
Zaidi ya wakimbizi 6,000 wa Sudan Kusini wameondoka katika moja ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi nchini Kenya, Umoja wa Mataifa umeliambia shirika la habari la AFP siku ya Alhamisi, wakati kupunguzwa kwa misaada kunasababisha kuongezeka kwa uhaba wa chakula.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kambi ya wakimbizi ya Kakuma kaskazini mwa Kenya ni ya pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na inahifadhi takriban watu 300,000 kutoka Sudan Kusini, Somalia, Uganda na Burundi.
Mashirika ya misaada yanatatizika, huku maandamano ya ghasia yalizuka mwezi uliopita kuhusu kupunguzwa kwa mgao kufuatia kupunguzwa kwa misaada, hatua iliyochukuliwa na Marekani na wafadhili wengine.
Sudan Kusini, ambayo iko katika hali mbaya, imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa utulivu wa miaka mingi na kwa sasa iko ukingoni mwa vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe, na kuwalazimisha wakimbizi kukimbia kuvuka mpaka.
“Tangu mwezi Januari, takriban wakimbizi 6,200 wa Sudan Kusini wameondoka Kakuma na Kalobeyei,” kambi nyingine jirani, Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Wakimbizi (UNHCR) limesema katika taarifa iliyotumwa kwa barua pepe kwa shirika la habari la AFP.
UNHCR imesisitiza kuwa ingawa vuguvugu hili lilipendekeza “mwelekeo unaoendelea,” “kuondoka hakuwezi kuhusishwa na sababu moja.”
Hata hivyo, shirika hilo limebainisha kuwa mabadiliko makubwa yalianza mwezi Julai, wakati Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilipoanza kupunguza mgao, likiainisha wakimbizi kulingana na kiwango cha madaraja manne na kuweka kikomo cha misaada kwa makundi mawili yaliyokosa fursa zaidi.
“Baadhi ya wakimbizi wameelezea wasiwasi wao kuhusu kugawanywa kwa msaada wa chakula,” UNHCR imesema, pamoja na machafuko ya hivi karibuni.