Chanzo cha picha, CCM
Katika siasa za Chama Cha Mapinduzi (CCM), mojawapo ya maswali ambayo mgombea mwenza wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano hutakiwa kujibu ni moja; ni lipi hasa analileta mezani?
Kwamba zaidi ya umaarufu wa chama, ni sifa zipi za mgombea mwenza zitaongeza nguvu ya ushawishi, kura na haiba ya mgombea wa urais? Kujibu swali hili, inabidi turudi nyuma kidogo.
Katika mazungumzo yangu na baadhi ya makada wakongwe wa CCM, wakati Baba wa Taifa, Julius Nyerere, na wenzake wakiwaza kuhusu nafasi ya mgombea urais na mgombea mwenza, mambo kadhaa yalikuwa vichwani mwao.
Mosi ni kuwa utaratibu wa kupokezana urais kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na kupunguza vita vya kuwania urais ndani ya chama. Kwa maana hiyo, wakati Dkt. Omar Ali Juma akiteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Benjamin Mkapa mwaka 1995, ilifikiriwa kuwa angekuwa mrithi wake mwaka 2005.
Kifo cha ghafla cha Dkt. Omar – Mzanzibari mwenye asili ya Pemba Julai 4, 2001, kilivuruga mpango huu wa awali. Wazo lilikuwa kwamba Omar angemteua mwanasiasa kijana kutoka Bara kuwa mgombea mwenza wake mwaka 2005, ambaye angemrithi mwaka 2015 akiwa amejifunza kama Makamu wa Rais kwa miaka kumi.
Hata hivyo, jambo moja lilipaswa kuwa dhahiri. Kwamba mgombea mwenza alipaswa kuwa na sifa zote za kuwa Rais, mwenye nguvu na ushawishi kutoka upande wake (Bara au Zanzibar) na atayemwongeza nguvu mgombea urais.
Katika muktadha huu, ni rahisi kufahamu ni sababu zipi zimemfanya Rais Samia Suluhu Hassan kumpendekeza Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wake.
Nchimbi ni mwanasiasa mwenye ushawishi ndani ya CCM, ana umri sahihi wa kujifunza na kukua zaidi kiuongozi, anazijua siasa za upande ambao hatoki mgombea urais na ni mtu wanayefahamiana na kuelewana kwa takribani miongo mitatu.
Rais Samia na Nchimbi wana sifa tofauti za kihistoria, kiutendaji na kihaiba, ambazo zinafanya iwe rahisi kujua sababu za muungano huu hu.
Historia ya CCM ya mgombea na mgombea mwenza
Walau katika miaka 30 iliyopita, CCM imekuwa na utaratibu wa kuchagua mgombea urais na mgombea mwenza wake wenye sifa za tofauti – kwa maana kwamba kwa sifa za pamoja zinakuwa nyingi kuliko sifa za mmoja mmoja.
Mwaka 1995, Mkapa alikuwa mgombea mwenye sifa za utendaji kuliko uanasiasa. Ingawa alikuwa mwana CCM, alijipambanua zaidi kama mtendaji na mjuvi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa kwa kuzingatia historia yake ya kimajukumu.
Ingawa Omar alikuwa amesomea masuala ya udaktari wa mifugo, historia yake kubwa ilikuwa ni kwenye majukumu ya kisiasa yaliyomfikisha kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) – wadhifa wa pili kimamlaka visiwani humo.
Tiketi ya Mkapa na Omar ilikuwa na uanasiasa, uanadiplomasia, ufanisi, ubobezi na ukada wa CCM usio na shaka.
Hali ilikuwa hivyo kwa Jakaya Kikwete na Dkt. Ali Mohamed Shein. Jakaya alikuwa mwanasiasa wakati Shein – daktari wa binadamu, akijipambanua kama mtendaji. Jakaya hakuwa mwanasiasa pekee lakini mwerevu wa masuala ya diplomasia na mjuzi wa siasa za Tanzania.
Hali ilikuwa hivyo pia wakati wa urais wa Dkt. John Magufuli. Magufuli. Yeye alijipambanua kama mtendaji zaidi kuliko mwanasiasa. Samia kama mgombea mwenza alikuwa analeta utulivu, uanasiasa na ukada wa CCM. Mwaka 2015, Samia alikuwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 10 ndani ya CCM kama mjumbe wa NEC na Kamati Kuu – nafasi ambazo Magufuli hakuwahi kuzishika katika maisha yake ya kisiasa.
Kifo cha Magufuli kilimpa nafasi Dkt. Philip Mpango – mchumi wa kiwango cha juu na mzoefu wa kusimamia mipango ya nchi akiwa Katibu Mtendaji wa Tume ya mipango, kuwa Makamu wa Rais kuchukua nafasi ya Samia aliyepanda kuwa rais. Mpango ni mtendaji ambaye alipewa nafasi hiyo katika wakati ambao dunia ilikuwa inapita kwenye kipindi kigumu kiuchumi kutokana na janga la UVIKO-19.
Uteuzi wa Nchimbi ambaye ni mtendaji kichama, unaweka tena fursa ya kuwa na rais mwanasiasa na makamu mtendaji – ingawa tofauti na Shein, Mkapa na Mpango ambao walikuwa watendaji nje ya chama – Nchimbi ni mtu wa ndani ya chama.
