Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeainisha kuwa kikosi hicho kipya kwa ajili ya Haiti kitakuwa na wafanyakazi wasiozidi 5,500 wakiwemo wanajeshi na maafisa wa polisi tofauti na kikosi maalumu cha sasa chenye maafisa 1,000 wa polisi pekee, wengi wao kutoka Kenya.

Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Mike Waltz amesema azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  limeonesha kuwa jumuiya ya kimataifa sasa inagawana mzigo kukabiliana na hali mbaya ya usalama inayoikabili Haiti. Zaid amesema, “Kupitishwa kwa azimio hili kunatoa matumaini kwa Haiti. Ni matumaini ambayo yamekuwa yakipotea kwa kasi wakati magenge ya magaidi yakijitanua, kufanya ubakaji, kupora na kuwatisha watu wa Haiti.”

Kwa upande wake Mjumbe maalumu wa Haiti katika Umoja wa Mataifa Ericq Pierre amesema kupitishwa kwa azimio la kuanzisha kikosi hicho kipya ni uamuzi muhimu utakaobadilisha mwelekeo wa mapambano ya nchi yake dhidi ya changamoto kubwa inayoikabili.

Naye mwakilishi wa Ufaransa kwa Umoja wa Mataifa Jérôme Bonnafont, ameeleza kuwa juhudi  zilizochukuliwa na Jumuiya ya Kimataifa hazina budi kuambatana na dhamira mpya katika kusaidia mchakato wa mabadiliko ya kisiasa. Amefafanua zaidi akisema kurejesha taasisi za kidemokrasia na utawala wa sheria ni hatua muhimu katika kukomesha mzozo mpana unaolikabili taifa la Haiti.

Ofisi maalumu ya kukisaidia kikosi kipya Haiti kuundwa Umoja wa Mataifa

Nguvu iliyoongezwa ya kikosi hicho imeambatana na kuundwa kwa ofisi ya kukisaidia ndani ya Umoja wa Mataifa pendekezo lililotolewa miezi kadhaa iliyopita na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Ofisi hiyo itatoa msaada wa Kifedha na vifaa unaohitajika.

Baraza la Usalama UN limeazimia kuweka kikosi kipya nchini Haiti
Polisi wa Kenya wanaounda Kikosi maalumu cha Kimataifa kwa Haiti MSS mjini Port-au-Prince, Port-au-PrincePicha: Patrice NoelZUMAPRESS/picture alliance

Wiki iliyopita, Rais wa Kenya William Ruto alisema usalama wa Haiti unaweza kurejeshwa kama kukiwa na rasilimali zinazohitajika, vifaa vya kutosha na  idadi sahihi ya wafanyakazi katika kikosi maalumu cha kukabiliana na magenge ya uhalifu nchini humo.

Nchi hiyo masikini zaidi Amerika imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa utulivu wa kisiasa kwa miongo kadhaa. Katika mwaka mmoja uliopita imekumbwa na ongezeko la vurugu za magenge ya uhalifu hasa mara baada ya shambulio lililochochea kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Ariel Henry.

Nafasi yake ilichukuliwa na baraza dhaifu la mpito lililopewa jukumu la kuandaa uchaguzi ifikapo Februari 26 mwaka ujao. Uchaguzi wa mwisho nchini humo ulifanyika mwaka 2016.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *