Mwaka 2006, Jack Dorsey alipozindua mtandao wa Twitter, sasa X, alidhani utatumika kutuma ujumbe mfupi kati ya marafiki. Lakini leo, mtandao huo umegeuka kuwa nyenzo kubwa ya kisiasa duniani.
Hali hii inajidhihirisha Tanzania, inapoelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani Oktoba 29. Kampeni, hoja na mijadala sasa inahamia kwenye mitandao kama X, TikTok, Instagram, Facebook na Telegram.
Vuguvugu la kisiasa kuhamia kwenye mitandao ya kijamii limechochea hoja kubwa: je, majukwaa haya yanaweza kuhamasisha mabadiliko na kuathiri maamuzi ya kisiasa katika uchaguzi mkuu?
DW imezungumza na mtaalamu wa masuala ya kidijitali, Kelvin Massai, ambaye ameeleza namna mitandao ya kijamii inavyoweza kubadili upepo wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2025.
Massai anaeleza kuwa kila jukwaa lina nguvu yake: “Instagram ni picha, YouTube ni video, Twitter ni mijadala ya ‘spaces’, na TikTok imejaa matangazo ya moja kwa moja. Uhamasishaji utategemea namna kila mtu anavyotumia jukwaa lake.”
Nguvu ya mitandao kwenye uchaguzi
Ripoti ya mwaka 2020 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha kulikuwa na watumiaji milioni 29.8 wa intaneti. Takwimu hizi zinaendana na ripoti za waangalizi wa uchaguzi waliobainisha ongezeko la matumizi ya mitandao na wanasiasa.
Wananchi hutumia majukwaa haya kuibua hoja za kisiasa, huku wagombea wakiyatumia kuchunguza upepo wa kisiasa na kubadili mikakati yao kwa haraka.
Katika kampeni za lala salama, mitandao hii imegeuka kuwa daraja kati ya wagombea na wapiga kura, ikirahisisha mawasiliano na kuboresha uwakilishi wa hoja za wananchi.
Profesa Wetengere Kitojo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, anasema mitandao imekuwa kipaza sauti cha wananchi wanaodai haki, demokrasia na usawa.
“Mitandao inawapa wananchi nafasi ya kuzungumza bila hofu, mara nyingi kwa kutumia majina ya kificho. Ni jukwaa huru kuliko mikutano ya hadhara,” alisema Kitojo.
Changamoto na matarajio ya baadaye
Hata hivyo, watumiaji wa mitandao wanalalamika kuhusu changamoto, ikiwamo kufungwa kwa majukwaa fulani wakati wa uchaguzi. William Kasembe, mtumiaji wa X, anasema mitandao huchambua mambo ambayo vyombo vikuu vya habari husita kuyasema.
“Kuna mambo fulani mainstream media wanayakwepa, lakini mitandao inayaweka wazi. Hata kama haitaleta matokeo makubwa sasa, katika chaguzi zijazo itawapa wananchi elimu zaidi,” alisema Kasembe.
Pamoja na fursa zinazotolewa na majukwaa haya, hatari ya upotoshaji na habari za uongo inaendelea kuwa changamoto. Wataalamu wanasema inahitaji umakini wa watumiaji kutofautisha kati ya habari sahihi na propaganda.
Serikali na wadau wa uchaguzi pia wanakumbushwa kwamba mitandao ni sehemu muhimu ya mjadala wa kisiasa, na kufungwa kwake wakati wa uchaguzi kunaweza kudhoofisha imani ya wananchi katika demokrasia.
Kadri Oktoba 29 inavyokaribia, swali kubwa linasalia: je, nguvu ya kura itaamuliwa majukwaani na mikutanoni, au sasa maamuzi ya Watanzania yatachochewa zaidi kwa “like”, “share” na mijadala ya mtandaoni?