Hapa ndipo kilipo Kituo cha Kukabiliana na Uhamiaji (MRC), kinachoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), ambacho hutoa nafasi adimu ya kupata usalama na msaada kwa wale wahamiaji wanaowasili baada ya safari zilizogubikwa na njaa, uchovu na kupoteza wapendwa.
Miongoni mwa watoa huduma kwenye kituo hicho ni Kadija Ahmed, Muuguzi Mwandamizi wa Afya ya Wahamiaji. Kwa zaidi ya miaka minne,amejitolea kutoa huduma, huruma, na matumaini kwa wahamiaji.
Muuguzi anayeleta matumaini
Safari ya Kadija katika kazi za kibinadamu imeanza baada ya kuondoka katika sekta binafsi ya afya. Alianza kama muuguzi msaidizi katika kituo cha Obock, akikumbuka hali ya kutokuwa na raha siku yake ya kwanza na ushupavu usiotarajiwa ambao ameushuhudia kwa wahamiaji ambao amewahi kukutana nao.
“Kilichonigusa zaidi ni ustahimilivu wao,” amesema. “Licha ya magumu yasiyoweza kufikirika,walibeba ujasiri usio wa kawaida.” Kukutana huko kwa mara ya kwanza ndiyo ukawa mwanzo wa kuunda wito wake.
Huko Obock, Kadija anasimama kimya, akiwa na nguvu na huruma, na miaka ya kujitolea kwa walio hatarini zaidi.
Kadija amejiunga rasmi na IOM mwaka 2018 na tangu hapo amebaki Obock, akisaidia kuongoza huduma za afya na kushirikiana katika shughuli za msaada wa kisaikolojia chini ya usimamizi wa wanasaikolojia waliobobea.
Sasa anaratibu huduma za matibabu na anachangia kwenye programu za Msaada wa Afya ya Akili na kisaikolojia(MHPSS), huku pia akifundisha wataalamu wa afya ili kuongeza uwezo wa kutoa huduma kwa wahamiaji walioko njiani.
Obock: Lango hatari kwa safari
Kwa miaka mingi, Obock imekuwa lango kuelekea Ghuba ya Aden kwa makumi ya maelfu ya wahamiaji, wengi wao kutoka Ethiopia, wanaojaribu kuvuka kuelekea Rasi ya Uarabuni—na wakati mwingine kurudi tena.
Njia hiyo inajulikana kwa kuwa na joto kali, ukosefu wa maji, ajali za meli, na vurugu, na kuifanya kuwa miongoni mwa njia hatari zaidi duniani. Katikati ya hatari hizi, kituo cha MRC cha Obock kinachoendeshwa na IOM kimekuwa msaada muhimu kwa wahamiaji tangu mwaka 2011, kikitoa makazi, chakula, huduma za afya na msaada wa kisaikolojia.
Doria za kijumla hupanua huduma hizi hadi jangwani na ufukweni, zikisaidia mara nyingi zikiwa kama watoa huduma wa kwanza na wa pekee wakati wahamiaji wanapozirai kutokana na uchovu au manusura wa ajali za baharini.
Ishara ndogo ya uponyaji
Katika moja ya huduma hizo za doria, Kadija na wenzake huwafikia wahamiaji kwenye njia hatari wakitoa msaada wa haraka wa kiafya. “Kila mtu anayepita kwenye lango la kituo hubeba simulizi juu ya kusalia hai,”amesema Kadija.
Katika doria tembezi karibu na Obock, Kadija na wafanyikazi wengine wa IOM wanawafikia wahamiaji kwenye korido hatari kwa huduma ya haraka ya matibabu.
Kwake dhamira si tu kuponya, bali pia kurudisha heshima na kusaidia kujenga upya maisha. Miongoni mwa hadithi nyingi alizoshuhudia ni ile ya Aïcha, msichana mdogo ambaye alifika kituoni na familia yake baada ya safari ya maafa,hii imebakia moyoni mwake.
“Wakati Aïcha alipokuja mara ya kwanza, alikuwa kimya. Hakumwangalia mtu yeyote machoni na hakuongea neno. Wazazi wake wakaeleza kwamba alikuwa ameshuhudia vurugu njiani wakati wa safari yao,” Kadija anakumbuka.
Kwa wiki kadhaa, Aïcha amekuwa kimya. Kisha, siku moja, Kadija wakati akiwa anachora nyumba kwenye karatasi, msichana huyo alichukua rangi ya kijani na kuchora mmea mdogo pembeni.
Katika MRC, wafanyakazi wa IOM kama vile Kadija wanasaidia watoto wahamiaji na watu wazima katika kujenga uwezo wa kustahimili ustahimilivu kupitia sanaa na uchezaji baada ya uzoefu mgumu.
Ishara hiyo ndogo ikawa mwanzo wa uponyaji. Baadaye mmea ulikua na kuwa mti, kisha mandhari. Maneno yakifuata. Kicheko kikarejea. Hatimaye, Aïcha akakimbia katika uwanja wa kituo, akicheza na watoto wengine. Akibeba kumbukumbu ya maumivu, lakini pia akaanza kurudisha kumbukumbu za enzi ya utoto wake.
Kwa Kadija, mmea ule mdogo wa kijani umekuwa alama ya kumbukumbu isiyofutika ya namna nafsi iliyojeruhiwa inaweza kuanza tena. “Wakati mwingine, mtu huhitaji muda, mazingira salama na rangi tu ya kuchora ili kuanza upya,” amesema.
Matumaini mapya na mafunzo ya utu
Kazi ya Kadija katika MRC imejaa nyakati kama hizo – kwake, kila tabasamu jipya la mhamiaji ni hadithi ya kuzaliwa upya. “Sehemu yenye thamani zaidi ya kazi yangu ni kuona nyuso zikimetameta tena baada ya kupitia mateso makali.” Zaidi ya kusaidia wahamiaji, kazi hii pia imemfundisha yeye binafsi uvumilivu, shukrani na heshima ya kina kwa utu.
“Kazi hii ni zaidi ya tiba ya kawaida,” akatafakari. “Ni kuhusu kuwawezesha wahamiaji, kuwarudishia utu na kuwasaidia kuamini tena katika mustakabali wao.”