
MSICHANA huyo akaongeza:
“Mimi nimeshawekwa ndani zaidi ya mara tano kutokana na biashara yangu ya gongo. Mara mbili nimeshinda kesi na mara tatu nimelipa faini. Kama safari hii watanifunga potelea mbali.”
Baada ya kunihubiria maneno yake akaniuliza:
“Haya, tuambie mwenzetu, umekamatwa kwa kosa gani?”
Kwa vile nilikuwa nimefadhaika sana na sikuwa na uzoefu wa kuwekwa ndani, sikutaka kuyatoa yaliyokuwa moyoni mwangu. Nikamwambia:
“Nitakuambia baadaye; niachie kwanza maana nimevurugwa.”
“Usijali. Tuko pamoja. Utachangamka tu; si upo na wenzako! Una wasiwasi gani?” akaniambia. Maneno yalikuwa yakimtoka kama chiriku.
Kama kweli alikuwa akiuza gongo, hilo gongo lilikuwa limeshamuathiri kiafya, kiakili na kisaikolojia. Maneno aliyokuwa akiropoka yalionyesha hakuwa mzima sawasawa.
Haikupita hata nusu saa wakaingizwa wasichana wengine wawili. Yule mwanamke akawadaka.
“Wadogo zangu vipi?”
“Poa tu,” mmoja akamjibu.
Alipoona mwingine hakujibu akamtazama kwa macho makali.
“Dogo mbona uko kimya?”
Yule msichana aliendelea kubaki kimya. Punde tu nikaona analia.
“Mna matatizo gani?”
Yule mwenzake akaeleza kuwa wale walikuwa ni mtu na wifi yake.
“Huyu ni mke wa mdogo wangu. Mume wake hasa ndiye mwenye kesi. Yeye amekamatwa kwa sababu mume wake amekimbia dhamana,” akaeleza.
“Amekimbia dhamana ya kesi gani?”
“Amekimbia dhamana ya kesi ya wizi wa kuaminiwa.”
“Na wewe una kesi gani?”
“Ni hiyo hiyo. Mimi ndiye niliyemdhamini huyo kaka yangu. Nilimdhamini jana na akatakiwa aripoti hapa kituoni leo lakini hakufika na hajulikani aliko.”
“Ameiba kiasi gani?”
“Hajaiba. Ila wanasema ni wizi wa kuaminiwa.”
“Ndiyo. Huo wizi ni wa kiasi gani?”
“Milioni tatu.”
“Kesi ndogo sana. Huyo mdogo wako aliyekimbia ni mpumbavu sana. Kesi kama hiyo kwangu mimi ni ndogo sana. Wizi wa kuaminiwa maana yake nini? Mimi nitakanusha tu na sitapatikana na hatia kwa sababu ninajua kuzungumza.”
Wakati stori zikiendelea humo mahabusu, alikuja polisi mmoja mwanamke akafungua lango la mahabusu na kuniita.
Nikainuka na kumfuata. Alifunga lango kisha akaniambia:
“Twende.”
Alinipeleka katika chumba kimoja ambako nilimkuta mume wangu Sufiani akiwa pamoja na askari niliyemfahamu kwa jina la Sajin Meja Robert.
Polisi hao walikuwa wamepata ushahidi kuwa siku ile lilipotokea tukio la kuuawa Shefa, mume wangu Sufiani hakuwa amekwenda safari kama alivyoniaga, bali alikwenda kulala gesti jambo ambalo lilisababisha ashukiwe kwamba ndiye aliyekwenda kumuua Shefa usiku.
Licha ya Sufiani kukiri mwenyewe kulala gesti siku ile, alikataa kuhusika na mauaji ya Shefa.
“Mimi nakubali kwamba nililala gesti lakini sikubali kwamba nimemuua Shefa. Kwanza nilikuwa sijui kama Shefa alikuja nyumbani kwangu,” Sufiani akajitetea.
“Sasa kwa nini ulidanganya kwamba siku ya tukio ulikuwa safarini?” aliulizwa na yule polisi.
Sufiani hakuwa na la kujibu. Kwa upande wangu tayari alikuwa ameshanitia shaka zaidi. Nikahisi kwamba ni yeye aliyenizunguka na kuja nyumbani usiku wa manane na kumuua Shefa. Hakuwa na sababu yoyote ya kulala gesti na kuja kunidanganya mimi.
“Wewe uliona ni sahihi kweli kunitia katika matatizo?” Hapo hapo nikamkoromea kwa sauti ya juu.
“Lakini mimi sijamuua Shefa. Uliyekuwa naye chumbani ni wewe. Wewe ndiye ueleze nani alimuua?” Sufiani akaniambia kwa macho makavu.
Sasa tulikuwa kama watu tunaotupiana mpira.
“Mimi ndiye mke wako na nyumbani kwangu ndiyo kwako, kwa nini ulinidanganya kuwa unakwenda safari kumbe unakwenda kulala gesti. Kwa nini hutaki kujibu swali hilo?”
Sufiani alizidi kuhamaki.
“Yaani mke wangu unataka kuniingiza mimi katika matatizo yako wewe na Shefa? Kwanza ilikuwaje ulale na Shefa nyumbani kwangu wakati mimi sipo?”
“Na wewe ulikuwaje ulale gesti wakati mimi nipo?”
“Sasa ninachosema mimi ni kuwa mauaji ya Shefa hayanihusu, yanakuhusu wewe. Wewe ndiyo ueleze Shefa ameuawa na nani?”
“Wewe ndiye uliyemuua Shefa!”
“Jamani, msibishane. Nyote tunaweza kuwapeleka mahakamani na kuwashitaki. Mahakama ndiyo itatoa uamuzi wa nani muuaji,” yule Sajin Meja akatuambia.
“Afande, mimi naona Sufiani ndiye aliyemuua marehemu baada ya kumfumania. Huyu msichana hawezi kumuua hawara yake tena nyumbani kwake,” kuna polisi aliyeingia mle ofisini na kuyadakia yale maneno.
Sajin Meja Robert akamtazama Sufiani.
“Hebu sogea hapa unipe maelezo yako,” akamwambia.
Sufiani alisogea karibu na meza ya Sajin Meja huyo.
Vile vile alivyosimama alianza kuhojiwa.
Kwanza aliulizwa jina lake, umri wake na kazi anayofanya. Baada ya hapo akatakiwa aeleze siku ya lile tukio alikuwa wapi.
“Nimeshasema kwamba nilikuwa hapa hapa Tanga,” Sufiani akajibu.
“Mke wako alikuwa na taarifa kama ulikuwa hapa Tanga?”
“Hapana. Yeye nilimuaga ninakwenda Dar.”
“Kwanini ulimuaga kuwa unakwenda Dar halafu hukwenda Dar, ukaenda kulala gesti?”
Sufiani akanyamaza kimya.
“Utakuwa na hoja ya kupinga nikikwambia kwamba ulilala gesti kwa nia ya kurudi usiku nyumbani kwako ili umuue Shefa?”
“Mimi nalipinga kabisa suala la mauaji. Sikurudi nyumbani kwangu kumuua Shefa. Kwanza nilikuwa sijui kama Shefa alikuja nyumbani kwangu na pia nilikuwa sijui kama mke wangu alikuwa na uhusiano na Shefa.”
“Sasa kwani ulimdanganya mke wako kuwa unakwenda Dar halafu ukaenda kulala gesti? Hilo ndilo linalotupa hoja kwamba wewe ndiye muuaji. Yule alikuwa mgoni wako, kwa hivyo ulipomuona ulihamaki na kumuua. Mke wako hana sababu za kumuua Shefa.”
Sufiani akatikisa kichwa.
“Nashangaa kwamba hii kesi mnataka kunipa mimi. Sitakubali.”
“Si lazima ukubali. Sisi tutakupeleka mahakamani hata kama hutakubali. Ni watuhumiwa wachache sana wanaokubali makosa wakiwa mikononi mwa polisi lakini tunawapeleka mahakamani hivyo hivyo,” Sajin Meja huyo alimwambia Sufiani kisha akaongeza:
“Hata hao wanaokubali makosa wakiwa mikononi mwa polisi, wakifikishwa mahakamani wanaweza kubadilika na kuamua kukana makosa. Ni hiyari ya mtu kukiri kosa au kukana kosa lakini mahakama inaangalia uzito wa ushahidi hata kama ni wa kimazingira.”
“Lakini jamani, kwa nini mmeamua kunigeuzia kibao mimi? Kuwaambia kuwa nililala gesti imekuwa nongwa. Gesti si unaweza kulala na mwanamke. Au mnataka niseme kuwa nililala na mwanamke? Kweli ningeweza kumwambia mke wangu kuwa niko gesti na mwanamke?”
“Hayo maelezo sasa utabaki nayo hadi utakapofikishwa mahakamani, utakwenda kujitetea mwenyewe.”
Sufiani alinitazama kwa jicho la uchungu kisha akatikisa kichwa kusikitika.
Ghafla nikamuona Inspekta Amour akiingia humo ofisini. Alikuwa amefuatana na watu wawili. Wote niliwatambua. Alikuwa ni yule mlinzi aliyeachiwa gari na Shefa usiku ule aliouawa na mtu wa pili alikuwa kijana wa bodaboda aliyekuwa na Raisa siku ile waliponifuma makaburini nikiutupa mwili wa Shefa.
Nilipowaona nilishtuka. Hao wote walikuwa na maelezo yanayoweka mazingira mabaya kwa upande wangu.
Mlinzi alimuona Shefa akiingia nyumbani kwangu usiku ule aliouawa na hakumuona alipotoka. Na kijana wa bodaboda ambaye alikuwa pamoja na Raisa, aliniona usiku ule nilipoutupa mwili wa Shefa makaburini. Ingawa hakuiona sura yangu, ilisemekana aliziona namba za gari langu.
Hata hivyo, hayo yote nilishayabainisha mimi mwenyewe mbele ya polisi. Sasa sikujua waliletwa pale kama mashahidi au vipi.
“Afande, muuaji tumeshampata!” Sajin Meja Robert akamwambia Amour alipomuona akiingia.
Amour alionekana kuyapuuza maelezo yake.
“Unasema mmempata muuaji, yuko wapi?” akamuuliza.
“Mume wa mtuhumiwa, alilala gesti siku ile kwa ajili ya kwenda kumfumania mke wake. Unadhani unapomkuta rafiki yako na mke wako nyumbani kwako, utafanya nini?”
“Utamuua,” nikajibu mimi.
“Mimi sijaua. Kama mnamtaka muuaji ni mke wangu,” Sufiani akasema. Aliamua kunishindilia waziwazi alipoona sikuwa upande wake.
Inspekta Amour akatikisa kichwa.
“Sufiani si muuaji,” akasema.
“Kwanini? Unataka useme muuaji ni mke wake?” Sajin Meja akamuuliza kwa pupa.
“Muuaji nimeshamkamata na nina ushahidi kamili. Nina ushahidi wa maelezo na pia nina ushahidi wa kitaalamu ambao hauwezi kupingika.”
Sote tukashituka.
Macho yetu sote yakaenda kwa kijana wa bodaboda kisha yakaenda kwa yule mlinzi.
Kwa mawazo yangu pale sikuona muuaji.
“Hawa ni kina nani?” Sajin Meja akauliza akiwaonyesha wale watu waliokuja na Inspekta Amour.
“Huyu ni kijana anayeendesha bodaboda na huyu mwenzake ni mlinzi wa nyumba ambayo Shefa aliacha gari lake usiku aliouawa.”
“Sasa hawa wanahusikaje na mauaji?”
“Nataka uwasikilize, muuaji yupo hapa hapa.”
Sajin Meja akaguna. Mimi pia niliguna. Niliona Inspekta huyo alikuja na mambo mapya.
Lakini Sufiani alikuwa amewakodolea watu hao macho ya matumaini.
“Hapa sioni muuaji zaidi ya Sufiani ambaye anataka kumuangamiza mke wake,” Sajin Meja akamwambia Inspekta Amour.
“Utamuona muuaji hapa hapa dakika chache tu zijazo. Na si kumuona kwa macho tu bali utajua ni kwanini aliua.”
Inaendelea…