Zaidi ya viongozi 50 wa Ulaya wamekutana mjini Copenhagen, Denmark, kujadili vita vya Ukraine na mustakabali wa usalama wa bara hilo, wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akitafuta msaada zaidi kutoka kwa washirika wake wa karibu.
Mkutano huo unafanyika chini ya ulinzi mkali baada ya matukio ya ndege zisizojulikana kuonekana juu ya anga la Denmark, jambo lililoongeza hofu ya shambulizi kutoka Urusi.
Zelensky anatarajiwa kutumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa msaada wa Ulaya, kufuatia uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha msaada wa kifedha na kijeshi kwa Kyiv.
Kwa upande mwingine, viongozi wa Ulaya wanaona uzoefu wa kijeshi wa Ukraine kama nyenzo muhimu katika kujenga “ukuta wa ndege zisizo na rubani” ili kuzuia mashambulizi ya Urusi barani humo.
Shinikizo limeongezeka baada ya kuongezeka kwa matukio ya ndege za Urusi kuingia katika anga za Estonia na Poland, hali ambayo imeongeza hofu ya vita kusambaa zaidi ya mipaka ya Ukraine.
Ulaya yajadili msaada wa kifedha na usalama
Katika mazungumzo ya siku ya kwanza, viongozi wa Umoja wa Ulaya walijadili pendekezo la kutumia mali zilizozuiwa za Urusi kufadhili mkopo wa euro bilioni 140 kwa Ukraine.
Wanaounga mkono pendekezo hilo wanasema ni haki Urusi ibebe gharama za uharibifu iliosababisha, badala ya walipa kodi wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, alisema msaada kwa Ukraine ni “uwekezaji wa moja kwa moja katika usalama wa Ulaya” na akasisitiza haja ya ufadhili wa muda mrefu kwa jeshi la Kyiv.
Ubelgiji, ambako mali nyingi za Urusi zimehifadhiwa, bado inauliza maswali kuhusu jinsi mpango huo unavyoweza kutekelezwa bila mzigo mkubwa wa kifedha kwake pekee.
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, alisema mazungumzo yataendelezwa ili kuhakikisha mzigo unagawanywa sawasawa miongoni mwa nchi wanachama wote.
Changamoto za Hungary na uanachama wa Ukraine
Zelensky alitoa wito kwa Umoja wa Ulaya kutimiza ahadi zake kuhusu kuikaribisha Ukraine katika uanachama wa jumuiya hiyo, lakini Hungary imeendelea kuweka pingamizi.
Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban, alisema wazi kuwa Ukraine haina nafasi ya kujiunga na EU kwa sasa, akionya kuwa hatua hiyo italeta vita na kuongeza gharama kubwa kwa Ulaya.
Orban pia amekataa kuacha kununua mafuta na gesi kutoka Urusi, akisema nchi yake haina njia nyingine kutokana na kutokuwa na pwani.
Zelensky, kwa upande wake, aliwaonya viongozi wa Ulaya kwamba kuchagua urafiki na Urusi badala ya mshikamano na Marekani na Ulaya kutawagawa na kudhoofisha usalama wa bara lote.
Kwa sasa, mustakabali wa Ukraine ndani ya EU na nguvu ya mshikamano wa Ulaya dhidi ya Urusi utaendelea kuamuliwa kupitia vikao hivi, huku Copenhagen ikibaki kitovu cha mjadala wa usalama wa bara.