Kuna sifa nyingine ya Nchimbi ambayo Mpango hakuwahi kuwa nayo. Sifa hiyo ni ukweli kwamba yeye ni mwanasiasa mwenye ushawishi ndani ya chama na jamii ambao Mpango na Shein hawakuwahi kuwa nao. Nchimbi amewahi kuwa balozi na hivyo ana uelewa wa masuala ya uhusiano wa kimataifa ambayo watangulizi waliyopita hawakuwa nayo.
Nguvu ya Kanisa
Kuna tofauti nyingine baina ya Mpango na Nchimbi ambayo Rais Samia na CCM wameizingatia kwenye kumfanya mbunge huyo wa zamani wa Songea Mjini kuwa mgombea mwenza.
Ni jambo linalofahamika nchini Tanzania kwamba Kanisa Katoliki ni miongoni mwa taasisi zenye nguvu na ushawishi mkubwa katika siasa za taifa hilo. Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na hali ya sintofahamu baina ya Serikali ya CCM na Kanisa hilo.
Ingawa Mpango ni Mkatoliki kama Nchimbi – wadadisi wa siasa za Tanzania wanamwona kama mtu ambaye ni muumini zaidi wa kanisa kuliko mtu mwenye ushawishi. Nchimbi, kwa upande mwingine, anatajwa kama mwanasiasa muumini lakini mwenye ushawishi ndani ya kanisa hilo.
Bila shaka, wakati Rais Samia anapendekeza jina la Nchimbi kwa Kamati Kuu, alikuwa anajua amepata mtu ambaye anaweza kumwachia kazi ya kuboresha mahusiano baina ya serikali, chama na kanisa na mambo yakaenda vema.
Watanzania huwa hawapigi kura zao kutokana na matakwa ya kidini au kikabila lakini kwa utamaduni, CCM huwa inalinda uhusiano wake na taasisi za kidini kwa wivu mkubwa, hususan zile zenya waumini wengi zaidi kama Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania BAKWATA.
Changamoto za Samia na Nchimbi
Chanzo cha picha, CCM
Changamoto kubwa ya tiketi hii ya Samia na Nchimbi ipo katika maeneo makubwa mawili ya kitaifa na kimataifa. Kimataifa – dunia sasa inashuhudia wimbi kubwa la wapiga kura ambao hawavitaki tena vyama vilivyodumu madarakani kwa muda mrefu.
Vyama vyote vikongwe barani Afrika – iwe ANC ya Afrika Kusini, ZANU PF ya Zimbabwe – na vyama vingine vya ukombozi vinapitia katika mazingira mgumu. Ni kama vile dunia inapita katika wimbi la mabadiliko.
Kwa maana hiyo, hata kama CCM ingemweka mwanasiasa yeyote awe mgombea urais na mgombea mwenza, bado kingepata shida kwa sababu mwenendo wa kidunia sasa ni kutaka mabadiliko. Hali hii pia inachangiwa na kuwepo wapiga kura wengi vijana ambao wanazingatia zaidi mazingira ya sasa na changamoto zinazowahusu zaidi kama ajira na kipato cha mtu mmoja mmoja, kuliko fikra na falsafa zinazolenga kujenga taifa lenye umoja na mshikamano.
Jambo lingine ni suala zima la kuibuka na kupanda kwa wanasiasa wasio wa kawaida, maarufu kwa jina la populists ambao wamekuwa mwiba mkubwa kwa vyama vinavyofuata demokrasia ya kiliberali duniani.
CCM iliwahi kunufaika na wanasiasa wa namna hii pale kilipomteua Magufuli kuwa mgombea wake wa urais mwaka 2015. Republican cha Marekani kimenufaika na Trump mwaka 2016 na miezi sita iliyopita.
Iwapo upinzani ukiwa na mgombea urais anayefuata siasa zisizo za kawaida wa aina ya Trump, Magufuli au Narendra Modi wa India, CCM inaweza kujikuta kwenye mtihani mkubwa kwa sababu Samia na Nchimbi hawafuati siasa za namna hiyo.
Changamoto nyingine kubwa ni suala zima la uwepo wa mitandao ya kijamii. Ukuaji wa matumizi ya mitandao ya kijamii unamaanisha kwamba vyama vya upinzani vitaweza kutumia mitandao – hata kama CCM itahodhi vyombo rasmi vya habari. Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2020, internet ilizimwa hivyo kuwa vigumu kupata mawasiliano ya mitandao ya kijami isipokuwa tu kwa kutumia matandao pepe wa faragha maarufu kama Virtual Private Network (VPN).
Katika taifa ambalo idadi kubwa ya vijana – ambao ndiyo kundi kubwa la wapiga kura, wanatumia mitandao ya kijamii, teknolojia inaweza kuwa mwamuzi wa mpambano baina ya Samia-Nchimbi na wapinzani wao wowote.
La mwisho ni ukweli kwamba siasa ni mchezo usiotabirika. Kati ya Agosti na Oktoba 29 mwaka huu, jambo lolote linaweza kutokea na kuharibu kila kitu ambacho sasa kinatabirika.
Kwa sasa, timu ya Samia na Nchimbi inaonekana kuwa ndiyo timu ya ushindi. Muungano wao umesheheni uzoefu, uzeefu, ukada, ubobezi na ujuzi wa ‘mizungu’ ya siasa za ndani.
Imehaririwa na Florian Kaijage.