Trump aliandika Jumapili kupitia mtandao wake wa Truth Social “Nimeambiwa kuwa awamu ya kwanza inapaswa kukamilika wiki hii, na nawasihi wote WAHARAKISHE,” Ujumbe huo ulitolewa dakika chache kabla ya muda wa mwisho alioutangaza Ijumaa kwa kundi la Hamas kukubali mpango wake wa amani.  Hamas ilikubali baadhi ya vipengele vya mpango huo Ijumaa, lakini ikaomba mazungumzo zaidi.

Haijafahamika wazi iwapo Trump bado anazingatia muda huo wa mwisho, kwani hakulizungumzia katika ujumbe wake wala kwa waandishi wa habari Jumapili jioni. Wawakilishi wa Israel na Hamas wanatarajiwa kukutana nchini Misri leo kujadili mpango wa amani uliopendekezwa na Trump.

Kuachiliwa mateka na wafungwa

Mzozo wa Mashariki ya Kati - Tel Aviv
Familia za mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza wakishikilia picha zao na kupiga kelele wakati wa maandamano ya kutaka waachiliwe, huko Tel Aviv, Israel, Desemba 30, 2023.Picha: Ariel Schalit/AP/dpa/picture alliance

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema mazungumzo ya awali, yatakayofanyika kupitia wapatanishi, yatalenga kufikia makubaliano ya kuwaachilia mateka waliobaki Gaza kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina walioko Israel.

Trump ameongeza kuwa “kumekuwa na mazungumzo chanya sana na Hamas, na nchi mbalimbali duniani mwishoni mwa wiki hii, kuhusu kuwaachilia mateka, kusitisha vita vya Gaza, lakini muhimu zaidi, kufikia amani ya muda mrefu iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.”

Wajumbe wafika Misri

Netanyahu amesema ujumbe wa Israel utaondoka kuelekea Misri Jumatatu kwa ajili ya mazungumzo hayo, yanayoanza siku moja kabla ya kumbukumbu ya miaka miwili tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023 lililoanzisha vita.

Mkuu wa ujumbe wa Hamas, Khalil al-Hayya, aliwasili Misri Jumapili usiku, kwa mujibu wa taarifa ya kundi hilo. Ikulu ya White House imesema Trump pia ametuma wajumbe wawili nchini Misri, Jared Kushner na mpatanishi wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff.

Wanamgambo wa Hamas waliteka mateka 251 wakati wa shambulio la Oktoba 7, ambapo 47 bado wako Gaza. Jeshi la Israel linasema 25 kati yao wamefariki.

Kwa mujibu wa mpango wa Trump, Israel inatarajiwa kuwaachilia wafungwa wa Kipalestina 250 waliopatikana na hukumu ya maisha, pamoja na zaidi ya wafungwa 1,700 kutoka Gaza waliokamatwa wakati wa vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *