chanzo cha picha, CHAUMMA

Mchambuzi Mohamed Issa anabainisha zaidi hali hii:

“Hakuna chama chenye mizizi imara kwa upande wa upinzani kuweza kukabiliana na CCM. Hata mikutano ya vyama vinavyoendelea na kampeni haionekani kuleta shamrashamra kama miaka ya nyuma.”

Katika chaguzi za miaka iliyopita, vyama kama Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi au hata TLP vilikuwa na nafasi ya kuibua mijadala mikali na kushindana vikali na chama tawala. Mikutano ya kampeni ya upinzani mara nyingi ilikuwa na umati mkubwa wa watu, ikionyesha hisia za kisiasa zilizogawanyika zaidi miongoni mwa wananchi.

Lakini mwaka huu hali hiyo haipo. Badala yake, CCM imeonekana kutawala kabisa uwanja wa kampeni, ikifanya mikutano mikubwa inayojaza maelfu ya wananchi huku wapinzani wakijikongoja na mikutano midogo isiyokuwa na uhamasishaji mkubwa.

Hata hivyo, sio kila mchambuzi anayeona hali hii kama ishara ya udhaifu wa demokrasia. John Ngwandu, mchambuzi wa masuala ya siasa aliyezungumza na Crown Media, anatoa mtazamo tofauti:

“Tunakwenda vizuri, vyama vyote vinavyoshiriki vinapambana kwa kadri vilivyojipanga.” Aligusia hayo alipohojiwa na Crown Media.

Kwa mujibu wake, hali ya kampeni sasa inaonyesha ushindani unaolingana na nguvu, maandalizi na rasilimali za kila chama. Anasisitiza kuwa, japo vyama vya upinzani havina ukubwa sawa, bado vinajitahidi kuweka ajenda zao mbele ya wapiga kura.

“Uchaguzi ni kama umemalizika”

UMD

Chanzo cha picha, eatv

Sauti za wananchi zinaonyesha mtazamo unaofanana kwa kiasi kikubwa na ule wa wachambuzi, hasa kuhusu ukosefu wa mvuto kwenye kampeni za mwaka huu.

Selemani Pacal, mkazi wa Dar es Salaam, anaona taswira ya kampeni kwa mtazamo wa matokeo:

“Uchaguzi ni kama umemalizika. Huoni ni kwanini CCM isishinde kwa kishindo kama utaangalia kampeni zilivyo?”

Mwananchi mwingine Naomi Metusela, anahisi kwamba kukosekana kwa Chadema kumeondoa ladha ya uchaguzi:

“Chadema kutokuwepo kumepunguza ladha ya uchaguzi. Ni kama uchaguzi hakuna. Mimi nimetembea Dar es Salaam hata bango moja la mgombea urais wa upinzani sijaona, naona CCM tu.”

Chadema yenyewe inasema kinachoendelea ni kiini macho, na huo ndiyo msingi wa kutoshiriki kwa uchaguzi wa mwaka huu, mpaka mifumo ua uchaguzi itakaporekebishwa ili kuwa na uchaguzi huru na wa waki na wenye ushindani.

HL

Chanzo cha picha, HL

Lakini si wote wanaojadili uchaguzi kwa mtazamo mmoja. Katika mazungumzo ya vijiweni, mijadala imegawanyika kati ya wanaozungumzia kampeni na uchaguzi wa Oktoba 29, na wale wanaojikita zaidi kwenye maandamano yaliyotangazwa kufanyika siku hiyo hiyo. Wapo wanaoona mjadala wa kura umepoteza mvuto na badala yake maandamano yanaibua hisia mpya za kisiasa.

Mchambuzi Issa anabainisha zaidi:

“Wakati fulani mikutano ya kampeni ilikuwa kivutio chenyewe. Vyama vya upinzani vilivyokuwa na nguvu kama CUF na Chadema vilileta hamasa kubwa. Lakini mwaka huu uchaguzi umedorora kiasi fulani tofauti na miaka ya nyuma.”

Kwa upande wa chama tawala, CCM, kwao uchaguzi huu umezingatia vigezo na utaratibu wote na ushahidi ni uwepo wa vyama 18 vinavyoshiriki kasoro Chadema. Kwa mantiki hiyo uchaguzi wa mwaka huu usiichukuliwe kirahisi hata kama upinzani hauna nguvu kubwa.

Mgombea wake, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwajibu wanaohoji kwanini chama chake kinatumia nguvu kubwa licha ya upinzani kuonekana dhaifu:

“Waswahili wanasema anayedharau mwiba ukimchoma mguu unaota tende. Sasa usisubiri mpaka uchomwe na msumari, hata mwiba lazima uushughulikie.”

Kauli hii inatoa picha kwamba CCM bado inaliona jukumu la kampeni kwa wananchi kama jambo la msingi, bila kujali ukubwa au udogo wa changamoto kutoka kwa wapinzani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *